Rais Dkt. Mwinyi amuapisha Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amemuapisha Mhandisi Zena Ahmed Said kuwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, akichukua nafasi ya Dkt. Abdulhamid Yahya mzee aliyestaafu, anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini. 
Hafla hiyo ya kiapo imefanyika leo Januari 2, 2021 Ikulu jijini Zanzibar na kuhudhuriwa na na viongozi mbalimbali wa Kitaifa, akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdalla, Mawaziri, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee pamoja na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid. 

Wengine ni pamoja na Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Dkt. Mwinyi Talib Haji, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa, Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaab, Askofu Dickson Kaganga, Wakuu wa Vikosi vya SMZ pamoja na wanafamilia. 

Rais Dkt. Mwinyi amemuapisha kiongozi huyo kushika wadhifa huo baada ya kumteua Januari Mosi, mwaka huu, kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya kifungu cha 49 (1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. 

Kabla ya uteuzi huo Mhandisi Zena Ahmed Said alikuwa Katibu mkuu Wizara ya Nishati katika Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Katika hatua nyingine, akizungumza na vyombo vya habari, Mhandisi Zena amesema atajitahidi kufanya kazi zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo ili kufikia matarajio ya Wazanzibari. 

Amesema, atafuata kanuni na sheria na kujiongeza katika ubunifu ili aweze kufikia malengo, huku akiahidi Serikali kuangalia kwa undani umuhimu wa ajira kwa vijana. 

Aidha, ametoa wito kwa wanawake nchini kote kujiamini na kufanya kazi zao kwa weledi pamoja na kuwataka kufanya shughuli zao kwa kuzingatia wakati na nafasi zao, sambamba na kutosubiri kusaidiwa. 

Mhandisi Zena Ahmed Said, anakuwa mwanamke wa kwanza nchini kushika wadhifa wa Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, tangu Mapinduzi ya 1964. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news