Naibu Waziri Dkt.Mollel atoa onyo kwa watendaji Sekta ya Afya

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Dkt. Godwin Mollel amewataka watoa huduma za afya nchini kuwajibika ipasavyo katika kuwahudumia wananchi, anaripoti Mwandishi Diramakini (Songwe).
Mheshimiwa Dkt. Mollel ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wataalamu watendaji wa Afya wa Mkoa wa Songwe katika ukumbi wa Halmashauri ya Songwe. 

Amesema, watumishi wa Serikali kada ya Afya kuna sehemu hawawajibiki ipasavyo ndio maana malalamiko hayaishi kutoka kwa wananchi. 

“Ninyi mmeajiriwa na Serikali na kila kitu kinatolewa na Serikali, lakini utashangaa mtu anashindwa kutoa huduma bora kwa mwananchi ila mtu huyo huyo jioni unamkuta kwenye kituo binafsi anahudumia vizuri ina maana huku serikalini anafanya makusudi kwa kutokumjali mteja,"amehoji Dkt. Mollel. 
Ameongeza kuwa, kutokana na hali hiyo unakuta wananchi wanakimbia Kituo cha Serikali wanaenda kwenye kituo binafsi wakati serikalini ndio kuna wataalamu wabobezi kuliko hata huko binafsi ila kutokana na huduma zisizoridhisha mwananchi anaona bora aende akalipe hela nyingi apate huduma kuliko kutibiwa kwenye gharama nafuu, "hii tabia ikome kuanzia sasa na kila mmoja awajibike ipasavyo. 

“ Inabidi tuanze kunyooshana pale tunaposkia malalamiko ili hadhi ya vituo vya kutolea huduma za Afya vya Serikali irudi watu wapewe huduma bora na wafurahie huduma hizo zinazotolewa na Serikali yao hii itasaidia kuongeza mapato ya Serikali na kuendelea kuboresha huduma kwa ujumla. 

"Watumishi wa Afya lazima wafanye kazi kwa weledi na kufuata kanuni za maadili ya utoaji wa huduma za Afya ili kufikia malengo ya upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote,"amesema. 

Dkt.Mollel amesisitiza usimamizi makini wa miradi ya maendeleo huku akitolea mfano Hospitali ya Wilaya ya Ileje inayojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.8 wakati maeneo mengine wakiwa wamemaliza kiasi hicho cha fedha na ujenzi haujakamilika. 

“Nizitake halmashauri zingine ziende kujifunza Ileje ambapo wametumia bilioni 1.8 kujenga jengo zuri la hospitali ilihali halmashauri hii iko pembezoni hata upatikanaji wa vifaa ni mgumu, lakini halmashauri zingine za mjini kabisa hawajakamilisha ujenzi na fedha wamemaliza na wanaomba kuongezewa fedha nataka niwaambie tu kuwa hakuna fedha za nyongeza na hospitali hizo zikamilike,” amesema Dkt.Mollel. 
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Afya Ustawi wa Jamii na Lishe, Dkt. Ntuli Kapologwe amemshukuru Naibu Waziri wa Afya kwa maelekezo aliyoyatoa kwa watumishi watendaji wa afya Mkoa wa Songwe na ameahidi kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo. 

Pia amewataka waganga wafawidhi wa vituo vyote vya Kutolea Huduma za Afya kuhakikisha wananunua kompyuta na kufunga mfumo wa GoT-HoMIS ili kudhibiti mapato ya vituo kwa matokeo bora zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news