Maalim Seif:Mimi na Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi tumeungana kwa dhamira njema na tutachapa kazi kuwaletea maendeleo

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad amewaeleza Watanzania kuwa, yeye na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi wameungana kwa dhamira njema hivyo jukumu walilonalo kwa sawa ni kuwaunganisha wananchi na kuwaletea maendeleo, anaripoti Mwandishi Diramakini (Chato).
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema hayo katika Soko la Kimataifa la Samaki Kasenda Wilaya ya Chato mkoani Geita alipotembelea Wavuvi na Wafanyabiashara wa soko hilo leo.

Baada ya shughuli ya kukagua soko hilo iliyofanywa na Rais Dkt. Mwinyi na yeye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kumalizia, Maalim Seif amezungumza na waandishi wa habari na kusema kwamba, ziara yake ya Chato imekuwa na mafanikio makubwa kwani yale waliyoyajia yote yamekwenda sawa.

"Mkutano na Rais wa Jamhuri wa Muungano umeleta mwangaza mkubwa kwa maslahi ya Wazanzibari. Rais Magufuli ametushauri, na sisi tukamueleza ya kwetu na ameahidi kutupa msaada wa kila aina ili kuhakikisha malengo ya kuiboresha Zanzibar yanafikiwa, lakini pia ametupa moyo wa kuendelea kuwaunganisha Wazanzibari,"amesema Maalim Seif.
Kuhusu watu ambao mpaka sasa hawaamini kama Maalim Seif ni kweli amekubali kuungana katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Maalim Seif amesema inabidi waamini tu kwani hakuna ambacho hakiwezekani, muhimu pawepo nia na dhamira njema.

Kuhusu matarajio ya Serikali ya Zanzibar Maalim amesema, "Wazanzibari watarajie mazuri kwa sababu ya umoja wetu, kwani kupitia umoja huu Wazanzibari watapata mafanikio ndani ya muda mfupi kabisa.

"Kwa sasa Tanzania inabadilika sana kimaendeleo na ni muda sahihi kwa Wananchi kushirikiana na Serikali zao kuboresha maendeleo hayo,"ameongeza.

Nae Mwenyekiti wa Wafanyabiashara na Wavuvi katika soko la Kasenda kwa niaba ya wenzake wote wamemzawadia gunia moja la Dagaa kavu Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar kama shukurani yao kwake kwa ujio wake na kuitangaza biashara yao Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news