Rhobi Samwelly afungua mwaka 2021 kwa kuwapa tabasamu mabinti 225 mkoani Mara

NA FRESHA KINASA

Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania (HGWT) linalojihusisha na kutoa hifadhi kwa wasichana waliokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly amesherehekea mwaka mpya leo Januari Mosi 2021 kwa kushiriki chakula cha pamoja na wasichana 225 waliopo Kituo cha Nyumba Salama Kiabakari mjini Butima wanaohifadhiwa kituoni hapo.
Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwelly (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wasichana wa Kituo cha Nyumba Salama Kiabakari Butiama baada ya kushiriki chakula cha pamoja leo Januari Mosi, 2021.

Katika ujumbe wake, Rhobi ametoa wito kwa wazazi na walezi nchini kujenga tabia ya upendo kwa watoto wao na kutowafanyia vitendo vya ukatili ambavyo vinaweza kuwafanya kuishi bila amani na kusababisha wasiyafikie malengo yao, kutokana na kufanyiwa visa mbalimbali vya ukatili ikiwemo vipigo, kuozeshwa katika umri mdogo na kutumikishwa katika umri mdogo kinyume cha katiba ya nchi.

Rhobi amesema ni jukumu la wanajamii wote kuendelea kuwapenda na kuwathamini watoto wa kike sambamba na kulinda haki zao ikiwemo kuwasomesha na kuwasaidia mahitaji yao ya msingi katika kuwawezesha kusoma ili wafikie ndoto zitakazowasaidia kuleta mapinduzi chanya katika jamii yao na Taifa kwa siku za usoni.

Ameongeza kuwa, si vyema kuwafanyia vitendo vya ukatili wasichana hasa ikizingatiwa kwamba vitendo hivyo ni kinyume cha haki za binadamu na katiba ya nchi, ambapo amewaomba wanajamii kuwalinda dhidi ya aina zote za ukatili na kuwa mabalozi wa kuripoti katika mamlaka wahusika wanaofanya ukatili ili wawajibishwe kwa mujibu wa sheria.
Baadhi ya mabinti wa Nyumba Salama Kiabakari Wilaya ya Butiama wakila chakula leo Januari Mosi, 2021 katika kuuanza mwaka 2021. Chakula ambacho kimeandaliwa na Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwelly. 

Katika hatua nyingine Rhobi ameomba kila mmoja kuwa sehemu muhimu ya kuunga mkono mapambano dhidi ya ukatili wa watoto na wanawake kwani kufanya hivyo kutasaidia kuwafanya waishi kwa usalama na amani katika jamii na kusaidia kujenga jamii yenye kuthaminiana na kutambua misingi ya haki na usawa katika jamii.

Nao baadhi ya wasichana wanaohifadhiwa kituoni hapo, wamempongeza Mkurugenzi huyo kwa juhudi kubwa anazofanya ikiwemo kuwapa mahitaji yote wakiwa kituoni hapo tangu walipofika wakikimbia ukeketaji na ndoa za utotoni kutoka makwao, ambapo wamesema ni jukumu la watu wote kupinga ukatili wa kijinsia na kuwa tayari kuwasaidia wahanga wa vitendo hivyo na kuwafichua wanaojihusisha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news