Rais Dkt.Mwinyi atoa msamaha kwa wafungwa

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametoa msamaha kwa wanafunzi (wafungwa) 49 waliokuwa wakitumikia Vyuo vya Mafunzo vya Unguja na Pemba ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za Sherehe za miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi. (Picha na Maktaba).

Dkt.Mwinyi ametoa msamaha huo kwa mujibu wa kifungu cha 59 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kinachompa mamlaka ya kutoa msamaha kwa wafungwa waliofungwa gerezani.

Kutokana na msamaha huo, Dkt.Mwinyi ameamuru kuwa kifungo kilichobaki cha wanafunzi (wafungwa) hao walionufaika na msamaha katika vyuo vya Mafunzo vya Unguja na Pemba kuwa kipindi hicho chote kinafutwa na waachiwe huru kuanzia leo Januari 11,2021.

Kwa vile, Zanzibar itakuwa inasherehekea miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964, Dkt. Mwinyi ameona kuwa kuna sababu za kutosha za kutoa msamaha kwa walengwa walionufaika na msamaha huo kwa Unguja ambao ni 46 na Pemba watatu.

Msamaha huo hutolewa kila mwaka katika kipindi cha sherehe za Mapinduzi matukufu na huwahusisha wanafunzi ambao ni wazee sana, wenye maradhi sugu au wenye makosa madogo ambao wamebakisha muda mfupi wa kutumikia chuoni, wanaoonesha nidhamu nzuri chuoni na kujutia makosa yao.

Wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo wenye makosa kama vile kuua kwa makusudi, wizi wa kutumia nguvu, wizi wa mali ya umma, makosa ya kudhalilisha wanawake na watoto, makosa ya dawa za kulevya na wenye makosa mengi ya zamani kwa kawaida huwa hawapewi msamaha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news