Maalim Seif ampa RC siku 21 mashine ifungwe hospitali

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ametoa muda wa wiki tatu kwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Bi.Salama Mbarouk Khatib kuhakikisha mashine ya kuchambua damu imefungwa na kuanza kazi katika Hospitali ya Wete.
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad alipofanya ziara ya kushtukiza leo hospitalini. (Picha na Mwandishi Diramakini).

Maalim Seif ametoa kauli hio baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Makamu huyo amefika katika kitengo cha damu salama na kutaka kujua namna shughuli zinavoendeshwa.

Sambamba na hilo, Maalim Seif ametaka kujua ni kwanini mpaka sasa mashine mpya ya kuchambua damu Blood Centrifuge Machine bado haijafungwa na kufanya kazi kama inavyotakiwa.

Mashine hio yenye uwezo wa kuchambua mpaka chupa mia moja za damu kwa siku imeletwa katika hospitali hiyo takriban miezi miwili sasa.

Kiongozi Mkuu wa Kitengo cha Damu Salama Pemba, Dkt. Khalfan Ali Masoud amesema mashine hiyo haijafungwa kutokana na ukosefu wa eneo sahihi.

Pamoja na utetezi huo wa Mkuu wa Kitengo cha Damu Salama Pemba, Makamu wa Kwanza wa Rais amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba kuhakikisha ndani ya wiki tatu tu mashine hiyo iwe imefungwa na kufanya kazi.

Post a Comment

0 Comments