Rais Nyusi ajifunza jambo kutoka kwa Rais Magufuli

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Joseph Magufuli ameiagiza Wizara ya Afya nchini kujenga Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato na kukamilika kwa haraka bila kuwa na awamu mbili,anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.
Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi akiweka jiwe la msingi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato akiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli leo Januari 11, 2021. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Amesema ujenzi huo uende sambamba kwa wakati mmoja na ujenzi ukamilike bila kukwama na kuhaidi kubanana na wizara hiyo ili ujenzi ukamilike kwa wakati.

Rais Magufuli amesema, hospitali hiyo itahudumia wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo mikoa ya Mwanza,Kagera,Simiyu,Shinyanga,Kigoma,Tabora na Mara.

Katika hatua nyingine, Rais wa Msumbiji, Felipe Jacinto Nyusi amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli anashughulikia maisha ya wananchi kwa kuendelea kuboresha sekta ya huduma za afya nchini. 

Rais Nyusi amesema hayo leo Januari 11, 2021 wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali hiyo ya Rufaa ya Kanda-Chato iliyopo wilayani Chato mkoani Geita. 

“Nashukuru kwa Rais Magufuli kunipa nafasi ya kuweka jiwe la msingi kwa sababu Serikali inayoaangalia afya ya wananchi hiyo ni Serikali inayopenda wananchi, Rais Magufuli anashughulikia sana maisha ya wananchi wa Watanzania kwa kuangalia nyumba bora za kuishi, huduma za maji, chakula na afya bora,”amesema Rais Nyusi. 

“Kwa hiyo hii ni zawadi kwetu kwa kutupa nafasi ya kuweka jiwe la msingi katika hospitali hii kubwa, kule Msumbiji tumeanza (Program ya presidential initiatives) ya kujenga hospitali kila wilaya hii ni zawadi kubwa kwetu ya kutupa nafasi ya kuweka jiwe la msingi katika afya ya wananchi. 

"Tunatakiwa tujue watu wangapi na umbali kutoka hospitali moja hadi nyingine, sasa hiki tulichoona hapa ni mfano mzuri kwa sababu hii ni hospitali kubwa sana ambayo ipo karibu na mikoa mitano na nchi jirani za Kenya na Uganda naamini wataweza kuhudumiwa hapa,”amesema Rais Nyusi.

Aidha, Rais Nyusi amesema kuwa, Mkoa wa Geita ni tajiri kwa kuwa kuna kilimo cha mpunga, madini ya dhahabu na uvuvi wa samaki, hivyo kuwataka wananchi wa mkoa huo kufanyakazi kwa bidii. 

Wakati huo huo, Rais Dkt. Magufuli amemshukuru Rais Filipe Nyusi kwa kumtembelea Chato na kuongeza kuwa Msumbiji ni rafiki wa muda mrefu wa Tanzania na nchi hizo zina makubaliano ya kushirikiana katika mambo mbalimbali ikiwemo biashara. 

“Biashara kati ya Tanzania na Msumbiji imeongezeka, hadi kufikia mwaka 2020 ilifikia shilingi bilioni 93.6, kuna makampuni ya Msumbiji yanafanya kazi hapa na baadhi ya makampuni ya Tanzania yanafanya kazi kule,"amesema Rais Magufuli. 

Ameongeza kuwa, Januari 9, 1967 Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alitembelea Wilaya ya Chato na kufungua kiwanda cha pamba kilichojengwa kwa shilingi milioni mbili wakati huo ambacho kilikuwa na uwezo wa kuchakata marobota 20,000. 

Rais Magufuli amesema kuwa, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alichangisha fedha na yeye binafsi kuchangia shilingi 2,000 kwa ajili ya kujenga Bandari ya Nyamirembe ili iweze kusafirisha pamba kwenda Mwanza na Dar es salaam kwa hiyo wa Rais Nyusi amefika eneo ambalo alifika Mwalimu Nyerere 

“Kwetu sisi tunaona hii ni zawadi kubwa kwa wewe kuja kuzindua hospitali hii ambayo ni kubwa na itahudumia pia nchi za jirani. Nawashukuru Wizara ya Afya na Wakandarasi, nitawabana Wizara ya Afya ili hospitali hii ikamilike mara moja,"amesema Rais Magufuli 

Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda -Chato ilikadiriwa kutumia sh. bilioni 16, Serikali imeshatoa sh.bilioni 14 ambapo ujenzi umekamilika kwa asilimia 90 na makabidhiano yanatarajiwa kufanyika mwezi Machi, 2021. 

Ameongeza kuwa, awamu ya pili ya ujenzi imeshaanza kwa jumla ya gharama ya shilingi bilioni 14 ambapo mpaka sasa Serikali imetoa shilingi bilioni 4.1 na utekelezaji wake umefikia asilimia 37. 

“Hospitali ya Rufaa ya Kanda-Chato itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi zaidi ya milioni 14 ambapo kwa siku itakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa kati ya 700-1000,”amesema Waziri Dkt.Gwajima.

Amefafanua kuwa, maboresho ya afya nchini yamesaidia kuharakisha matibabu bobezi na kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje kutoka wagonjwa 682 mwaka 2014/15 hadi wagonjwa 42 mwaka 2020.

Hata hivyo, Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi amesema kuwa amejifunza kwa Rais Magufuli mpango mzuri wa kujenga hospitali za wilaya kwa ajili ya kuboresha huduma za afya na namna bora ya kuwahudumia wananchi.

Rais Nyusi amesema kuwa, wakati yuko kwenye harakati za kugombea Urais,alikuja Tanzania na kukutana na Mama Maria Nyerere na alimuhusia Nyusi ahakikishe amejenga angalau kiwanda kimoja cha dawa kwa sababu watu wengi wanakufa kwa ajili ya kukosa aspirin.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news