Prof.Manya atoa siku mbili wavamizi kuondoka eneo la mwekezaji madini

Apinga uvamizi wa maeneo yenye leseni hai, asisitiza kuondoka katika kesi za utoroshaji madini na uvamizi wa maeneo, aeleza kuheshimu mifumo iliyopo sasa kwenye Sekta ya Madini, atoa angalizo kwa wafanyabiashara na madalali wanaohamasisha uvamizi

Wavamizi wa eneo la mwekezaji wa kampuni ya El Hillal Limited iliyopo katika eneo la Mwang'holo Kata ya Mwadui mkoani Shinyanga wamepewa siku mbili ili kupisha shughuli za mwekezaji huyo kuendelea, anaripoti Steven Nyamiti (WM) Shinyanga.
Maagizo hayo yametolewa leo Januari 21, 2021 na Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya alipotembelea eneo hilo na kuitaka Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Shinyanga kuwaondoa wavamizi ili kulinda eneo hilo la mwekezaji.

Agizo hilo lilitolewa baada ya Naibu Waziri wa Madini, Prof.Manya kupokea malalamiko kutoka kwa Kampuni ya El Hillal Minerals Limited yenye leseni ya uchimbaji mkubwa wa madini ya almasi SML 404/2010 kuhusiana na kuvamiwa na wachimbaji wadogo katika eneo lake.
Awali katika kikao baina ya uongozi wa wizara na wachimbaji wakubwa wa madini ya Almasi, wachimbaji wadogo pamoja na wafanyabiashara wa madini, Prof.Manya alitoa maelekezo maalumu akiwataka kusitisha utaratibu wa kuendelea kudhamini vikundi mbalimbali vya wachimbaji wadogo kuvamia kwenye eneo lenye leseni na kushauri wazingatie sheria za madini zilizopo sasa kwa faida ya pande zote.

“Ninaelekeza wachimbaji wote waliovamia eneo hili la mgodi kuondoka ndani ya siku mbili kwa kuwa mnafanya shughuli za madini kinyume na sheria,”amesema Naibu Waziri.

Prof.Manya ameeleza kuwa, ili wawekezaji wajitokeze kwa wingi ni lazima Serikali ilinde haki za wachimbaji wakumbwa, wadogo na wakati. 
“Sheria ya Madini inasema mwenye leseni anao wajibu wa kuheshimiwa pamoja na kupatiwa ulinzi na usalama ili afanye shughuli zake ipasavyo,"amesema. Aidha, Prof.Manya amemuelekeza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha anaongeza ulinzi na usalama wa eneo hilo baada ya siku mbili kukamilika kuanzia.

”Ninawataka wachimbaji wote mliovamia eneo hili mfuate utaratibu uliopangwa na namuelekeza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa huu kuhakikisha anawapatia eneo tofauti ili muendelee na uchimbaji, lakini mkiwa kwenye taratibu zinazotambulika kisheria,”amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Teleck alimpongeza Prof. Manya kwa kutoa maelekezo kwa wachimbaji kuondoka ndani ya siku mbili na kutoa maelekezo kwa kamati yake ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kuzingatia maagizo hayo ili kutatua mgogoro huo wa uvamizi. 

Naye Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Joseph Kumbulu amesema kuwa, mnamo tarehe 20/03/2020 Ofisi ya Madini kwa kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama imewatoa wachimbaji wadogo zaidi ya 400 waliovamia eneo lenye leseni ya uchimbaji ya mgodi wa mwekezaji huyo.
Ameongeza hadi sasa eneo hilo lina idadi kubwa ya wachimbaji zaidi ya 1,000. Hivyo amesisitiza kusimamia kikamilifu maagizo yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Madini ili kulinda haki za mwekezaji kwenye eneo hilo na kutatua migogoro inayotokea kwenye maeneo ya kimadini hapa nchini.

Kumbulu amesema kuwa, anaomba elimu itolewe kwa viongozi wa vijiji, vitongoji na kata kuhusu umiliki halali wa ardhi na Sheria za Madini kwa kuwa kumekuwa na changamoto kubwa ya utoaji wa vibali na uuzwaji wa ardhi kwenye maeneo ambayo yanamilikiwa na mgodi kisheria.

Naibu Waziri wa Madini, yupo kwenye ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali yenye shughuli za madini hapa nchini na ziara yake katika eneo la mgodi wa Kampuni ya El Hillal limekuwa la faida kwa mwekezaji huyo baada kutoa maelekezo kwa wavamizi kuhakikisha wanatoka kwenye eneo hilo ambalo ni leseni halali ya mchimbaji mkubwa wa madini ya almasi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news