Waziri, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara wafanya ziara FCT, watoa rai kwa wafanyabiashara

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Geoffrey Mwambe (Mb) amewasihi wafanyabiashara kuwasilisha rufaa zao iwapo hawakuridhika na maamuzi yanayotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (EWURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri na Usalama wa Anga (TCAA), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa nchi Kavu (LATRA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) pamoja na mamlaka ambazo sheria za uundaji wake zinaelekeza rufaa za maamuzi yake zifanywe na FCT, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Geoffrey Mwambe (Mb) akisaini kitabu cha wageni alipotembelea Baraza la Ushindani, akiambatana na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (Mb) wa kwanza kulia naye akisaini kitabu cha wageni. Aliyesimama katikati ni Mrajis wa Baraza la Ushindani, Bw. Renatus Rutatinisiwa.

Waziri Mwambe ameyasema hayo alipokuwa akiongea na menejimenti na wafanyakazi wa FCT alipofanya ziara katika Baraza hilo akiambatana na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) pamoja na baadhi ya wakurugenzi wa Wizara ya Viwanda na Biashara.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Geoffrey Mwambe (Mb) akitoa maelekezo kwa menejimenti ya Baraza. Kulia ni Naibu Waziri wa Viwanda Mhe. Exaud Kigahe (Mb) na kushotoni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Bw.Ludovick J.Nduhiye 

Akiwa katika ziara hiyo katika baraza hilo lenye jukumu la kupokea,kusikiliza na kuamua kesi za rufaa zinazotokana na maamuzi ya Tume ya Ushindani (FCC) pamoja na Mamlaka za Udhibiti, Mhe. Waziri amesema wananchi wasiogope kwenda kutafuta haki katika baraza hilo ambalo limepewa hadhi ya kimahakama ya utoaji haki kwenye masuala ya ushindani udhibiti wa soko, kumlinda mlaji na maamuzi ya kesi za rufaa yanayotolewa na baraza hilo ni ya mwisho. 
Aidha Waziri Mwambe amewataka watumishi wa Baraza la Ushindani (FCT) kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kuepuka vitendo vya rushwa wakati wakiwahudumia wafanyabiashara wanaofika katika baraza hilo kutafuta haki katika kesi zinazohusu biashara zao na wajiendeleze kielimu ili kuendana na wakati.
Waziri wa Viwanda na Biashara,Mhe. Geoffrey Mwambe (Mb) akitoa maelekezo kwa menejimenti ya Baraza (haipo pichani) Kulia ni Naibu Waziri wa Viwanda Mhe. Exaud Kigahe (Mb) na kushotoni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Bw.Ludovick J.Nduhiye 

Naye Naibu Waziri akiongea na watumishi wa baraza hilo aliwapongeza kwa kufanya kazi vizuri na amewaahidi kuwa Wizara ya Viwanda itaendelea kushirikiana na Baraza hilo ambalo ni muhimu katika kuendeleza biashara nchini ili kuliwezesha kufanya kazi kwa ufanisi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news