Shirika la Bima la Taifa latoa milioni 14.7/- kufanikisha Kombe la Mapinduzi

Shirika la Bima la Taifa Tanzania (NIC) limetoa mchango wa shilingi 14, 700,000 kwa ajili ya kufanikisha mashindano ya soka ya Kombe la Mapinduzi ya mwaka huu yanayotarajiwa kuanza leo Januari 5, 2021 katika Uwanja wa Amani jijini Zanzibar, anaripoti Mwandishi Diramakini (Zanzibar).

Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Dkt. Elirehema Doriye amemueleza Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita kwamba ameamua kuyapa msukumo mashindano hayo baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukaribisha mashirika,wafanyabiashara na wadau wa michezo kuchangia mashindano hayo.

Amesema, lengo la mchango huo ni kusaidia gharama za uendeshaji wa mashindano na zawadi ya mchezaji bora kwenye michuano hiyo inayoshirikisha timu tisa, nne kutoka Zanzibar na tano kutoka Tanzania Bara.

Mkurugenzi Doriye amemuahidi Waziri Tabia Maulid Mwita kwamba NIC itaendelea kuwa washirika wa karibu wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi kwa miaka mengine ijayao.
Waziri Tabia Maulid Mwita akizungumza kwenye mkutano na viongozi wa Shirika la Bima la Taifa Tanzania (NIC) uliofanyika Ofisi ya Wizara Migombani jijini Zanzibar.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika wizarani kwake Migombani, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita amelishukuru Shirika la Bima la Taifa Tanzania kwa msaada huo na ahadi walizotoa kwa miaka ijayo katika kuendesha mashindano hayo.

Amesema mchango wa shilingi milioni 14.7 waliotoa utasaidia sana katika kufanikisha mashindano ya mwaka huu ambayo yemekuwa endelevu tokea yalipoanzishwa kitaifa mwaka 2007.

Waziri Tabia amewaeleza viongozi wa Shirika la Bima la Taifa Tanzania kuwa Serikali imeazimia kuimarisha michezo mbalimbali ikiwemo Ligi Kuu ya Zanzibar na michango ya wadau inahitajika katika kufanikisha lengo hilo.

Ameahidi kuwa wizara itaendelea kushirikiana na shirika hilo na amewakaribisha kutumia vyombo vya habari vilivyo chini ya wizara hiyo katika kuimarisha shughuli zao za kibiashara nchini,

Post a Comment

0 Comments