Mbunge Ridhiwani Kikwete amshukuru Flaviana Matata kwa moyo wa upendo

Mbunge wa Jimbo la Chalinze mkoani Pwani, Ridhiwani Kikwete amempongeza na kumshukuru Mwanamitindo wa Kimataifa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Flaviana Matata, Bi.Flaviana Matata kwa kujitoa kwake kusaidia masuala ya elimu ndani ya jimbo hilo, anaripoti Mwandishi Diramakini. 
Mbunge Ridhiwani Kikwete akishirikiana na Mwanamitindo Flaviana Matata kugawa zawadi ya mabegi kwa wanafunzi jimboni humo.

Awali akizungumza wakati wa kutoa shukrani zake kwa mwanamitindo huyo, Mbunge Ridhiwani Kikwete amesema, wameupokea kwa mikono miwili huku akimuomba kuendelea kusaidia bila kuchoka na maeneo mengine.

"Tunakupongeza sana kwa misaada hii unayotoa kwetu hasa kijiji hiki cha Msinune. Sisi tutaendelea kukuombea dua njema na kukupa ushirikiano mkubwa kuhakikisha kuwa malengo ya taasisi yako yanafikiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wetu wanafaidika na uwepo wa taasisi yako,''amesema.
Wanafunzi wakionyesha furaha yao baada ya kupewa zawadi ya mabegi.

Mbunge Kikwete amemuhakikishia, Bi. Flaviana Matata kuwa ofisi yake na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, inatambua michango yako katika shule hii ikiwemo kusaidia ujenzi wa nyumba za walimu, madarasa, vyoo na hata maji na leo hii vifaa vya shule kwa wanafunzi.

Aidha, Mbunge amemhakikishia, Bi.Flaviana kuwa atamuunga mkono katika ujenzi wa nyumba za walimu. 
Baadhi ya wanafunzi wakiwa wameshikilia zawadi zao za mikebe jimboni Chalinze.

"Mimi kama Mbunge lazima nikupatie sapoti kwa hatua hii. Pili sisi kama halmashauri na kupitia mfuko wa jimbo nipo tayari kusaidia vifaa vya ujenzi ilikukamilisha nyumba za walimu ili kuboresha elimu yetu,"amesema Ridhiwani Kikwete.

Kwa upande wake, Flaviana Matata amewashukuru walimu, kamati ya shule, Diwani wa Kata hiyo pamoja na Mbunge kwa namna wanavyotoa ushirikiano mkubwa hali ambayo amewaahidi kuendelea kusaidia juhudi hizo bila kuchoka. 
Wanafunzi wakionyesha furaha yao baada ya kupewa zawadi jimboni Chalinze.

Aidha, Flaviana Matata amemhakikishia Mbunge Ridhiwani Kikwete kuendelea kuchangia elimu ikiwemo kuendeleza ujenzi wa nyumba za walimu na miundombinu mingine akiwa kama mlezi wa shule hiyo.

Katika hatua nyuingine, Flaviana Matata aliwaomba wazazi kuacha tabia ya kuwataka watoto wa kike kuwasimamisha masomo na baadala yake amewataka waache wasome ilikuja kuwa msaada kwao hapo.

No comments

Powered by Blogger.