Rais Dkt.Mwinyi awataka viongozi kwenda kushirikiana na wananchi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewakumbusha viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wajibu wa kurudi kwa wananchi kuwatumikia pamoja na kushirikiana nao katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili baada ya uchaguzi mkuu kumalizika, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akiwahutubia na kulifungua Kongamano la jumuiya tatu za CCM za UWT, UVCCM na Wazazi lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni jijini Zanzibar Januari 6, 2021. (Picha na Ikulu/Diramakini).

Mheshimiwa Dkt. Mwinyi amesema hayo katika ufunguzi wa Kongamano la Jumuiya za CCM za UWT, Wazazi pamoja UVCCM lililofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakil Kikwajuni jijini Zanzibar, likiwa na lengo la kuwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli pamoja an Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali mwinyi kwa ushindi mkubwa waliopata katika uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba, 2020. 

Amesema, wananchi wanashida mbalimbali zinazohitaji misaada kutoka kwa viongozi wao, hivyo akawataka kutokuwasahau wale waliowachagua na kubainisha kuwa huo ndio mwelekeo sahihi wa viongozi wanaotoka CCM.

Amesema, uchaguzi umemalizika, hivyo kazi kubwa iliyopo mbele ya viongozi wa chama hicho ni kuwatumikia wananchi kwa kuyatekeleza mambo mbalimbali waliyoyaahidi katika kampeni pamoja na kuitekeleza Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya 2020-2025. 

Aidha, amewakumbusha wanachama wa chama hicho wajibu walionao katika kujiandaa na uchaguzi ndani ya chama hicho ifikapo mwaka 2022, hivyo akawataka kujiandaa kwa msingi kuwa hatua hiyo itatoa fursa ya kupanga safu za uongozi katika chama hicho.

“Nasaha zangu kwenu wakati utakapofika, wachagueni viongozi wenye mapenzi ya dhati na CCM na sio wanaotafuta maslahi yao wenyewe kupitia CCM,”amesema. 

Ameeleza kuwa, ni muhimu kupata viongozi wenye uwezo wa kukitumikia chama hicho ili waweze kukivusha katika uchaguzi mkuu ujao, akiamini chama hicho kina hazina kubwa ya viongozi bora.

Aidha, Dkt. Mwinyi amesema hatua zilizoanza kuchukuliwa katika kupambana na vitendo vya ubadhirifu wa mali za umma, uzembe na ukiukwaji wa sheria pamoja na rushwa zinalenga kuleta nidhamu katika matumzi ya fedha za Serikali. 

Amesema serikali imeanza kuchukua hatua za kupambana na vitendo vya ubadhirifu wa mali ya umma, uzembe, ukiukwaji wa sheria, pamoja na rushwa miongoni mwa watendaji wake kwa dhamira njema ya kuleta nidhamu katika matumizi ya fedha za Serikali kwa manufaa ya wananchi.

Amewahakikishia wana CCM kuwa wale wote watakaohusika na matukio ya vitendo hivyo watachukuliwa hatua za kisheria bila kumuonea mtu, hivyo akawataka wananchi kuunga mkono hatua hiyo.

“Nafahamu kuwa hatua hizi tunazozichukua kuna wengi wanazifurahia, ingawa wapo wachache zinawaumiza lakini ni vyema watuvumilie,”amesema. 

Akigusia maudhui ya kufanyika kwa kongamano hilo, Dkt.Mwinyi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM amesema, ushindi mkubwa uliokipata chama hicho katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Oktoba 2020 katika pande mbili za Muungano na katika ngazi zote, ni kielelezo cha imani na matumaini waliyonayo Watazania kwa chama chao.

Amesema, Watanzania wanaridhishwa na utendaji wa chama hicho na ndio maana wakafanya maamuzi ya kuendelea kukichagua kwa kura nyingi.

Amesema CCM kinajipambanua na vyama vingine vya siasa kwa kuwa na ukweli katika utekelezaji wa Ilani yake ya Uchaguzi pamoja na ahadi zake kwa asilimia kubwa katika kila awamu ya uongozi.

“CCM ina Ilani na sera zinazotekelezeka kulingana hali halisi ya wananchi hasa walio wanyonge, zikiwa na lengo la kuwaletea maendeleo na ustawi wa maisha yao,"amesema. 

Rais Dkt. Mwinyi ametoa shukurani kwa viongozi na wanachama wa jumuiya hizo kwa uamuzi wa kuandaa kongamano hilo lenye lengo la kumpongeza kutokana na ushindi mkubwa wa asilimia 76.27 aliopata katika Uchaguzi Mkuu pamoja na kuipongeza CCM kwa kuwa na utaratibu mzuri wa Kidemokrasia wa kupata viongozi katika ngazi mbalimbali.

Aidha, amewapongeza wanachama wa CCM kwa namna wanavyojitokeza kwa wingi katika hafla mbalimbali za ufunguzi wa miradi ya maendeleo na uwekaji wa mawe ya msingi katika kipindi hiki cha shamrashamra za kuelekea maadhimisho ya miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

Mapema, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Sadalla ‘Mabodi’amesema chama hicho kinaunga mkono hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi katika kuimarisha ustawi wa jamii pamoja na mapambano dhidi ya Udhalilishaji.

Sambamba na hatua ya kuunda serikali ya umoja wa Kitaifa (GNU).Amesema, hatua ya kuunda GNU itaendeleza umoja na mshikamano wa Wazanzibari na kudumisha utawala bora.

Ametoa pongezi kwa kusimamia na kuweka kipaumbele katika uimarishaji wa uchumi wa nchi kupitia uchumi wa Buluu, akibainisha Bahari kuwa ni rasilimali muhimu hapa nchini. 

Amesema, CCM itaendelea kusimamia kikamilifu uibuaji wa matukio mbalimbali ya ubadhirifu na uwajibikaji.

Aidha, amesema miongozo ya utekelezaji wa jumuiya hizo inafanya kazi kwa pamoja na ndio iliosababisha kushuka hadi chini na kukipatia chama hicho ushindi. 

Nae Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Othman Ali Maulid amesema, kongamano hilo linalenga kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Mwinyi kwa ushindi mkubwa wa asilimia 76.27 aliopata katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba, 2020.

Amesema kwa pamoja jumuiya hizo zinampongeza Dkt.Mwinyi kutokana na hotuba mbalimbali alizozitoa kwa nyakati tofauti na hivyo kuwapa matumaini makubwa wananchi katika utumishi wake.

Katika kongamano hilo mada tatu ziliwasilishwa ikiwemo ya ‘Uchumi wa Buluu’ ; Utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020-2025 pamoja na Historia ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964. 

Katika Kongamano hilo lililoandaliwa na Jumuiya za CCM za UWT, Wazazi pamoja na UVCCM, viongozi mbalimbali wa chama hicho na Serikali walishiriki, wakiwemo wake wa viongozi wakuu wa Kitaifa wakiongozwa na mama Mariamu Mwinyi pamoja na wake wa viongozi wakuu wastaafu, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Abdalla Juma Sadalla, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan Juma, Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Mawaziri pamoja na Wabunge na Wawakilishi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news