Rais Dkt.Mwinyi aazimia kukomesha udhalilishaji kwa watoto, wanawake

Waziri wa Nchi (OR) Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mikakati maalum kwa kipindi cha mwaka 2017-2022 ikiwa ni hatua ya kupambana na vitendo vya udhalilishaji dhidi ya watoto na wanawake nchini, anaripoti Mwandishi Diramakini. 

Waziri Haroun amesema hayo wakati akifungua tamasha la kwanza la pongezi kwa Wana Sunni Madrasa katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa Sunni Madrasa, Mkunazini jijini Zanzibar.
Waziri wa Nchi (OR) Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman. (Picha na Maktaba).

Akimwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi, Waziri Haroun ameahidi kukutana na wadau wanaoshughulikia vitendo vya udhalilishaji, ikiwemo Jeshi la Polisi, Mahakama na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka kwa lengo la kujenga mikakati ili kuharakisha usikilizaji wa kesi za makosa hayo yalioshamiri nchini. 

Amesema, Serikali hairidhishwi na mrundikano uliopo wa kesi za udhalilishaji na hivyo akaitaka jamii kujenga ushirikiano na vyombo vya sheria ili kufanikisha mchakato wa kesi pamoja na kuondokana na muhali. 

Ametumia fursa hiyo kuwapongeza walimu wanaofundisha fani hiyo ya ‘Nasheed’ kwa kazi nzuri wanayofanya pamoja na kuwaomba kuendelea na juhudi za kuisambaza taaluma hiyo hadi vijijini Unguja na Pemba. 

Katika hafla hiyo Waziri Haroun amekabidhi zawadi kwa washindi wa Tamasha hilo la ‘Nasheed’ , ambapo mwanafunzi Nasra Abdalla Mohamed alikuwa mshindi wa kwanza na hivyo kuzawadiwa Friji, Mkoba pamoja na Ma-shafu. 

Aidha, mwanafunzi Asiat Ramadhan Jussa alikuwa mshindi wa pili na kuzawadiwa zawadi za Cherehani, Mkoba na Mas-hafu, huku mwanafunzi Mudrik Msellem Ali akiondoka na ushindi wa tatu na kuzawadiwa Baiskeli, Mkoba na Mas-hafu. 

Mapema, Katibu mtendaji Idara ya Sensa na Sanaa Omar Abdalla Adamu amewashukuru waandaji wa tamasha hilo na kusema wamekamilisha taratibu zote za kisheria na kufuata mila, silka na utamaduni wa Mzanzibari. 

Nae, Sheikh Habibu Othman ‘Mazinge’ amewata waislamu nchini kote kumuomba Mwenyezi Mungu adumishe amani na umoja miongoni mwa Wazanzibari. 

Aidha, aliumuomba Mwenyezi Mungu kuilinda Zanzibar ili iendelee kubaki na amani na usalama pamoja na kuwajaalia viongozi wote wa Serikali amani. 

Katika tamasha hilo wanafunzi 20 walisoma ‘Nasheed’ mbalimbali zenye maudhui ya kupinga vitendo vya Udhalilishaji kwa watoto na wanawake. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. Mwenyenzi Mungu awaongoze, hakika yajayo yanafurahisha Zanzibar

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news