Gari la kusafirisha maiti lakamatwa likisafirisha madawa ya kulevya Tanga

Jeshi la Polisi mkoani Tanga limemkamata mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam, Simon Pasian Tarimo (37) akiwa amebeba mirungi bunda 1,685 ambazo ni sawa na kilogramu 133 ikiwa imehifadhiwa ndani ya mifuko sita ya salfate kwenye gari la kusafirishia maiti, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 13, 2021 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Blasius Chatanda amesema kwamba, gari hilo lilikamatwa Januari 12 mwaka huu saa nane usiku huko kwenye Kijiji cha Manga Kata ya Mkata Tarafa ya Mazingira wilayani Handeni.

Akieleza namna walivyofanikiwa kukamatwa na gari hilo amesema Askari waliokuwa doria walilishtukia na walipotaka kulisimamisha dereva akataka kukimbia na wakamkimbiza na kufanikiwa kumkamata na walimuhoji sababu za kukimbia akiwa amesimamishwa na Polisi.

Amesema baada ya hapo Askari hao walitaka kulipekua na walipolipekua gari wakakuta kwenye eneo la kuweka mwili wakakuta mafurushi sita yakiwa yamehifadhiwa mirungi ndani yake na ni eneo ambalo wakati wa kwenda lilikaa Jeneza na wakati wanarudi ndipo walipoweka mirungi.

Kamanda huyo amesema katika mahojiano na dereva huyo alisema baada ya kupelekea mwili Makanya Usangi wakati wa kurudi njiani eneo ambalo aliweka maiti akaaamua kuweka mirungi akiamini kwamba angeweza kusafiri salama asipekuliwe kwa sababu anaamini watanzania hawana utamaduni wa kukagua na kupekua magari ambayo yamebeba maiti.

Alilitaja gari la kusafirisha miili ya marehemu ambalo limekamatwa na mirungi hiyo kuwa ni lenye namba za usajili T.569 DSZ aina ya Volvo ambalo ni maalumu kwa kubebea miili ya marehemu ambalo linamilikiwa na mali ya Nuru Funeral Service iliyopo jijini Dar es Salaam.

Kamanda Chatanda amesema, mtuhumiwa huyo alikuwa akisafirisha mirungi hiyo akitokea Usangi kuelekea Jijini Dar es Salaam ambapo mbinu iliyotumika ni kuweka mfuko kwenye jokofu linalotumika kuhifadhia jeneza lenye maiti wakati wa kusafirisha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news