Rais Dkt.Mwinyi aingia rasmi mapambano dhidi ya udhalilishaji watoto, wanawake

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameshauri kuundwa Kamati Maalum itakayowashirikisha wadau mbalimbali wa masuala ya udhalilishaji ikiwa ni hatua ya kulitafutia ufumbuzi tatizo la udhalilishaji wa kijinsia lililoshamiri katika jamii hapa nchini, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi (katikati) akiongoza Mkutano wa siku moja wa wadau wanaohusika na masuala ya udhalilishaji ambao umewashirikisha viongozi na wananchi mbalimbali uliofanyika leo katika ukumbi wa Idrissa Abdulwakil Kikwajuni jijini Zanzibar. (Picha na Ikulu/Diramakini). 

Mheshimiwa Dkt. Mwinyi ametoa ushauri huo leo Januari 7, 2021 katika mkutano uliofanyika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul-wakil, Kikwajuni jijini Zanzibar ambapo umejadili masuala ya udhalilishaji wa kijinsia na namna ya kukabiliana na uhalifu huo na kuwashirikisha wadau wa ngazi zote. 

Amesema, kutokana na ukubwa wa tatizo la udhalilishaji lililoshamiri hapa nchini, kuna umuhimu wa kuunda Kamati Maalum itakayowashirikisha wadau mbalimbali wa masuala ya udhalilishaji, ikiwemo Polisi, Mahakama na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka na kufanyakazi kuambatana na hadidu rejea na kuyapatafutia ufumbuzi matatizo mbalimbali, ikiwemo yale yatokanayo na wao wenyewe.

Amesema, miongoni mwa majukumu ya kamati hiyo itakuwa ni kufuatilia kesi zilizoko Mahakamani, kuangalia haja ya marekebisho ya sheria, uimarishaji wa maeneo ya kupima wadhuriwa (victims) wa matukio ya udhalilishaji, kuimarisha madawati ya polisi pamoja na matatizo yatokanayo ya taasisi za kidini katika eneo la ufundishaji kama vile madrasa. 

Ameeleza kuwa, suala la udhalilishaji ni kubwa na limekuwa likiitia aibu nchi pamoja na kuleta maumivu makubwa kwa wanaodhuriwa, hivyo akataka itambulike kuwa ni vita ya Kitaifa na hivyo kila mmoja mahali alipo atapaswa kutoa ushirikiano ili kumaliza tatizo hilo.

Amesema, suala la rushwa ni miongoni mwa changamoto zinazokwaza utoaji haki katika vyombo vya sheria, hivyo akazitaka taasisi za polisi, Mahakama na hospitali kujitathmini na kuondokana na mambo hayo.

“Tusipopambana na rushwa hili jambo litakuwa gumu, naitaka ZAECA kuongeza bidii, wakati mwingine wala sio rushwa, ni urasimu tu, lazima tutafute njia ya kuondoa urasimu,”amesema. 

Amesema, takwimu zilizowasilishwa na watoa mada katika mkutano huo zinatia shaka kutokana na kuwepo idadi kubwa ya kesi ambazo watuhimiwa wameachiliwa.

Rais Dkt.Mwinyi amesema ni wakati mwafaka wa kuangalia mitaala ya skuli pamoja na kufanya tathmini kwa madrasa ziliopo baada ya kuwepo taarifa kuwa baadhi ya walimu kutuhumiwa kuhusika na vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanafunzi, lakini hatimae baada ya kufukuzwa huanzisha vyuo vyao.

Amesema ni wakati sasa kwa Wizara ya Afya kuimarisha sehemu za upimaji wa wadhuriwa wa matukio ya udhalilishaji pamoja na kuwa na vifaa vya kazi vya kutosha, ili jamii iweze kuondokana na usumbufu. 

Aidha, ameitaka Idara ya Mahakama kuondokana na mkwamo katika usikilizaji wa kesi unaochukua kipindi kirefu, hatua aliyosema inawachosha walalamikaji wa kesi hizo.

Ameliagiza Jeshi la Polisi kupitia Madawati ya kijinsia kuwa na utaratibu mzuri wa kuweka taarifa zote za matukio ya udhalilishaji na kuyaripoti kwa viongozi wa ngazi za juu.

Katika kulipatia ufumbuzi wa changamoto hiyo, Dkt.Mwinyi ameitaka idara hiyo kuja na njia za ubunifu na kuangalia uwezekano wa kuanzisha Mahakama Maalum ya Makosa ya Udhalilishaji. 

Kuhusiana na changamoto zinazohusu sheria mbalimbali, Dkt.Mwinyi amesema ni wakati sasa wa kuziangalia kwa kina sheria ziliopo na kuzifanyia mabadiliko, na kuwataka wadau kukaaa chini na kuwasilisha miswada ya sheria hizo katika baraza lijalo la wawakilishi. 

Mapema, jumla ya mada tano ziliwasilishwa katika mkutano huo, ambapo Mkurugenzi wa Jinsia na Watoto, Nasima Haji Chum amesema suala la udhalilishaji ni suala mtambuka linalohitaji ushirikiano kati ya jamii na vyombo vya sheria. 

Aidha, Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar Mohamed Ali Mohamed amesema miongoni mwa changamoto zinazofanya kukosekana ufanisi wa kesi hizo ni mashahidi kushindwa kufika mahakamani kutokana na mnasaba wa kifamilia na hivyo kesi nyingi hatimae kuishia kwa usuluhishi.

Amesema pamoja na Zanzibar kupata tuzo ya kuwa na sheria bora ya watoto (no 6 ya 2011), sheria hiyo haitoi adhabu ya kifungo kwa watoto, hivyo baadhi yao watoto hao hurejea kufanyamakosa hayo.Alitoa mapendekezo kadhaa, ikiwemo ya mabadiliko ya sheria mbali mbali pamoja na kupendekeza matumizi sahihi ya sheria kwa mujibu wa maelekezo. 

Nae Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mohamed Hassan amesema, kuna umuhimu mkubwa wa kuwaongezea uwezo wapelelezi wa kesi hizo pamoja na kupanua wigo katika utoaji wa elimu katika jamii kuhusu matumizi bora ya talaka katika ndoa.

Vile vile, Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, Ibrahim Mzee amesema, mchakato wa kesi za udhalilishaji unakabiliwa na changamoto ya utoaji wa dhamana mahakamani, mbali ya sheria ya kesi hizo kubainisha kuwa hazina dhamana. 

Mwanaharakati Amina Yussuf Ramadhan amesema miongoni mwa vichocheo vinavyochangia makosa hayo ni pamoja na mmong’onyoko wa madili, utitiri wa baa mitaani pamoja na ‘Guest Bubu’ akibainisha kuwepo taarifa za vituo vidogo vya Polisi (post) visivyotumika hivi sasa, kutumika kama ‘guest bubu’. 

Katika mkutano huo wadau mbalimbali walitoa michango juu ya nini cha kufanya ili jamii iweze kuondokana na wimbi la makosa ya udhalilishaji yanaoyojiri kila kukicha. 

Mkutano huo umewashirikisha viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Sadalla, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk. Mwinyi Talib Haji, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa pamoja na Mawaziri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news