Maalim Seif:Tuendelee kuyalea maridhiano yetu kwa maslahi ya Taifa na wananchi wetu

Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuwa, maridhiano ya Zanzibar ni mtoto anayehitaji malezi bora zaidi ili aendelee kuwepo kwa maslahi mapana ya nchi na wananchi wake, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad akitoa salamu zake katika mkutano huo jijini hapa. (Picha na OMRZ/Diramakini).

Maalim Seif ameyasema hayo katika Mkutano wa Zanzibar Peace Confererence ambao umeandaliwa na Taasisi ya Friends of Zanzibar wakishirikiana na Ofisi ya Mufti Zanzibar, Januari 16, 2021.

Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort iliyopo Mazizini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja jijini Zanzibar umewakutanisha Wawakilishi wa kibalozi na taasisi nyingine mbalimbali ambao ni wajumbe wa taasisi ya Friends of Zanzibar. 

Wawakilishi hao wametoa salamu zao sambamba na kusema kwamba wao wapo pamoja na Taifa la Zanzibar na wanawapongeza sana viongozi kwa kushirikiana na kuleta amani katika nchi hii.

Pamoja na hayo wageni hao wamesema hata wao wanaamini kwamba ushirikiano uliopo Zanzibar kwa sasa ni ujumbe mzuri kwa Mataifa mengine mengi ya Bara la Afrika.

Kwa upande wake, Maalim Seif katika kutoa salamu zake kwa wajumbe hao amesema, katika nchi mbalimbali migogoro huwa haiachi kutokea, lakini inapotokea kuna njia mbili hutumika ya kwanza ni kupigana hadi kuumizana ndio mwisho viongozi hukaa kwenye meza kutafuta suluhu na nyingine ni kuepuka kugombana na kukaa kwenye meza kuyatatua.

"Na sisi Zanzibar tuliamua kukaa kwenye meza moja kuyajadili bila ya kuumizana na ndio njia nzuri zaidi,"amesema.

Pia Maalim Seif ametoa nasaha zake kwa mgeni rasmi wa mkutano huo ambaye alikuwa ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa kumwambia kuwa, "Mheshimiwa Rais maridhiano ni kama mtoto ambae ni mwema, hivyo tunahitaji kumlea vyema ili vizazi vyetu vije kuirithi amani hii sambamba na kuiacha Zanzibar kuwa ni nchi ya amani na iliyo salama".

Katika hatua nyingine, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif ameishukuru sana Taasisi ya Friends wa Zanzibar kwa kusema kuwa,anayekufaa kwa dhiki ndio rafiki.

"Na taasisi hii iliyokusanya wajumbe wa Mataifa mbalimbali nawashukuru sana kuwa pamoja nasi na kuendelea kuwa marafiki zetu hata wakati wa matatizo,"amesema Maalim Seif.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news