IGP Sirro:Wasithubutu, atakayethubutu asitulaumu

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, IGP Simon Nyangoro Sirro ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao hawajiingizi kwenye makundi ya kigaidi,anaripoti Mwandishi Diramakini (Dar es Salaam).
IGP Sirro amesema kwa yeyote ambaye atathubutu kufanya hivyo, watashughulikiwa kikamilifu na kamwe hakuna ambaye anapaswa kumlaumu mwingine ikiwemo Serikali kutokana na vitendo hivyo.

Ameyasema hayo leo Januari 4, 2021jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na utendaji kazi wa Jeshi la Polisi kwa mwaka 2020 na malengo waliyojiwekea kwa mwaka huu wa 2021.

IGP ametoa onyo hilo kutokana na swali aliloulizwa na mmoja wa wanahabari kuhusiana na hali ya usalama ilivyo mkoani Mtwara,eneo ambalo siku za karibuni yaliripotiwa matukio ya uhalifu ambayo jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama viliyadhibiti. 

"Kule Mtwara tunaenda vizuri, timu zetu zipo na ninawashukuru sana wananchi kule mpakani wanatupa taarifa vizuri na huku ndani wanaofanya chokochoko wananchi wanatupa taarifa na tunawashughulikia vizuri. Nitoe wito kwa wazazi na walezi kujitahidi sana watoto wao wasijiingize kwenye hayo makundi, kwa maana wakiishajiingiza kwenye makundi hayo hawatailaumu Serikali,"
amesema IGP Sirro.

Pia amesema kuwahawana mchezo na watu wanaojiingiza kwenye ugaidi. "Ukishajiingiza kwenye ugaidi maana yake hiyo ni vita na ukiishajiingiza kwenye vita pia matokeo yake yanakuwa mabaya. Ukiishaingia huko tukipambana utakayoyapata usilaumu, umetaka mwenyewe, ndiyo maana niliwaambia siku moja mama mtunze mwanao, maana akina mama ndiyo wana uchungu na watoto.

"Kwa hiyo mama mtunze mwanao, kumtunza sio kumpa chakula tu, ni pamoja na kuhakikisha haiingii kwenye hayo makundi ambayo mwisho wa siku atapata tabu,"amesema ambapo alipoulizwa kuhusu taarifa za mmoja wa wanaharakati kukamatwa, IGP Sirro amesema hata mwanaharakati anaweza kuwa gaidi, lakini huyo anayeitwa mwanaharakati watu wa Uhamiaji ndiyo wanashughulika naye, maana suala lake linahusu watu hao, lakini wao (Jeshi la Polisi) sio la kwao sana. 

"Hata ukiwa ni Sheikh au Padre hata kama ulikuwa ni Katekista gani ukiingia kwenye ugaidi, wewe ni gaidi utashughulikiwa kama gaidi mwingine. Habari ya kuniambia wewe ni padre hizo hakuna,"amesisitiza IGP Sirro.

Wakati huo huo amesema suala la maadili bado ni changamoto katika jeshi, "Kwa upande wa maadili bado kuna changamoto kidogo kwa sababu wapo wachache wanakuwa na lugha mbaya, wakati mwingine kwa kutomhudumia mteja mzuri, hivyo lazima mteja ataondoka na jambo lolote,"amesema.

Pia amesema,wateja hasa wa nje wenye magari wamekuwa wakilalamikia Trafiki kuhusiana na vitendo vya rushwa. Kwa msingi huo, amesema, wamekubaliana malalamiko ya rushwa kwenye kikosi cha trafiki yapungue kwa mwaka huu.

Amefafanua kwamba, wameweka mpango mkakati wa kuhakikisha makosa ya kudai na kuomba rushwa yanapungua. Sirro alisema moja ya mkakati huo ni kuhakikisha elimu inazidi kutolewa kwa askari wao na kwa umma kwa kutumia vikundi shirikishi na vyombo vya habari.

"Lengo ni kuhakikisha vitendo vya rushwa vinafikia ukomo." Hata hivyo, IGP Sirro amesema suala la huduma kwa mteja linategemea aina ya mteja wanayemhudumia.

Kwa mujibu wa IGP Sirro, wateja wengine wao ni hasira muda wote. "Ukishamwandikia faini tu ya elfu 30 hata kama unamwambia lugha nzuri, yeye ni hasira elfu 30 inamuuma zaidi."Alisema Sirro na kusisitiza kuwa wateja wengine hawataki kuambiwa ukweli. 

Mbali na hayo, IGP Sirro amekiri kuwepo upungufu wa baadhi ya vitendea kazi vyao, kama vile vipimia ulevi na speed na kwamba watajitahidi kuhakikisha wanavipata.

Katika hatua nyingine, IGP Sirro amekemea vikali vitendo vya baadhi ya askari ambao sio waaminifu wanaoweka watu ndani kwamuda mrefu kwa kesi ya trafiki.

"Labda mtu awe amesababisha ajali na mtu kafa na ionekane kuna ugumu fulani, lakini makosa ya trafiki hatuhitaji kukaa na mtu muda mrefu. Kuna makatazo ambayo tumeyatoa ili kuhakikisha tunawatendea watu haki. Makatazo tuliyoyatoa ni kwamba tuheshimu watu,"amesema.

IGP Sirro amesema, kuna suala ambalo linaonekana kana kwamba wamewekeana malengo ya kukusanya kiasi fulani cha fedha kutokana na makosa ya barabarani.

"Watanzania wenzangu, hilo halipo, makosa yanakamatwa kutokana na yanavyofanyika na wala hakuna suala la kuwekeana malengo kwa ajili ya kuongeza pato la Taifa. Hilo sio kweli makosa yanakuwa ni mengi, lakini kuna watu ambao wanajua wana deni wanadaiwa shilingi laki mbili, wanaamua kuficha gari.Ninawaombe sana mkono wa Serikali ni mrefu, hauwezi kuficha gari, wengine wana magari mengi wanaamua kubadili namba za gari inayodaiwa na kuziweka kwenye gari ambalo halidaiwi.

"Kwa hiyo ukiingia kwenye mfumo inakuwa haisomeki, unapofanya namna hiyo maana yake unafanya makosa ya kughushi, niwaombe Watanzania wanaofanya hivyo, maelekezo niliyoyatoa wakamatwe washtakiwe kwa makosa ya kughushi. Fedha inayodaiwa ni Serikali, sasa shida ni nini. 

"Lakini kuna magari ya IT vijana wao walikuwa wanafanya makosa wanaingia kwenye faini wakati yana taratibu zake na hauwezi kumuingiza kwenye mfumo na kesho ukamdai,"amesema.

Post a Comment

0 Comments