Waziri Mkuu azindua barabara ya Matemwe-Muyuni

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua barabara ya Matemwe hadi Muyuni yenye urefu wa kilomita 7.58 iliyojengwa na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Cooperation (CCECC) kutoka China kwa gharama ya shilingi bilioni 5.48 zikiwa ni mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), anaripoti Mwandishi Diramakini. 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua barabara ya Matemwe hadi Muyuni yenye urefu wa kilomita 7.58 katika Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja, barabara hiyo imejengwa na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Cooperation (CCECC) kwa ufadhili kutoka benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa gharama ya shilingi bilioni 5.48, Januari 7, 2021 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu/ Diramakini).

“Barabara hii ni kiungo muhimu kwa wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja na maeneo mengine ya mashariki mwa Kisiwa cha Unguja kwani imeungana na barabara nyingine kuanzia maeneo ya Chwaka kuelekea Uroa, Pongwe, Kiwengwa, Pwani Mchangani, Matemwe hadi Muyuni. 

Waziri Mkuu amezindua barabara hiyo leo Januari 7, 2021 akiwa katika Wilaya ya Kaskazini A, mkoa wa Kaskazini Unguja, kisiwani Unguja ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya kutimiza Miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964. 

Amesema uzinduzi huo ni kielelezo cha juhudi kubwa za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miundombinu ya barabara Mijini na Vijijini kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wote wa Zanzibar. 

“Hii itakuwa ni chachu kubwa ya kurahisisha shughuli za kiutalii na sekta nyingine zikiwemo kilimo, uvuvi na biashara kuelekea katika kujenga na kuimarisha uchumi wetu. Kwa msingi huo, nitoe wito kwa wananchi kuchangamkia fursa zinazojitokeza kutokana na uwepo wa barabara hii ili kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na uchumi wa Zanzibar kwa ujumla,”amesema. 

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema uwepo wa barabara hiyo utawarahisishia wakaazi na wageni katika maeneo ya Matemwe, Mbuyu Tende hadi Muyuni na maeneo mengine ya Mkoa wa Kaskazini kuondokana na adha ya usafiri waliyokuwa wakikabiliana nayo kabla ya ujenzi wake. 

Waziri Mkuu amesema ni vyema wananchi wote wakatambua kwamba kupatikana kwa mafanikio hayo katika sekta ya barabara kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuwepo kwa umoja na mshikamano katika kutekeleza majukumu yao ili kuharakisha maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. 

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha kuwa inawawezesha wananchi wake katika nyanja zote za kiuchumi na kijamii kwa kuwapatia huduma bora za msingi katika maendeleo ikiwemo kuendelea kuzijenga barabara mbalimbali Mijini na Vijijini, Unguja na Pemba,"amesema. 

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wote wa Zanzibar kuepuka kujenga ndani ya eneo la hifadhi ya barabara (road reserve) kwa lengo la kuondoa usumbufu wakati wa upanuzi wa barabara na miradi mingine ya maendeleo. 

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa namna alivyoanza kutekeleza majukumu yake ya kuiongoza Zanzibar. 

“Katika kipindi hiki kifupi tangu aingie madarakani, sote tumeshuhudia dhamira na azma yake njema ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar. Kupitia mwanzo huu mzuri aliouonesha, binafsi ninaamini tayari wananchi tumeshaona nuru ya kiongozi wetu huyu. Hivyo, nasi hatunabudi kumuunga mkono ili aweze kutimiza ndoto yake ya kujikwamua kiuchumi. Hakika “Yajayo Yanafurahisha” 

Awali, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Rahma Kassim Ali alisema kukamilika kwa barabara hiyo kutaboresha maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa mkoa wa Kaskazini Unguja pamoja na mikoa jirani. 

Amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea na ujenzi wa barabara ili kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, hivyo aliwaomba wananchi wahakikishe wanailinda miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news