Maafisa wanne wa Polisi watumbuliwa akiwemo aliyejiunganishia umeme

Jeshi la Polisi nchini Tanzania limewafukuza kazi askari wanne akiwemo askari aliyetambuliwa kwa jina la F.1445 Koplo William aliyekamatwa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kenan Kihongosi Januari 6, 2021 kwa kosa la kujiunganishia umeme na kukutwa na bangi na pombe haramu jijini Arusha, anaripoti Mwandishi Diramakini (Arusha).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Salum Hamduni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Salum Hamduni amesema kuwa, Koplo William amekamatwa Januari 5, 2021 usiku akiwa Mtaa wa Muriet uliopo Kata ya Sokoni One jijini Arusha na DC Kihongosi akijihusisha na matukio ya uhalifu. 

Ametaja matukio hayo kuwa ni pamoja kujiunganishia umeme wa wizi kinyume na sheria, kupatikana na misokoto ya bangi 20, pombe ya gongo lita tano na ya viroba boksi 84 ambavyo vimekatazwa na serikali.

Kamanda Hamduni amesema, matukio mengine ni kukutwa na vyuma vya bomba, mafuta ya dizeli lita 85, chupa zenye konyagi tisa na pakti tatu za viroba.

Mbali na askari huyo, Kamanda Hamduni amesema Desema 24,2020 askari watatu na raia sita walikamatwa kwa tuhuma za kushawishi rushwa kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya Gems and Rocks Venture, Sammy Mollel. 

Kwa mujibu wa RPC huyo, uchunguzi wa tukio hilo umekamilika na tayari wamechukua hatua za kinidhamu na kiutawala dhidi ya askari hao.

"Napenda kuwafahamisha askari hao wamefukuzwa kazi kwa fedheha tangu jana tarehe 6, 2021 na watafikishwa mahakamani kwa kuwa jalada tayari limeishapelekwa kwa mwanasheria wa mashtaka na kwa ushahidi ambao tumekusanya tunaamini uwezekano mkubwa upo wa kuweza kuwafikisha kwenye mahakama za kiraia,"amesema Kamanda Hamduni.

Kamanda huyo amewataja askari hao kuwa ni Heavenlight Mushi aliyekuwa kitengo cha intelijensia Mkoa wa Kinondoni, Gasper Paul wa Kitengo cha Intelijensia ya Jinai Makao Makuu na Bryton Murumbe aliyekuwa askari wa kawaida Mkoa wa Dodoma.

Pia amefafanua kwamba, tayari upelelezi wa makosa yao umekamilika na jalada limepelekwa ofisi ya Taifa ya mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria.

Kwa mujibu wa Kamanda Hamduni, askari hao walimteka na kumuomba rushwa ya sh. milioni 30 mfanyabiashara huyo wakiwa pamoja na watu sita akiwemo meneja wa kampuni ya kuuza madini ya Crown Lapidary ya Arusha, Lucas Mdeme.

Amesema, kutokana na askari hao kujihusisha na makosa ya kiuhalifu wamekosa sifa ya kuendelea kuwa askari na hivyo wamefukuzwa kazi.

Hata hivyo, amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoani humo katika kufichua na kutoa taarifa za waharifu na uhalifu. 

Awali Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kenani Kihongosi alimtia mbaroni askari Koplo William, akidaiwa kuiba umeme kwa kipindi cha takribani mwaka mmoja. 
Polisi huyo amedaiwa kukutwa na misokoto ya bangi, viroba vya pombe kali vilivyopigwa marufuku na Serikali ambavyo inadaiwa alikuwa akivijaza kwenye chupa za konyagi na kwenda kuuzia wananchi.

Wakati huo huo,ndani ya nyumba ya askari huyo inadaiwa kukutwa madumu mawili ya mafuta aina ya dizeli.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news