Simba SC yaanza kwa ushindi Kombe la Mapinduzi, Yanga watangulia nusu fainali

Wekundu wa Msimbazi, Simba SC imeanza vema michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya wenyeji, Chipukizi FC ya Pemba kwenye mchezo wa kundi B, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mtanange huo umepigwa katika dimba la Amaan lililopo jijini Zanzibar Januari 8, 2021. Miraj Athumani (Madenge) ametikisa nyavu za Chipukizi FC mara mbili baada ya kuanza na bao la dakika ya 53 na 83.

Awali mshambuliaji, Meddie Kagere alifunga bao la kwanza katika kipindi cha kuelekea mapumziko dakika ya 45 kufuatia Chipukizi kutangulia kwa bao la Fakhi Mwalimu Sharrif dakika 36.

Wakati huo huo, Wanajangwani, Yanga SC imetinga nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga Namungo FC bao 1-0, mchezo uliochezwa usiku wa Januari 8, 2021 kwenye dimba la Amaan jijini hapa.
Zawadi Mauya ameipatia Yanga SC bao ndani ya dakika ya 24 baada ya kupia shuti kali lililotinga moja kwa moja golini katika mechi iliyokuwa na ushindani mkali.

Mechi ya kwanza Yanga walicheza na Jamhuri ya kisiwani Pemba ambapo timu hizo zilitoka sare tasa hivyo mechi ya kwa Yanga inatoa mwanga wa wao kusonga mbele kama matokeo yataendelea kubaki hivi, kwani hadi sasa wao wanaongoza kwa alama nne katika kundi lao.

Aidha, kwa upande wa Namungo FC wao ni mechi ya kwanza ambapo baada ya hii watacheza na Jamhuri ili kujua hatma yao kwenye mashindano haya ambayo kilele chake ni Januari 13, 2021. 

Timu zote mbili kipindi cha kwanza zilicheza kwa kushambuliana na kukosa nafasi kadhaa za wazi ambapo Namungo FC dakika ya 33 walikosa mpira ukiwa ni wa piga nikupige langoni mwa wapinzani wao Yanga SC.

Awali Azam FC ililazimishwa sare ya 1-1 na Mlandege katika mchezo wa Kundi C Kombe la Mapinduzi katika dimba hilo la Amaan jijini Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news