Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif aeleza malengo ya Serikali ya Awamu ya Nane

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amewataka wananchi kushirikiana na kudumisha umoja ikiwemo kufanya kazi kwa bidii ili kufanikisha malengo ya Serikali ya Awamu ya Nane ya kuwaletea maendeleo chini ya Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Maalim Seif ameyasema hayo alipopata fursa ya kuwasalimia waumini wenzake wa dini ya kiislamu katika Msikiti wa Jumuiya ya Waarabu Muembeladu Mkoa wa mjini Magharibi Unguja, aliposali sala ya Ijumaa leo Januari 8, 2021.

Maalim Seif amesema, kwa sasa changamoto zote zinazowakabili zitakuwa basi na badala yake Serikali hii itajikita katika kuleta maendeleo ya haraka katika nchi kama vile ajira za kutosha ili kila mmoja aweze kuwa na shughuli ya kufanya ya kumpatia kipato, sambamba na kuleta maendeleo ya jumla katika nchi.

Katika kusisitiza hilo Maalim Seif amesema, jambo hilo litafanikiwa ikiwa tutashirikiana, kuungana na kuwa pamoja.

Maalim Seif amesema, kwa sasa lengo la Serikali ni kuwaunganisha Wazanzibari ili kuwa kitu kimoja, kuondoa ubaguzi wa kila aina, kila Mzanzibari apate haki zake bila bughza yoyote na kila kiongozi afanye haki kwa kila mwananchi wa Zanzibar.

Pia Maalim Seif amewaomba waumini hao kuiombea dua Serikali na viongozi wake ili viongozi wawe na moyo wa dhati katika kuwatumikia wananchi hapa nchini.

Post a Comment

0 Comments