Uganda yawagomea waangalizi wa Marekani uchaguzi wa kesho

Serikali ya Marekani imetangaza kuwa, haitatuma waangalizi kufuatilia uchaguzi mkuu wa Uganda utakaofanyika kesho Januari 14, 2021. Asilimia 75 ya maafisa wake wamenyimwa vibali vya kufuatilia uchaguzi huo nchini humo.
Balozi wa Marekani nchini Uganda, Natalie Brown amesema kwamba, Tume ya Uchaguzi ya Uganda haikutoa sababu yoyote ya kukataa maombi hayo licha ya juhudi kadhaa za kutaka maelezo kutoka kwa ubalozi wa Marekani nchini humo. 

Amesema kwamba, waangalizi wa kutoka ubalozi huo, ambao wengi wao ni raia wa Uganda, wamenyimwa fursa ya kutumikia raia wenzao.Balozi huyo amesema, hatua hiyo itapelekea uchaguzi wa Uganda kukosa uwazi, imani na uwajibikaji. 

Pia Marekani imeituhumu hatua ya Serikali ya Uganda kuzima mitandao yote ya kijamii, wakati nchi hiyo inaandaa uchaguzi mkuu, huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres akitoa wito kwa utawala wa Uganda kuheshimu haki za kibinadamu.

Guterres ameitaka Serikali na wagombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo kujizuia na uvunjani wa sheria na vitendo vinavyoweza kuchochea ghasia.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amezituhumu kampuni zinazomiliki mitandao ya kijamii hasa Facebook na Twitter, kwa kile ambacho alidai kuwa ni majivuno na upendeleo, akisema kwamba ameamrisha zifungwe nchini humo kwa sasa.

Baada ya wito huo, Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC) iliagiza jana makampuni yanayotoa huduma ya intaneti kufunga mitandao ya kijamii na programu tumishi zote za mawasiliano.

Mkurugenzi Mkuu wa UCC, Irene Sewankambo aliyaandikia barua makampuni hayo na kuyataka kuhakikisha kwamba huduma ya mitandao ya kijamii imesitishwa.

Kufuatia agizo hilo, watumiaji wa mitandao ya kijamii waliripoti visa vya kutoweza kuingia kwenye mitandao kama vile Facebook na Twitter, kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor la Uganda.

Mitandao mingine ni kama vile Viper, Whatsapp na Signal.Vyombo vya habari nchini Uganda viliripoti kwamba raia wengi walikuwa wanajaribu kutumia njia mbadala za VPN ili kuwasiliana kupitia baadhi ya App za mawasiliano nchini humo.

Aidha, Marekani kwenyewe tayari Twitter na Facebook zimefunga kurasa za mitandao ya kijamii ya Rais Donald Trump kwa kuchochea wafuasi wake kuvamia bunge la Marekani kuhusiana na kushindwa kwake katika uchaguzi.

Wakati huo huo, Rais wa sasa Yoweri Museveni anawania muhula wa sita, lakini serikali yake inakosolewa kwa ukiukaji mkubwa wa haki na kukandamiza upinzani.

Rais Museveni mwenye umri wa miaka 76, anakabiliana na nyota wa muziki aliegeuka mbunge Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine mwenye umri wa miaka 38.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news