Simba SC, Namungo FC zaipaisha Tanzania soka la Kimataifa

Wekundu wa Msimbazi, Simba SC wamefanikiwa kwenda hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa 4-0 dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Kupitia kandanda safi ambalo limetandazwa katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, Simba SC kupitia hamasa yao ya War in Dar imetoa majibu.

Kwa matokeo ya leo, Simba SC inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 4-1 kufuatia kufungwa 1-0 kwenye mchezo wa kwanza Jumatano iliyopita mjini Harare, Zimbabwe.

Aidha, hii inakuwa mara ya tatu kwa Wana Msimbazi hao kutinga hatua ya makundi baada ya mwaka 2003 walipoitoa Zamalek ya Misri waliokuwa mabingwa watetezi na 2018 walipoitoa Nkana FC ya Zambia. 

Simba SC inayofundishwa na Mbelgiji, Sven Ludwig Vandenbroeck ilikwenda kupumzika ikiwa inaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Erasto Edward Nyoni kwa penalti dakika ya 39 baada ya beki mwenzake, Shomari Salum Kapombe kuvutwa jezi na Tawana Chikore. 

Aidha, kipindi cha pili Kapombe aliifungia Simba SC bao la pili dakika ya 61 akimalizia mpira uliotemwa na kipa Francis Tizayi kufuatia shuti la kiungo Rally Bwalya. 

John Raphael Bocco ambaye ni nahodha aliyetokea benchi kipindi cha pili kuchukua nafasi ya mshambuliaji mwenzake,Meddie Kagere akaifungia Simba SC bao la tatu dakika ya 90 akimalizia pasi ya Bwalya. 
Wakati huo huo, mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Tanzania, kiungo Clatous Chotta Chama ameifungia Simba SC bao la nne kwa penalti dakika ya 90 baada ya yeye mwenyewe kuvutwa kwenye boksi na Gift Bello.

Haya yanajiri baada ya msimu mbaya uliopita timu za Tanzania, Simba na Azam FC kutolewa mapema michuano ya Afrika, lakini mwaka huu mambo yanaonekana kuwa moto moto.

Tayari vijana kutoka Lindi, Namungo FC wametinga kwenye mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho. 

Januari 5, 2021 Namungo FC imefanikiwa kusonga mbele kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika baada ya sare ya 3-3 na wenyeji, na Al Hilal Obayed.

Mtanange ho wa nguvu ulichezwa katika dimba la Al-Hilal mjini Omdurman, Sudan majira ya jioni.

Matokeo hayo yanaifanya Namungo FC kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 5-3 na sasa itamenyana na moja ya timu zitakazotolewa kwenye Ligi ya Mabingwa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho. 

Hata hivyo, droo ya hatua ya makundi ya michuano hiyo itafanyika Ijumaa hii huko
jijini Cairo nchini Misri ambapo ni makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Post a Comment

0 Comments