Serikali yaingia makubaliano kuchimba madini ya Nickel Kabanga

Imeelezwa kuwa, Mkoa wa Kagera upo katika ukanda yanapopatikana madini ya Nickel na Bati hivyo ili nchi iweze kunufaika na madini hayo, Serikali imeamua kuingia makubaliano na Kampuni ya LZ Nickel Limited na makubaliano hayo yanalenga kuunda ubia utakaokuwa chini ya kampuni ya pamoja ijulikanayo kama Tembo Nickel Corporation Limited, anaripoti Tito Mselem (WM) Kagera.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wageni mbalimbali waliohudhuria hafla fupi ya utiaji saini Mkataba kati ya Serikali na Kampuni ya Lz Nickel limited kwa ajili ya uchimbaji wa madini hayo Ngara mkoani Kagera leo tarehe 19 Januari 2021.

Hayo yameelezwa leo Januari 19, 2021 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Jonh Pombe Magufuli alipokuwa kwenye hafla ya utiaji saini wa mkataba kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kampuni ya LZ Nickel Limited ya nchini Uingereza.

Rais Magufuli amesema, ikumbukwe kuwa madini ya Nickel katika eneo la Kabanga Wilaya ya Ngara mkoani Kagera yaligunduliwa mwaka 1976 na utafiti wa kina wa madini ya nickel na madini mengine katika eneo hilo ulianza toka miaka ya 2000 na kugundulika kuwa nickel iliyopo eneo hilo ni daraja la kwanza na ni madini bora duniani.

“Nimetaarifiwa kuwa kutokana na utafiti wa madini ya nickel katika eneo la Kabanga, mashapo yapatayo takribani tani milioni 51.73 za madini ya nickel zimegundulika ambazo zitachimbwa kwa miaka 32 na ukubwa wa eneo la mradi ni kilomita za mraba 201.85 ambapo Kabanga ndiyo eneo lenye madini mengi zaidi duniani, huu ni mradi mkubwa sana,”amesema Rais Magufuli.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wageni mbalimbali waliohudhuria hafla fupi ya utiaji saini Mkataba kati ya Serikali na Kampuni ya Lz Nickel limited kwa ajili ya uchimbaji wa madini hayo Ngara mkoani Kagera leo tarehe 19 Januari 2021.

“Ni azma ya Serikali kuona kuwa nchi ya Tanzania inanufaika na madini yake na pia kuona wawekezaji wanapata manufaa kwa kuwekeza nchini. Kupitia mradi huo Serikali itapata manufaa mbalimbali kupitia kodi, tozo, ajira, huduma kwa jamii na ununuzi wa bidhaa na huduma zinazopatikana hapa nchini. Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa shughuli za uchimbaji, uchenjuaji na uchakataji wa madini zinasimamiwa vizuri ili tuweze kunufaika na madini yetu,”ameongeza Rais Magufuli.

Kwa upande wake Waziri wa Madini, Doto Biteko alimpongeza Rais Magufuli kukubali kuja kushuhudia hafla hiyo ya kutiliana saini makubaliano ya kuendesha uchimbaji wa madini ya Nickel kwa ubia na Kampuni ya LZ Nickel Limited na pia alimshukuru kwa miongozo ambayo umekuwa ukiwapatia katika kusimamia Sekta ya Madini.

“Naomba kutoa pongezi za kipekee kwa timu yetu ya majadiliano kwa kufanikisha majadiliano kwa ufanisi mkubwa na uzalendo wa hali ya juu katika Sekta ya Madini hasa katika madini ya kimkakati kama Nickel.

"Ninatambua kazi hii ilikuwa ngumu na yenye jasho jingi, lakini mlijitoa kwa dhati hadi kufanikisha na leo hatimaye tunafungua ukurasa mpya,”amesema Waziri Biteko.

Aidha, Waziri Biteko amesema kuwa, Sekta ya Madini imeendelea kukua mwaka hadi mwaka na kuongeza mchango wake kwenye Pato la Taifa mathalani mwaka 2019 Sekta ya Madini imekuwa kwa asilimia 17.7 na kuongoza katika ukuaji ukilinganisha na sekta zingine hapa nchini ambapo mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 3.4 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 5.2 mwaka 2019. 

Pia sekta ya madini ndio inaongoza kwa sasa tangu mwaka 2020 kwa kuingizia nchi yetu fedha za kigeni na imeendelea kuimarika hata katika kipindi chote cha janga la virusi vya corona (COVID-19).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wageni mbalimbali waliohudhuria hafla fupi ya utiaji saini Mkataba kati ya Serikali na Kampuni ya Lz Nickel limited kwa ajili ya uchimbaji wa madini hayo Ngara mkoani Kagera leo tarehe 19 Januari 2021.

“Hivyo, ni matarajio yetu kuwa, Sekta ya Madini itazidi kukua na kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa na kuwanufaisha wananchi waliopo katika maeneo yanakopatikana madini kama ilivyo kwa madini ya Nickel ya Kabanga, unaamini kuwa hadi kufikia Mwaka 2025 mchango wa sekta hii utafikia asilimia 10 katika pato la Taifa kama inavyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo,”ameongeza Waziri Biteko.

Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila amesema, katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda kutokana na rasilimali madini, Serikali kupitia Wizara ya Madini ilikaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza katika tasnia ya uyeyushaji (smelting) na usafishaji (refining) madini ili shughuli hizi ziweze kufanyika nchini ambapo hadi sasa, Serikali imetoa leseni nne (4) za usafishaji (refinery) na leseni sita (6) za uyeyushaji (Smelting).

Prof. Msanjila ameongeza kuwa, hatua ya kukaribisha wawekezaji katika shughuli za uyeyushaji na uchenjuaji madini itawawezesha wachimbaji wa madini waongeze thamani ya madini yao nchini na hivyo kukuza Pato la Taifa na kuongeza ajira.

Naye Makamu wa Rais wa Kampuni ya Nickel, Anthony Von Christierson alisema, Kampuni ya LZ Nickel unauzoefu katika shughuli za madini kwa kipindi cha zaidi ya miaka 40, hivyo aliwahakikishia watanzania wana utaalam wa kutosha katika shughuli za uchimbaji na uchenjuaji madini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwashukuru Wananchi na kuwaaga mara baada ya hafla ya utiaji saini Mkataba kati ya Serikali na Kampuni ya Lz Nickel limited kwa ajili ya uchimbaji wa madini hayo mkoani Kagera leo tarehe 19 Januari 2021.

Vile vile, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia, Marco Kaguti, amesema kuwa, Mkoa wa Kagera kwa sasa umepiga hatua kubwa hususan katika madini ya bati ambapo uzalishaji umeongezeka kwa kiwango kikubwa na sasa takriban tani 1,4000 za madini hayo zinauzwa nje ya nchi kwa mwezi mmoja ukilinganisha nailivyokuwa hapo awali ambapo soko lake lilikuwa gumu.

Pia Christierson alisema mradi huo utasaidia kuongeza ajira ambapo wanategemea baada ya mradi kukamilika wataajiri zaidi ya watu 8,000 na kusaidia kuongeza pato la taifa ambapo madini yatakayopatika watagawa na Serikali sawa kwa sawa.

“Kabanga ndiyo eneo pekee lenye madini ya nickel mengi zaidi kuliko eneo lolote duniani hivyo, tutashirikiana kwa pamoja ili madini yaweze yapatikanayo sehemu hiyo yaweze kuwanufaisha watanzania wote,”ameongeza Christierson. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news