Rais Dkt.Mwinyi afungua Le Mersenne Beach Resort, atoa wito

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewasisitiza wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu na kuwa wakarimu kwa wageni ili kila mgeni anayefika Zanzibar apende kurejea tena, anaripoti Mwandishi Diramakini. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (wa pili kushoto) akipata maelezo kutoka kwa mmiliki wa Hoteli ya Lemersenne iliyopo Michamvi Wilaya ya Kusini Unguja yenye hadhi ya nyota tano, Bw.Riaz Mawani (kulia) mara baada ya kuifungua hoteli hiyo leo ikiwa ni katika shamrashama za miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, kushoto ni Mke wa Rais Mama Mariam Mwinyi. (Picha na Ikulu/ Diramakini).

Rais Dkt. Hussein ameyasema hayo leo Januari 9, 2021 katika ufunguzi wa Hoteli ya Le Mersenne Beach Resort iliyopo katika Mradi wa “Jumeira Holdings Company Ltd” iliyopo Michamvi, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja. 

Amewapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kuwakaribisha vyema wageni na kuwataka kuidumisha amani na utulivu ili watalii wandelee kuona Zanzibar ni kisiwa cha amani. 

Rais Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi wa Michamvi kwa kuwakaribisha watalii kwa ukarimu wao mkubwa ambao umeweza kuwavutia. 

Katika hotuba yake Rais Dkt. Mwinyi aliuhimiza uongozi wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kwa kushirikiana kwa karibu na Kamisheni ya Utalii, Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) na wadau wote katika sekta hii kuongeza kasi ya kuitangaza Zanzibar katika masoko mapya.

Vile vile, Rais Dkt. Mwinyi alihimiza umuhimu wa kuendeleza utalii unaozingatia uhifadhi wa mazingira.

Aidha, alieleza haja ya kutolewa kwa elimu na kuwaelekeza vizuri wawekezaji juu ya taratibu za ulipaji wa kodi na utii wa sheria za nchi. 

Rais Dkt.Mwinyi alitoa shukurani na pongezi kwa wawekezaji wa hoteli hiyo kwa uamuzi wao wa busara wa kuichagua Zanzibar na kuja kuwekeza hatua ambayo itasaidia kutekeleza lengo la Serikali la kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya kutengeneza ajira 300,000 kazi ambayo inahitaji hoteli nyingi, viwanda vingi na miradi mingi. 

Aidha, Rais Dk. Mwinyi amesema kuwa, mradi huo umetoa ajira kwa wananchi 103 katika nafasi mbalimbali bila shaka idadi hiyo itaongezeka wakati hoteli hiyo itakapokuwa inapokea wageni wengi zaidi. 

Amemshukuru kwa kufuata Sera za nchi na kuwataka kuwaajiri wananchi wa Zanzibar pamoja na kuhakikisha kwamba wanaoajiriwa ni wale wanaokaa katika maeneo ambayo hoteli ipo. 

Rais Dkt.Mwinyi ameongeza kuwa, Serikali itaendelea na Sera ya kuweka vivutio vya kodi kwa kuhakikisha inapata mapato na wananchi wote wanafaidika. 

Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi alieleza furaha yake kuona kwamba wawekezaji wa mradi huo wanaendelea kukamilisha taratibu zitakazowawezesha kutekeleza mradi mwingine mkubwa kama huo katika kisiwa cha Pemba. 

Ameeleza kuwa, hatua hiyo, vile vile inaendana na dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kukifanya Kisiwa cha Pemba kuwa eneo maalum la uwekezaji na kuitaka ZIPA kuhakikisha kwamba zoezi hilo la kukamilisha taratibu za kuwekeza Pemba linakwenda vizuri kwa kuwatafutia maeneo husika bila kuwepo kwa urasimu. 

Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane imeelekeza juhudi kubwa katika kuendeleza uchumi wa buluu, ambao umejumuisha sekta ya utalii. 

Pamoja na hayo, Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, Serikali itatekeleza mpango wa kuwasaidia wavuvi na wakulima wa mwani kwa zana za kisasa ili kuhakikisha kwamba mipango ya kuendeleza uchumi wa buluu inatekelezwa kwa ufanisi mkubwa. 

Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kupigiwa mfano kwa kuwa na mipango imara ya kukabiliana na maradhi ya virusi vya Corona (COVID-19) kwani maradhi hayo yameathiri sana sekta ya utalii. 

Ameongeza kuwa, inakadiriwa kwamba watalii wapatao 40,000 walipokelewa Zanzibar katika mwezi wa Disemba, 2020 hatua ambayo ni nzuri na inatia moyo. 

Rais Dkt.Mwinyi amezitaka mamlaka zote zinazohusika na masuala ya utalii kuanzia uwanja wa ndege hadi hoteli kuhakikisha zinawawekea mazingira mazuri watalii ili waendelee kuja tena. 

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Mudrik Soraga amesema kuwa, kufunguliwa hoteli hiyo ya kitalii yenye hadhi ya nyota tano ni miongoni mwa azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kupokea watalii wa daraja la juu ambao watakuza hadhi ya nchi kiutalii pamoja na kuongeza pato la nchi na kipato cha mtu mmoja mmoja. 

Amesema kuwa, Ilani ya CCM pamoja na Mipango Mikuu ya Serikali imeelekeza kuwa na uchumi wa buluu ambao miongoni mwake ni matumizi ya rasilimali za fukwe za bahari kwa kuanzisha hoteli zenye hadhi ya juu. 

Ameongeza kuwa, katika kuweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji nchini, Serikali kupitia Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji (ZIPA) inatoa huduma zake kupitia kituo kimoja cha huduma (One Stope Center) ambapo kwa sasa kinaendelea kuimarishwa. 

Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya kukuza Uwekezaji Zanziar (ZIPA), Salum Khamis Nassor alieleza kuwa mradi huo unaendeshwa na Kampuni ya Jumeira Holding Ltd ambapo pia kampuni hiyo inamiliki hoteli nyingine ya kitalii kati ya mji mkongwe inayoendeshwa kwa jina mashuhuri duniani “Best Western”. 

Amesema kuwa, mradi huo ulianzishwa Machi 15, 2011 ukiwa na mtaji wa makisio wa Dola za Kimarekani milioni 8.4 ambapo kama ilivyotarajiwa ni hoteli yenye hadhi ya nyota 5 na uwezo kuhudumia wageni 120 kwa wakati mmoja. 

Amesema kuwa, tayari mradi huo umewekeza mtaji wa Dola za Kimarekani milioni 9.1 ambayo ni ziada ya Mpango wa uwekezaji wa awali ambapo hoteli hiyo ina idadi ya vyumba 51, ukumbi wa mikutano wenye uwezo wa kuhudumia watu 200, SPA pamoja na huduma nyingine ambapo mradi huo unatarajiwa kuajiri watu 103 ambapo wageni ni wawili tu. 

Kwa upande wa ZIPA, Mkurugenzi huyo amesema kuwa, hadi kufikia mwezi Disemba 2020, ZIPA imeidhinisha jumla ya miradi 761 ya uwekezaji yenye mtaji wa makisio wa dola za Kimarekani Bilioni 7.3 katika sekta ya utalii. 

Ambapo kati ya hiyo alisema kuwa miradi 364 inatoa huduma za miradi mbalimbali ambapo sekta ya utalii inaongoza kwa kuwa na miradi 452 ambayo ni sawa na asilimia zaidi ya 60 ambayo yote imezalisha ajira 54,000 za moja kwa moja. 

Nae mwekezaji wa hoteli hiyo Bw.Riaz Mawani amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa kushinda uchaguzi na kuwa Rais wa Zanzibar na kueleza matumaini ya wawekezaji kutokana na kasi yake. 

Ametumia fursa hiyo kwa kupongeza amani, utulivu na usalama mkubwa uliopo Zanzibar ambao ni miongoni mwa vivutio vilivyowavutia kuja kuwekeza. 

Sambamba na hayo, mmiliki huyo ameeleza azma yake ya kushirikiana na Serikali katika kutekeleza Ilani ya CCM katika kuwasaidia vijana kupata ajira ambapo vijana 103 wamepata ajira.

Sambamba na hayo, ametoa pongezi kwa Serikali zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kupambana na maradhi ya corona na kusema kuwa hatua hiyo imepelekea kuwavutia watalii wengi kuja kutalii hapa nchini. 

Katika ufunguzi huo viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na serikali walihudhuria akiwemo Mama Mariam Mwinyi. 

Post a Comment

0 Comments