Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar ahamasisha mshikamano kwa wote

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla amesema mshikamano wa pamoja kati ya viongozi, waumini wa dini pamoja na wananchi mahali popote walipo ndio njia ya msingi itakayorahisisha kulijenga Taifa imara, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akitoa salamu zake baada ya kukamilika sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Ijumaa jijini Zanzibar. (Picha na OMRZ/ Diramakini).

Akitoa salamu mara baada ya kukamilika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Ijumaa pembezoni mwa Uwanja wa Michezo wa Aman jijini Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman amewakumbusha waumini hao kwamba kila mwananchi ana nafasi yake katika kujenga nchi si lazima awe mtumishi wa umma. 

Mheshimiwa Hemed amesema, hatua hiyo ya mshikamano wa pamoja ambayo Serikali Kuu tayari imeshaonyesha muelekeo wa mfano katika ngazi ya uongozi itawezekana na kufanikiwa ipasavyo endapo jamii nzima itaendelea kuhamasishana katika usimamizi wa masuala ya amani. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametahadharisha kwamba yapo mataifa duniani baadhi ya waumini wake wenye imani ya Uislamu wameshindwa kutekeleza ibada ya sala ya Ijumaa kutokana na machafuko yaliyosababishwa na itikadi za kisiasa au kidini. 

Mheshimiwa Hemed Suleiman amehimiza umuhimu wa waumini na wananchi kuendelea kuzingatia uadilifu katika matendo yao kama ulivyosisitizwa katika hotuba ya Ijumaa ili kuleta utulivu wa moyo ndani ya vifua vya watu katika maeneo yao. 

Ameeleza kwamba, changamoto za kijamii kwa asilimia kubwa zinaweza kuondoka au kupungua kabisa kama ulafi wa baadhi ya watu hasa katika masuala ya fedha utadhibitiwa jambo ambalo hivi sasa Serikali Kuu imekuwa ikiendelea kuchukua hatua za kukabiliana nalo. 

Amewahimiza wananchi pamoja na waumini wa dini kuvumilia kipindi hiki ambacho uongozi wa Serikali umekuwa ukichukua hatua hizo zinazoonyesha mwanga kwa baadhi ya washirika wa maendeleo ndani na nje ya nchi kwa kutaka kuungwa mkono jitihada hizo za Serikali. 

Mapema akitoa hotuba ya sala ya Ijumaa Mwanachuoni Maarufu Ustaadh Rajab Mohamed Shaali amewakumbusha waumini wa dini ya Kiislamu kuhakikisha kwamba suala la uadilifu linapewa nafasi yake ili jamii mitaani iendelee kuishi kwa upendo. 

Ustaadhi Rajab amesema, utamaduni wa baadhi ya watu kupenda kujilimbikizia mali za dhuluma sio malengo ya uwepo wao duniani katika kufanya ibada bali unazidisha chuki na uhasama miongoni mwa jamii katika ngazi ya ufukara, umasikini na utajiri.  

Awali Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alikutana na Uongozi wa Jumuiya Wazee Wastaafu Zanzibar ili kubadilishana mawazo mazungumzo yaliyofanyika ofisini kwake Vuga jijini Zanzibar. 

Katika mazungumzo hayo, Mheshimiwa Hemed amesema Serikali itaendelea kuwaheshimu wazee wote Nchini kwa kuwapatia huduma stahiki ikitimiza wajibu wake ili waendelee kupata utulivu wa maisha yao huku ikizingatia kuwa mchango wao ndio uliosababisha Taifa hili kufikia hatua kubwa ya maendeleo. 

Mheshimiwa Hemed amesema, Serikali inaelewa changamoto na matatizo mengi yanayowakumba Wazee katika maisha yao ya kawaida na ndio maana hulazimika kufanya utafiti wa kutosha unaosaidia kupata muelekeo wa kuwajengea mazingira rafiki. 

Amesema, katika hatua ya kuyakidhi mahitaji yao ya lazima Wazee , Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati wote imekuwa na mfumo wa kuangalia mazingira ya hali ya uchumi inavyozunguuka na pale inaporuhusu haioni tatizo nguvu hizo kuzielekeza kwa Wazee hao waliotoa mchango mkubwa kwa Taifa wakati wa utumishi wao. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akitoa ushauri kwa viongozi hao wa Jumuiya Wastaafu amesema, ipo haja ya kuendelea kutoa elimu kwa watumishi wanaokaribia kustaafu ili pale watakapofikia muda waendelee na maisha yao bila ya wasiwasi wowote. 

Mheshimiwa Hemed amesema, watumishi wengi wanapopata barua ya kumaliza muda wao wa Utumishi huchanganyikiwa huku wakijisahau kwamba wapo Vijana wengi waliomaliza masomo yao ambao wanahitaji kuziba nafasi zao kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma Serikalini. 

Mapema Katibu wa Jumiya ya Wastaafu Zanzibar, Bibi Salama Kombo Ahmed amesema, wazee wengi nchini wamefuharia uwepo wa sheria iliyowashirikisha moja kwa moja wazee wenyewe ingawa bado haijawa na kanuni zake. 

Bibi Salama amesema Jumuiya ya Wastaafu Zanzibar iliyoasisiwa mnamo Mwaka 2001 pamoja na mambo mengine inaendesha mradi wa kuwaelimisha Wazee kupitia Mabaraza yao ya shehia Unguja na Pemba ili kutambua kwamba miaka 60 ya ustaafu sio mwisho wa maisha yao. 

Katibu wa jumuiya hiyo ya Wastaafu Zanzibar kwa niaba ya wanajumuiya wameishukuru Serikali Kuu kwa uamuzi wake wa kuendelea kuwapatia pensheni kila mwezi sambamba na ile ya shilingi 20,000 kwa wazee wa zaidi ya miaka sabini. 

Hata hivyo Bibi Salama amesema zipo baadhi ya changamoto zinazoendelea kuwasumbua wazee akizitaja kuwa ni pamoja na ukosefu wa Kitambulisho ili kuwapa uangalizi wa huduma za Afya na Hospitali pamoja na Uwakilishi wa Wazee katika Mabaraza ya Kutunga Sheria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news