Wataalam Sekta ya Maji watakiwa kutumia taaluma zao vizuri

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewataka wataalam Sekta ya Maji kote nchini kutumia utaalam wao ili wananchi wapate huduma ya uhakika na toshelevu ya majisafi na salama, anaripoti Mohamed Saif (Tarime).
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akimtua ndoo kichwani mmoja wa akina mama wa wilayani Tarime wakati wa ziara yake kwenye mradi wa maji wa Gamasara.

Ametoa maelekezo hayo Januari 5, 2021 wakati wa ziara yake ya kukagua mradi wa maji wa Gamasara Wilayani Tarime mkoani Mara na kuzungumza na wanufaika wa mradi huo ambao kwa nyakati tofauti walimueleza changamoto zilizopo kwenye mradi.

Miongoni mwa changamoto zilizoelezwa na wananchi hao ni pamoja na mradi kushindwa kutoa maji inavyopasa kwani kuna wakati mabomba huwa hayatoi maji.

Mara baada ya kujionea hali halisi ya mradi na maelezo ya wananchi wa maeneo husika, Waziri Aweso alisisitiza kuwa dhamira ya Serikali ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni kuwafikishia huduma ya maji wananchi wake na kwamba hatakubali kuwa kikwazo cha kufikiwa kwa dhamira hiyo na hivyo aliwataka wataalm wote kwenye Sekta ya Maji kujitathmini.

Waziri Aweso ameelekeza Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mara kuhakikisha maboresho yanafanyika ili mradi uweze kutoa maji kama inavyopasa kwa lengo la kuhudumia wananchi wengi zaidi.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akikagua tenki la maji mradi wa Gamasara Wilayani Tarime Mkoani Mara.

Amesema kuwa, wananchi wanachohitaji ni maji na aliwaelekeza wataalam katika Sekta ya Maji kujiepusha na porojo badala yake wahakikishe wanajikita na kudumu kwenye falsafa ya maji bombani.

“Wataalam wetu kwenye Sekta ya Maji acheni porojo, elekezeni taaluma zenu na ubunifu katika kuhakikisha wananchi wanaondokana na kero ya maji,” ameelekeza Waziri Aweso.

Aliongeza kuwa, “unapokuwa mtaalam lazima utoe ushauri kulingana na utaalamu wako, tunapoanzisha mradi maana yake ni wananchi wapate huduma, wataalam tutumie taaluma zetu kusaidia wananchi wapate maji,” ameelekeza Waziri Aweso.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akimsikiliza Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tarime Mhandisi Marwa Murasa wakati wa ziara ya kukagua mradi wa maji wa Gamasara

Aidha, Waziri Aweso alizielekeza jumuiya za Watumia Maji kote nchini kuhakikisha zinasimamia vizuri miradi ya maji kwenye jumuia zao ikiwa ni pamoja na kuongeza umakini kwenye makusanyo kwa lengo la kuwa na miradi endelevu.

“Miradi mliyokabidhiwa inapaswa kuwa endelevu, sasa ni jukumu lenu kuhakikisha hili linafikiwa, hakikisheni mnashirikiana, mnaitunza na mnaisimamia vizuri,”ameelekeza Waziri Aweso.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news