Rais Dkt.Mwinyi awapa pole wanamichezo waliopata ajali

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewapa pole wanamichezo wa kundi Shirikishi la Mazoezi la MUWAFAKI waliopata ajali ya kugongwa na gari iliyokuwa ikienda mwendo kasi, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwafariji wanamichezo waliopata ajali ya kuvamiwa na gari katika barabara ya Migombani wakati wakiwa katika mazoezi, Ndg. Sastenesi Amasi na Ali Abdulla, waliolazwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja jijini Zanzibar. (Picha na Ikulu/Diramakini).

Dkt.Mwinyi amewapa pole majeruhi hao na kumuomba Mwenyezi Mungu awape nafuu na waendelee kupona haraka ili waweze kuendelea na majukumu yao ya kimaisha. 

Kwa mujibu wa maelezo ya Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, Dkt. Marijani Msafiri Marijani ajali hiyo imetokea leo Januari 2,2021 mapema asubuhi huko katika barabara ya Migombani Jeshini, Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi na kusababisha majeruhi 14. 

Rais Dkt.Mwinyi ameelezwa kuwa, ajali hiyo imetokea wakati kundi hilo la MUWAFAKI likifanya mazoezi ambalo linajumuisha vikundi vitano kikiwemo kikundi cha Kitambi noma kutoka Zanzibar, kikundi cha Fighter na Wakali kutoka Dar es Salaam, kikundi cha Muungano kutoka Dodoma na kikundi cha Uluguru kutoka mkoani Morogoro. 

Wanamichezo hao wa kundi hilo ambao jana walishiriki kikamilivu katika Bonaza la Maadhimisho ya Siku ya Mazoezi ya Viungo Kitaifa lililofanyika hapa Zanzibar ambapo kwa mujibu wa maelezo ya Dkt. Marijani majeruhi hao wanaendelea kupata matibabu katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mnazi Mmoja na watano miongoni mwao wamepata huduma na kuruhusiwa kurejea nyumbani. 

Ajali hiyo imesababishwa na mwendo kasi wa gari aina ya IST yenye namba za usajili 634 HK iliyokuwa ikiendeshwa na dereva Nassor Jabir Magondi ambae alikuwa akiendesha gari hiyo kwa mwendo wa kasi licha ya kuonyeshwa kibendera chekundu na miongoni mwa wasimamizi wa kundi hilo la mazoezi lakini gari hiyo ilimshinda na kuwagonga wafanya mazoezi hao.

Post a Comment

0 Comments