Simba SC yaandaa kipigo cha kufungua mwaka kwa FC Platinum

Wekundu wa Msimbazi, Simba SC wamepania kulipiza kisasi cha aina yake Januari 6, 2021 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Msemaji Mkuu wa Simba SC, Haji Sunday Manara.

Hamasa kuu ikiwa imetolewa kwa mashabiki kuupamba uwanja huo ambao unakusanya maelfu ya watu, wimbo mkuu kwa ajili ya kuwapa zawadi FC Platinum ya nchini Zimbabwe umetajwa kuwa ni WIDA! WIDA! WIDA! WIDA! WIDA! WIDA!.

Wimbo ambao umetajwa kuwa na nguvu ya kushinikiza ushindi kwa timu hiyo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika

Afisa Habari wa Simba SC, Haji Manara ameyabainisha hayo Januari 4, 2021 alipozungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kuelekea kwenye mchezo huo wa marudiano jijini humo.

"Sisi Simba SC mtaji wetu mkubwa wa ushindi ni mashabiki wetu kujaa uwanjani, tunaamini wakija kwa wingi watawapa hamasa wachezaji wetu kucheza kwa kujituma na kupata ushindi katika mchezo dhidi ya FC Platinum,"amesema Manara.

Manara amesema tayari Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) limeridhia mchezo huo uchezwe majira ya saa 11 alasiri kwa saa za Afrika Mashariki ili kutoa nafasi zaidi kwa mashabiki wa soka hususan wale wanaotoka sehemu za mbali.

"Majibu ya barua kutoka CAF wameridhia mechi ichezwe saa 11 Alasiri, CAF walipanga mchezo uchezwe saa 1 usiku, kwa upande wetu tulisema hapana lazima tuombe saa 11 ili kuwapa nafasi mashabiki wetu kushuhudia mchezo huo kutokana na miundombinu ya mji wetu wa Dar es Salaam, hulka za mashabiki, mwisho wa siku tuwape nafasi mashabiki kurejea kwao mapema,"ameeleza Manara.

Amesema Simba SC imeiandika barua CAF kuhusu suala la kujaza mashabiki katika dimba la Benjamin Mkapa kwa asilimia 100 ya uwezo wa Uwanja huo, amesema hawatauza tiketi kwa asilimia zote 100 ya idadi ya uwanja hadi CAF watakorudisha majibu ya ruhusa ya kujaza uwanja huo wa Benjamin Mkapa.

Wakati huo huo Manara amesema kuwa, kiungo mzawa Jonas Mkude hajafukuzwa ndani ya kikosi hicho bali suala lake lipo kwenye kamati ya nidhamu.

Ameyasema hayo baada ya Desemba 28,2020 taarifa rasmi kutoka Simba SC kueleza kuwa kiungo huyo ambaye ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck amesimamishwa ndani ya kikosi hicho kutokana na utovu wa nidhamu.

Mkude tayari amekosa mechi mbili ambapo ya kwanza ilikuwa ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Majimaji na ule wa pili wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ihefu FC zote zilichezwa Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

"Kuhusu Jonas Mkude ijulikane tu kuwa mpaka sasa ni sehemu ya Simba hajafukuzwa kazi, amepitia changamoto kama mfanyakazi mwingine kokote. Mkude ni mchezaji wa Simba. Jambo lake lipo kamati ya maadili. Mkude hajafukuzwa Simba. Bila shaka yoyote baada ya kamati atarejea klabuni. Huyu ndiye mchezaji mwandamizi ndani ya Simba kwa miaka 10,”amesema Haji Manara.

Wekundu wa Msimbazi ili kutinga hatua ya makundi wana kazi ya kusaka ushindi wa mabao zaidi ya mawili na kulinda lango lao lisiguswe na wapinzani hao waweze kusonga mbele.

Post a Comment

0 Comments