UN yataja ushirikiano kuwa nguzo muhimu Duniani

Umoja wa Mataifa umezindua ripoti yake ya mwisho ya maoni ya wakazi wa Dunia kuhusu chombo hicho kinapotimiza miaka 75 tangu kuanzishwa kwake.
Wafanyakazi wa kijamii wanaowezeshwa na Umoja wa Mataifa wakihamasisha umma kuhusu mbinu za kujikinga na virusi vya Corona (COVID-19) na kusambaza vifaa vya usafi miongoni mwa kaya maskini nchini Bangladesh.(Picha na Fahad Kaize/UNDP Bangladesh/Diramakini).

Kwa mujibu wa UN kipaumbele chao cha muda mfupi ni huduma za msingi kama vile afya, elimu, maji na huduma za usafi ikiwemo ushirikiano wa Kimataifa.

Watu zaidi ya milioni 1.5 kutoka mataifa 195 walishiriki katika kampeni hiyo ya kukusanya maoni kupitia utafiti na majadiliano.

Kuhusu kilichojitokeza katika kampeni hiyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema, mchakato huo wa maoni ya UN75 umeonyesha kwamba asilimia 97 ya walioshiriki wanunga mkono ushirikiano wa kimataifa katika kushughulikia changamoto za kimataifa. 

"Na hii inaonyesha dhamira muhimu katika ushirikiano wa kimataifa na kwa lengo la Umoja wa Mataifa. Na sasa ni juu yetu nchi wanachama na sekretariati ya Umoja wa Mataifa kukidhi matarajio ya watu tunaowahudumia,"amesema.

Washiriki wengi hususan katika nchi za kipato cha chini na kati wametaka usaidizi zaidi kwa watu walio hatarini, jambo ambalo kwa watu wa kipato cha juu halikupatiwa kipaumbele. 

Tishio la mabadiliko ya tabianchi na mazingira lilionekana kubwa zaidi kwa asilimia 73 ya washiriki wa utafiti kutoka Amerika Kusini na Caribean wakati ni asilimia 37 tu ya washiriki kutoka nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara walioona kuwa hoja hiyo ni tatizo. 

Hata hivyo suala lingine ambalo kwa ujumla linatakiwa kupatiwa kipaumbele ni fursa za ajira, haki za binadamu na mizozo. 

Maoni hayo yanafuatia utafiti wa miezi 12 ulioanza mwezi Januari mwaka 2020 ambapo Umoja wa Mataifa ulihoji wakazi wa Dunia kuhusu matarajio na hofu yao juu ya mustakabali wa dunia hususan chombo hicho kilichotimiza miaka 75. 

Licha ya changamoto hizo, asilimia 49 ya washiriki wanaamini kuwa maisha yatakuwa bora mwaka 2045. Akitangaza matokeo ya utafiti na ukusanyaji wa maoni hayo kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswis, Fabrizio Hochschild, mshauri maalum wa Katibu Mkuu kuhusu maadhimisho ya miaka 75 ya Umoja wa Mataifa amesema, njia mbalimbali zilitumika katika kukusanya maoni na kupata tathimini ikiwa ni pamoja na majadiliano, maoni, njia mbalimbali bunifu, akili bandia, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Ameongeza kuwa, mbali ya mbinu hizo pia kulifanyika tafiti mbili huru zikitumia maswali hayo hayo ili kupata ukweli hali halisi na matokeo yake yalikuwa ya kusisimua na mambo yaliyojitokeza ni pamoja na masuala ya umoja kwa mrika, makundi katika kipato kwenye kanda mbalimbali na viwango vya elimu. 

Pia maoni yalikuwa sawa lilipokuja suala la matumaini ya watu na hofu zao kuhusu mustakbali wao, pia matarajio yao katika suala la ushirikiano wa kimataifa.

Katika vipaumbele vya haraka baada ya virusi vya Corona (COVID-19) Dunia imeungana katika kutaka fursa bora zaidi za kupata huduma za msingi kama za afya, elimu bora, maji na usafi na pia wanataka mshikamano zaidi na maeneo na jamii zilizoathirika vibaya zaidi.

Ukusanyaji maoni hayo wa Umoja wa Mataifa limekuwa ni moja ya zoezi kubwa na lenye matamanio zaidi kufanywa na Umoja wa Mataifa ili kupata maoni ya umma kuhusu vipaumbele kwa ajili ya kujikwamua na janga la COVID-19.

Washiriki wengi pia wamezungumzia kuhusu Umoja wa Mataifa kuongoza katika ushiriukiano wa kimataifa katika kushughulikia changamoto za kimataifa za muda mrefu na za muda mfupi.

Matokeo yanaonyesha kuwa wengi pia wanataka shirika la umoja wa Mataifa kuwa bunifu, kuwa jumuishi zaidi, kuwa shirikishi, lenye kuwajibika na lenye ufanisi zaidi.

Katika utafiti huo na majadiliano ya UN75 yaliyofanyika kote duniani, washiriki wametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuwa na uongozi wa kimaadili, wenye mabadiliko na Baraza la Usalama linalozingatia matakwa ya watu linaowahudumia na kuwa na mfumo wa Umoja wa Mataifa ambao ni shirikishi na jumuishi.

Pia wametaka kuwe na maboresho na uelewa wa kazi za Umoja wa Mataifa miongoni mwa raia wa Dunia na shirika ambalo linaonyesha kujali zaidi mahitaji ya watu.

Post a Comment

0 Comments