Rais Dkt.Mwinyi atoa maagizo muhimu kwa wakuu wa wilaya zote

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka Wakuu wapya wa wilaya walioapishwa kuhakikisha kunakuwepo ulinzi na usalama wa kutosha katika wilaya zao, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi akimuapisha, Bi. Marina Joel Thomas kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kati Unguja, hafla hiyo imefanyika Januari 4, 2021 katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar. (Picha na Ikulu).

Dkt. Mwinyi ametoa maelekezo hayo wakati alipowaapisha wakuu wa wilaya 10 za Unguja na Pemba katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Zanzibar. 

Desemba 28, mwaka 2020 Rais Dkt. Mwinyi alifanya mabadiliko ya Uteuzi wa Wakuu wa Wilaya 11 za Zanzibar kwa kumteua Marina Joel Thomas kuwa Mkuu wa Wilaya Kati Unguja, Issa Juma Ali (Mkoani), Hamida Mussa Khamis (Magharibi ‘B’) na CDR Mohamed Mussa Seif kuwa Mkuu wa Wilaya Micheweni Pemba.

Wengine walioteuliwa na kuapishwa ni Rashid Simai Msaraka (Mjini Unguja), Sadifa Juma Khamis (Kaskazini ‘A’), Aboud Hassan Mwinyi (Kaskazini ‘B’), Rashid Makame Shamsi (Kusini Unguja), Mgeni Khatibu Yahya (Wete) na Abdalla Rashid Ali Wilaya ya Chakechake Pemba.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi akimuapisha Bw.Rashid Simai Msaraka,kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mjini Unguja, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar. 

Amesema, viongozi hao wakiwa Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama katika wilaya zao, wana wajibu wa kuhakikisha kunakuwepo Ulinzi na Usalama wa kutosha wakati huu ambapo matukio mbalimbali ya uhalifu yakiwa yameshamiri.

Ameeleza kuwa, nchi haiwezi kupata maendeleo yoyote endapo hakutakuwepo na amani na usalama na kubainisha kuwepo kwa matukio mengi ya uhalifu, ikiwemo wizi wa mazao pamoja na mifugo, kiasi ambacho baadhi ya wananchi wameamua kuachana na kilimo au ufugaji.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi akimuapisha, Bw.Issa Juma Ali,kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Pemba, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar. 

Amewataka Wakuu hao wa Wilaya kusikiliza migogoro mbalimbali inayowakabili wananchi pamoja na kutoa haki kwa mambo yalio ndani ya uwezo wao na kuwataka kuyapeleka katika ngazi zinazohusika mambo yalio nje ya uwezo wao, akibainisha umuhimu wa kuondokana kabisa na migogoro iliyo ngazi za chini (shehiya).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akimuapisha, Bw.Aboud Hassan Mwinyi,kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar.

Aidha, amewataka viongozi hao kuhakikisha wanasimamia kikamilifu masuala ya usafi ndani ya wilaya zao, kwa kigezo kuwa sekta ya utalii ikiwa ndio mhimili wa Uchumi wa Zanzibar inategemea zaidi kuwepo kwa usafi katika maeneo yote ya nchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akiwa katika hafla ya kuapishwa kwa Wakuu wa Wilaya za Unguja na Pemba, hafla iliofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar Januri 4, 2021, kulia kwake ni Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Mgeni Hassan Juma. 

Katika hatua nyingine, Dkt.Mwinyi amegusia suala la udhalilishaji wa watoto na wanawake kijinsia na kusema kuwa ni tatizo linalohitaji ushirikiano kati ya jamii, asasi za kiraia na wadau wote wa mapambano dhidi ya udhalilishaji ikiwemo Polisi, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka na Mahakama.

Amewataka wadau hao kuja na mipango mipya katika ushughulikiaji wa tatizo hilo linaloendelea kushamiri kila kukicha.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akimuapisha CDR.Mohammed Mussa Seif,kuwa Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Pemba, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar. 

Aidha, amewataka wakuu hao wa wilaya kufanya juhudi katika kuinua viwango vya elimu ndani ya wilaya zao, kwa kuhakikisha kunakuwepo miundombinu bora, idadi ya walimu wanaotosheleza pamoja na vifaa vya kufundishia vilivyo katika hali nzuri.
Wakuu wa Wilaya za Unguja na Pemba wakifuatilia hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) baada ya kuwaapisha katika ukumbi wa Ikulu.

Amesema katika miaka ya nyuma kulikuwa na mashindano yaliosaidia kuinua viwango vya wanafunzi kielimu, hivyo akabainisha umuhimu wa jambo hilo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi akimuapisha Bw.Abdalla Rashid Ali,kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chakechake Pemba, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar. 

Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza umuhimu wa viongozi hao kwenda kufanya kazi kwa kujituma pamoja na kufanya ziara za mara kwa mara katika maeneo yao, akibainisha kuwa wao sio viongozi wa kukaa ofisini muda wote.“Ni muhimu kuwatembelea watu kwa kuwa kuna changamoto mbalimbali zinazowakabilia katika maeneo yao,”amesema.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi akimuapisha, Bw.Sadifa Juma Khamis kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A Unguja, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar. 

Vile vile amewataka viongozi hao kuitekeleza kikamilifu Ilani ya CCM ya 2020-2025 pamoja na kuhakikisha ahadi zote zilizotolewa wakati wa Kampeni ya Uchaguzi mkuu zinatekelezwa kikamilifu, akibainisha mwamko mkubwa walionao wananchi katika kupata maendeleo kwa haraka.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi akimuapisha, Bw.Rashid Makame Shamsi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar.

Pamoja na kuwashukuru viongozi hao kwa kukubali uteuzi huo, Dkt. Mwinyi amewataka kuwa mstari wa mbele katika kukamilisha wajibu wao pamoja na kuwaondolea kero wananchi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akimuapisha, Bi. Hamida Mussa Khamis kuwa Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B Unguja hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar.

Hafla hiyo ya kiapo iliwashirikisha viongozi mbalimbali wa Kitaifa akiwemo Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdalla, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Ahmed Said, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mgeni Hassan Juma, Jaji Mkuu wa Zanzibar , Omar Othman Makungu, Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Dkt. Mwinyi Talib Haji. 

Wengine ni Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab, Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar Saleh Kinana, Wakuu wa Mikoa mitatu ya Zanzibar, Makamanda wa vikosi vya Ulinzi na Usalama, Askofu Dickson Kaganga pamoja na wanafamilia.
rRais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi akimuapisha, Bi.Mgeni Khatib Yahya kuwa Mkuu wa Wilaya ya Wete Pemba, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar. (Picha zote  na Ikulu/Diramakini).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news