Rais Magufuli kumpokea Waziri wa Mambo ya Nje wa China kesho

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikino wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Mjumbe wa Baraza la Taifa wa  China, Wang Yi  atafika hapa nchini kesho Januari 7, 2021 kwa ziara ya siku mbili hadi tarehe 8 mwezi huu, anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) mjini Chato leo. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Amesema kuwa, Waziri Wang Yi Yuko katika ziara siku tano katika nchi tano za Afrika ikiwemo Tanzania,DR Congo, Botswana na Shelisheli.

Kabudi amesema kuwa, ziara hiyo ni matokeo ya mazungumzo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli aliyofanya kwa njia ya simu na Rais wa Chini Xi Jinping Desemba 15, mwaka jana.

Amesema, katika ziara hiyo atapokelewa katika uwanja wa ndege wa Geita ulioko wilayani Chato na baada ya kuwasili atafungua na kuweka jiwe la msingi katika Chuo cha Ufundi (Veta) wilayani Chato na kuzungumza na wananchi.

Amesema, Waziri Wang Yi anafungua chuo hicho cha Veta cha Wilaya ya Chato kwa sababu tatu ambazo ametaja kuwa ni kumpa heshima kama mila zetu zilivyo kwa mgeni anayekutembelea,pili ni kutambua kwamba nchi ya China imepiga hatua kubwa katika teknolojia ya ufundi.

Ameongeza kuwa, sababu ya tatu ni kutambua mchango wa nchi ya China ambayo kwa sasa inajenga chuo cha Veta mkoani Kagera ambapo taifa hilo lilikubali kujenga vyuo vya ufundi 50 kwa nchi za Afrika.

Profesa Kabuni amefafanua kuwa, Waziri Wang Yi baada ya kufika Chato atafanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli  na Baadaye atafanya mazungumzo na Waziri mwenzake wa Tanzania pamoja na ujumbe wake.

Ameongeza kuwa, siku ya pili Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi  atatembelea mwalo wa uvuvi wa samaki wa Chato  katika ziwa Victoria ili kujionea shughuli za uvuvi katika eneo hilo.

Amesema, Tanzania imeomba kusafirisha moja kwa moja na kuuza nchini China bidhaa zitokanazo na samaki hasa Mabondo ya samaki ambayo amesema yana thamani na bei kubwa kuliko samaki wenyewe.

Profesa Kabuni ameeleza kuwa,nchini China wanatumia Mabondo ya samaki kwa ajili ya kutengeneza madawa na urembo hivyo ni bidhaa yenye thamani kubwa.

Shughuli nyingine itakayofanywa na Waziri Wang Yi ni kushuhudia kusainiwa mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Mwanza kwenda Isaka yenye urefu wa kilometa 341 itajengwa kwa gharama ya Dola 1,000,326,000 ambayo ni sawa na Trilioni 3.0617 za Kitanzania.

Amesema, kipande hicho cha SGR kinajengwa kwa fedha za serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 lakini wazabuni walioshinda kujenga mradi huo ni wawili kutoka nchini China.

Ametaja Wazabuni hao kuwa umoja wa Wazabuni ambao ni China Civil  Engeering Construction Corporation(CCECC) na China Railway Construction Limited (CRCC).

Profesa Kabudi ameongeza kuwa, katika msafara wa Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi ataambatana na ujumbe wa mawaziri kadhaa akiwemo waziri wa biashara wa nchi hiyo huku akisema msafara wake utakuwa ndogo kutokana na changamoto ya ugonjwa wa Corona.

Amesema katika, mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Mje wa China na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikino wa Afrika Mashariki, Tanzania itaomba China kufungua wigo kwa Tanzania kuuza bidhaa za kilimo,Mifugo na uvuvi pamoja na kuendelea kushiriki katika maonyesho ya kibiashara na kiuchumi yanayo fanyika nchini China.

Aidha, amesema watazungumza kuhusu  China kushiriki kununua bidhaa zetu zitokanazo na madini hususani Dhahabu na vito vya thamani kama Tanzanite.

Mazungumzo mengine yatahusu uwezekano wa China kutoa Mikopo yenye riba nafuu hususani katika ujenzi wa miradi mikubwa ya umeme wa maji hususani maeneo ya Rumakali na Huji.

Maeneo mengine ni kuhusu misaada katika ujenzi wa chuo Cha usafirishaji,ujenzi wa barabara Zanzibar pamoka na upanuzi wa taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete.

Profesa Kabuni ameongeza kuwa watazungumza na Waziri Wang Yi ili kuona uwezekano wa kushirikiana kujenga Hospitali kubwa ya kitaifa Dodoma baada ya serikali kuhamia katika mji huo na idadi ya watu kuongezeka.

Taifa la Tanzania na taifa la China lina mahusiano mazuri ya muda mrefu ambayo yalianzishwa na Rais wa Kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere na Mao The Dong Rais wa China.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news