DAWASA yakabidhiwa mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe

Wizara ya Maji imekabidhi mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe (SMK) kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) baada ya kusitisha mikataba na kampuni za M.A Kharafi & Sons na Badr East African Enterprises Ltd, anaripoti Dickson Busagaga (Kilimanjaro).

Maamuzi ya Wizara ya Maji yanatokana na kusuasua kwa mradi huo kwa muda mrefu sasa huku wananchi katika maeneo ya wilaya za Mwanga,Same na Korogwe mkoani Tanga wakiendelea kukabiliwa na changamoto ya huduma ya maji.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso akiwa ameongozana na viongozi mbalimbali wakiwemo wataalamu kutoka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji wakati akitembelea maeneo mbalimbali kujionea sehemu ya mradi wa maji wa Same -Mwanga -Korogwe uliokua umesimama. Katika mradi huo ambao chanzo chake ni Bwawa la Nyumba ya Mungu,kampuni ya ukandarasi ya M.A Kharafi &Sons iliingia mkataba wa kujenga chanzo na mtambo wa kusafisha maji katika Kijiji cha Njiapanda wilayani Mwanga pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kupeleka maji hadi katika tenki la Kisangara.

Katika hafla ya kukabidhi mradi huo kwa Dawasa, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema mkataba na kampuni hiyo ulisainiwa Novemba 2014 na ulitarajiwa kukamilika Julai 16,2017 na kwamba mkandarasi amekuwa akisuasua katika utekelkezaji.

 “Hadi mkandarasi anasitishiwa mkataba Desemba 29,2020 utelezaji wa kazi hii ilikuwa imefikia asilimia 64,”amesema Aweso.

Waziri Aweso amesema, mkataba mwingine ulikuwa ni usambazaji wa maji katika mji wa Mwanga na kujenga miundombinu ya kutoa maji Kisangara hadi Kiverenge na kutoka Kiverenge hadi Mwanga mjini,kazi iliyokuwa ikifanywa na Mkandarasi Badr East African Enterprises Ltd.
 “Kama alivyo mkandarasi wa kwanza huyu naye alisuasua katika utekelezaji wa mradi, lakini pi aligushi nyaraka muhimu za kimkataba na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na hadi kufikia mwisho wa mwaka 2020 alikua amefikisha asilimia 60.

 “Wizara ninayoiongoza imechukua maamuzi magumu ya kumsimamisha mkandarasi huyu Desemba 30,2020,"ameongeza Aweso.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso akitizama moja ya chujio la maji katika mradi mkubwa wa Maji wa Same- Mwanga- Korogwe alipotembelea pamoja na wataalamu kutoka katika wizara hiyo.
Waziri wa maji Jumaa Aweso akiwa katika eneo la kupolelea maji kutizama namna ambavyo wataalamu wa ndani wanaweza kuendeleza kazi hiyo ambayo kwa sasa imekabidhiwa rasmi kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) 
Waziri wa Maji Jumaa Aweso akizungumza wakati wa hafla fupi ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa Same -Mwanga -Korogwe ,mradi ambao sasa umekabidhiwa kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA). 
 
Amesema, mkataba namba nne unahusisha kazi za usambazaji maji katika mji wa Same na kujenga matenki manne na miundombinu ya kutoa maji Kiverenge hadi Same mjini kupitia mkandarasi BADR East African Enterprises Ltd,mkataba ulionesha mkandarasi alipaswa kumaliza kazi Desemba 1,2019.

 “Ni kwa sababu hii tuliona kuwa upo umuhimu wa Serikali yenyewe kupitia taasisi yake ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) yenye uzoefu wa utekelezaji na usimamizi wa miradi mikubwa ikamilishe kazi hii,”amesema Aweso.
Baadhi ya Watendaji kutoka Wizara ya Maji wakiwa katika hafla fupi ya utekelezaji wa mradi huo ,hafla iliyofanyika katika ofisi za Mamlaka ya Maji ya Same Mwanga .
Katibu Mkuu Wizara ya Maji ,Mhandisi Anthony Sanga akizungumza katka hafla hiyo ambapo aliwanyooshea kidole wahandisi watakao suasua katika utekelezaji wa miradi ya maji kote nchini ,
Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa ,Mhandisi Cyprian Luhemeja akizungumza katika hafla hiyo ambapo amewatoa hofu wakazi wa wilaya za Mwanga na Same kuhusu huduma ya Maji na kwamba ifikapo Novemba 30 mwaka huu wateja 100 kwa wilaya ya Mwanga na wateja 100 kwa wilaya ya Same watakua wanatumia maji safi na salama.
Baadhi ya Wananchi waliohudhuria hafla hiyo wakifuatilia hotuba mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na viongozi .
Waziri wa Maji Jumaa Aweso akikata utepe kuashiria kuanza rasmi kwa utekelezaji wa mradi wa MAji wa Same -Mwanga -Korogwe muda mfupi baada ya kukabidhiwa kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).
 
“Baadhi ya kazi kama Electro-mechanical works zitafanywa kupitia wakandarasi wenye uzoefu zaidi na kazi nyingine zitatekelezwa moja kwa moja na Dawasa,”ameongeza Waziri Aweso.

 Aweso amemtaka Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja ahakikishe kuwa mradi unatekelezwa kwa wakati na kwa ubora kama ilivyo katika makabrasha ya usanifu.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso akiunganisha moja ya mabomba yaliyoanza kusambazwa katika mji wa Mwanga mara baada ya mradi huo sasa kikabidhiwa Dawasa.
Wakuu wa wilaya za Mwanga na Same Thomas Apson na Rosemery Senyamule wakishirikiana na wananchi wengine kufukia mitaro ambayo tayari bomba za maji zimewekwa.
Baadhi ya Wananchi wakishiriki katika kazi ya kujitolea kwa kufukia mtaro kulikolazwa Bomba mara baada ya mrad huo kukabidhiwa Dawasa.
Sehemu ya Mradi wa Maji wa Same Mwanga Korogwe unavyoonekana kwa juu ,mradi ambao sasa umekabidhiwa Dawasa.

Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cypriani Luhemeja amesema, kazi ya ulazaji wa miundombinu ya maji katika maeneo hayo imeanza na kwamba wananchi katika wilaya ya Mwanga na Same wataanza kupata huduma ya maji ifikapo Novemba 30, mwaka huu.

 “Kwa unyenyekevu kabisa mimi pamoja na timu yangu pamoja na bodi inayoongozwa na Jenerali Davis Mwamnyange,mkuu wa majeshi mstaafu,kazi hii tunaiweza na itakamilika tarehe 30 Novemba,ninakuomba katika ratiba zako tarehe 19 Desemba tutakualika kuja kuzindua huu mradi,”amesema Mhandisi Luhemeja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news