Mhandisi Kemikimba ampa Mkandarasi Suma JKT siku 60 kukamilisha ujenzi

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba ametoa siku 60 kwa mkandarasi Suma-JKT kukamilisha ujenzi wa tenki la maji la Buigiri-Chamwino litakalogharimu kiasi cha shilingi milioni 998 ambalo linatarajiwa kuhudumia wakazi wa Chamwino na Hospitali ya Rufaa ya Uhuru jijini Dodoma, anaripoti Happiness Shayo (WM).

Ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya kikazi kukagua maendeleo ya ujenzi wa tenki hilo litakalokuwa na ujazo wa lita milioni mbili na laki tano lililoko eneo la Buigiri-Chamwino.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba (katikati) akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph (wa kwanza kushoto) alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu kazi ya flushing ya kisima katika eneo la Nzuguni Jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba akiuliza maswali kuhusu ramani ya uchimbaji visima katika eneo la Ihumwa alipofanya ziara ya kikazi katika eneo hilo jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) alipofanya ukaguzi wa ujenzi wa tenki la maji lililoko eneo la Buigiri Wilayani Chamwino jijini Dodoma.

"Tumekubaliana na mkandarasi kuwa tenki hili likamilike ndani ya mwezi wa pili, kwa hiyo wana siku 60 tu kuhakikisha ujenzi umekamilika,"amesema.

Naibu Katibu Mkuu, Kemikimba amesema kuwa, ilitakiwa tenki hilo lijengwe tangu mwezi wa tisa mwaka 2020, lakini kutokana na mipango yao wenyewe imepelekea kuchelewa kwa ujenzi huo.

Aidha, ameitaka menejimenti ya Wakala wa Majina Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kufanya ufuatiliaji wa ujenzi wa tenki hilo kila siku ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.

Muonekano wa Hospitali ya Rufaa ya Uhuru iliyopo jijini Dodoma itakayotumia maji kutoka tenki la maji lililoko eneo la Buigiri Wilayani Chamwino.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba akiangalia eneo la Hospitali ya Rufaa ya Uhuru litakalopitiwa na miundombinu ya maji kutoka tenki la maji lililoko eneo la Buigiri Wilayani Chamwino alipofanya ziara ya kikazi jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba (wa pili kutoka kushoto) akitoa maelekezo kwa mkandarasi SUMA-JKT kukamilisha ujenzi wa tenki la maji la Buigiri – Chamwino alipokagua ujenzi wa tenki hilo jijini Dodoma leo. Wengine ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph (wa kwanza kushoto) na baadhi ya watendaji wa DUWASA.

Muonekano wa eneo kunakojengwa tenki la maji la Buigiri Wilayani Chamwino.

Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu, Kemikimba ametembelea eneo la Ihumwa panapochimbwa visima na amekiagiza kitengo cha uchimbaji kilicho chini ya RUWASA kuongeza kasi ya uchimbaji visima ili kukamilisha miradi kwa wakati lengo ikiwa ni kuongeza kiasi cha maji kwa Jiji la Dodoma.

Akiwa katika eneo la Nzuguni, Naibu Katibu Mkuu, Kemikimba amekagua kazi inayoendelea ya flushing ya kisima itakayosaidia kuongeza kiasi cha maji kwa Jiji la Dodoma na alisema kuwa, ameridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA) kwa kuwa wabunifu katika kutafuta vyanzo vya maji. Ziara hizo muendelezo wa ziara zake za kukagua utekelezaji wa miradi ya maji katika Jiji la Dodoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news