Yajayo Zanzibar yazidi kutoa faraja,ni mwendo wa elimu bora

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla amesema Tangazo la Elimu Bila Malipo lililotolewa mara tu baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 lilikuwa na maana ya kuongeza fursa za kupata elimu iliyo bora kwa wote, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Skuli ya Sekondari ya Donge Mkoa Kaskazini Unguja ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya kusherehekea Miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964. 
Amesema, elimu bora na ya kiwango ndio inayomuwezesha mwanaadamu hasa watoto wa Taifa hili kukabiliana vyema na changamoto mbalimbali watakazokuwa wakipambana nazo katika maisha yao, wazazi na hata Taifa kwa ujumla. 

Hemed ameeleza kwamba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane chini ya usimamizi wa Rais wake Dkt. Hussein Ali Mwinyi itaendelea kutoa elimu bila ya malipo kwa taaluma ya msingi hadi sekondari ili kuwawezesha wananfunzi wenye sifa kupata elimu bila ya vikwazo. 

“Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Aman Karume aliyeongoza Mapinduzi ya Zanzibar kwa lengo la kuwakomboa Wazanzibari alitangaza Elimu bure kwa wote bila ya ubaguzi wowote mnamo Tarehe 23 Septemba 1964,"amesisitiza Mheshimiwa Hemed Suleiman. 

“Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Saba, Dkt. Ali Mohamed Shein naye alitoa Tamko katika Sherehe za Miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar pale Uwanja wa Aman Tarehe 12/01/2015 kwa kufuta kabisa ile michango midogo midogo ya Skuli, kwa nganzi ya Elimu ya Msingi na baadae Sekondari,” amekumbusha Mheshimiwa Hemed. 

Amewapongeza wananchi wa Donge kwa jitihada, mshikamano,ushirikiano na ustahamilivu wao wa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kujiletea maendeleo hasa katika sekta muhimu ya elimu ambapo sasa jamii inashuhudia matunda hayo. 

Makamu wa Pili wa Rais amesema kwamba Donge imekuwa mfano mzuri wa kuigwa na Jamii nyengine hapa Nchini kwa kujenga Skuli kubwa na ya Kisasa ya Ghorofa jambo ambalo limesaidia kupunguza changamoto za ufinyu wa nafasi katika Elimu ndani ya Wilaya ya Kaskazini B. 

Amesema ujenzi wa Skuli hiyo ni kielelezo cha juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaletea Maendeleo Wananchi wake ikiwa ni Mkakati wa kuhakikisha nafasi za masomo kwa Watoto wa Visiwa vya Unguja na Pemba zinapatikana katika maeneo yote. 

“Fursa sawa za kupata Elimu ni miongoni mwa malengo ya Mapinduzi yetu ya Mwaka 1964 ambapo hivi sasa tumo katika kuadhimisha Miaka 57,”ameeleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar. 

Mheshimiwa Hemed amesema, historia inaeleza kwamba Wilaya ya Kaskazini B haikuwa na hata Skuli Moja ya Sekondari kabla ya Mapinduzi na wakati huo Elimu ilikuwa ikitolewa kwa ubaguzi katika maeneo na watu maalum. 

Amebainisha kwamba hivi sasa Wilaya ya Kaskazini B ina jumla ya Skuli 11 za Sekondari pekee ikiwa ni maendeleo makubwa na ni Matunda ya Mapinduzi ya Mwaka 1964 ambapo Wananchi wanapaswa kujivunia kwa vile Elimu imekuwa ikiwafikia Wananchi pale walipo. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesisitiza umuhimu wa Wazazi, Walezi, Walimu na Kamati za Maskuli Nchini kuendelea kushirikiana hatua itakayorahisisha upatikanaji wa Maendeleo ya haraka ya Watoto wao.
Aidha Mheshimiwa Hemed Suleiman amewakumbusha Wanafunzi kuyatumia mazingira bora wanayowekewa na Serikali kwa kuzidisha juhudi za masomo zitakazozalisha matokeo mapya ya viwango vya juu katika Mitihani yao ya Taifa. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameridhika na gharama zilizotumiwa za Ujenzi wa Mradi wa Skuli ya Sekondari ya Donge jambo ambalo wasimamizi wa Mradi huo wanastahiki kupongezwa kutokana na Uzalendo wao waliyouonyesha. 

Amesema alikuwa akifuatilia muenendo wa watangulizi wake katika hafla hiyo na kama asingeridhika na Mradi huo aliweka wazi kwamba asingeufungua Mradi huo na angelazimika kuiagiza Mamlaka ya kupamba na Rushwa na kuzuia Uhujumu Uchumi Zanzibar {Zaeca} kufanya uchunguzi. 

Amewatahadharisha Walimu Wakuu wa Maskuli ya Sekondari kusimamia majukumu yao katika kuona kiwango cha Ufaulu kinaongezeka mara dufu kuanzia sasa vyenginevyo Wizara ya Elimu italazimika kumuwajibisha Mwalimu Mkuu husika. 

Uongozi wa Serikali Mkoa wa Kaskazini Unguja unapaswa kuweka mkakati maalum katika kuhakikisha Wilaya zilizomo ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja zinaondoa au kupunguza kabisa Zero zinazotokea katika Skuli mbali mbali za Mkoa huo. 

Akitoa Taarifa za Kitaalamu kuhusiana na Ujenzi wa Jengo la Skuli ya Sekondari ya Donge, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Zanzibar Mhandisi Dr. Idriss Muslim Hijja alisema Jamii ya Kijiji hicho ilifikia hatua ya kuanzisha Mradi huo ili kukidhi mahitaji halisi. 

Dr. Muslim amesema ujenzi rasmi wa Jengo hilo la Ghorofa Mbili ulianza mnamo Mwaka 1992 kwa kutumia nguvu za Wananchi wenyewe licha ya ujenzi wake kusua sua kwa kipindi kirefu kilichopelekea Mradi huo kuachiwa Serikali Kuu kwa hatua zinazoendelea. 

Amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ilitafuta wafadhili na wahisani kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo uliomalizika rasmi Mwishoni mwa Mwaka 2020. 

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Elimu amesema kwamba Mradi wa Ujenzi huo wa Skuli ya Sekondari ya Donge uliogharimu Jumla ya Shilingi Bilioni 1.3 utakidhi mahitaji halisi kwa vile msongamano wa Wanafunzi wa Sekondari na Msingi kwa sasa umeondoka kwa vile watakuwa wakipata elimu kwa kutumia mkondo Mmoja tu wa Asubuhi. 

Kwa upande wao Mwakilishi wa Jimbo la Donge Dr. Khalid Salum Mohamed na Mbunge wa Jimbo hilo Mheshimiwa Soud walisema ndani ya Miaka Mitano ijayo watahakikisha Skuli ya Sekondari ya Donge inaanza kutoa Wanafunzi wa Kidato cha Tano na kuendelea na cha Sita. 

Walisema mpango huo unawezekana kabisa kwa vile wamekusudia na kinachohitajika zaidi ni nguvu za pamoja kati ya Uongozi, Wazazi, Wananchi pamoja na Kamati ya Skuli. 

Viongozi hao wa Jimbo la Donge wameikumbusha Serikali kufikiria Utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Zanzibar katika ujenzi wa Bara bara ya Donge hadi Chaani kwa kiwango cha Lami wazo ambalo tayari Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alithibitisha kwamba halina mjadala wakati ni ahadi ya Serikali. 

Dr. Khalid na Mheshimiwa Soud waliomba katika kuimarisha Elimu ya Sekondani Serikali iangalie pia uwezekano wa Kujenga Dakhalia pamoja na Ukumbi wa Mikutano kwenye Skuli hiyo ili kukidhi mahitaji halisi ya Wataalamu wa Skuli hiyo. 

Akitoa salamu za Mkoa wa Kaskazini Unguja. Mkuu wa Mkoa huo Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud alisema Mkoa huo utaendelea kusimamia Elimu ili kuongeza matokeo ya ufaulu wa Wanancfunzi katika Mitihani yao ya Kitaifa na hatimae kubakia kuwa Historia kwa mikakati itakayowekwa ya kuondosha changamoto ya matokeo mabaya. 

Mh. Ayoub alisema Serikali ya Mkoa imethibitisha kuendelea kuliona Jengo hilo la Skuli ya Sekondari ya Donge linatunzwa kutokana na Historia yake iliyotokana na Wananchi wa eneo hilo kubeba dhima ya kuwajengea mazingira bora ya Elimu Watoto wao. 

Alisema Jengo hilo lina Historia Maalum likiingia katika Tunu ya Mapinduzi kutokana na kujengwa katika misingi ya nguvu za Wananchi wenyewe waliokuwa chini ya Waasisi wa Afro Shirazy Party wa eneo hilo. 

Akimkaribisha Mgeni rasmi kuzungumz na Wananchi hao wa Kijiji cha Donge na Vitongoji vyake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mheshimiwa Simai Mohamed Said alisema Wizara hiyo inakusudia kufanya mapitio ya Mitaala ya Elimu kwa lengo la kuwajengea mazingira bora zaidi ya Taaluma Wanafunzi wake. 

Mh. Simai alisema hatua hii ndio itakayosaidia ufaulu mkubwa wa Wanafunzi jambo ambalo Serikali Kuu kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali katika kuimarisha Sekta hiyo imekusudia kujenga Majengo mengine Matatu ya Sekondari katika maeneo ya Gamba na Mfenesini kwa Unguja na Micheweni kwa Pemba. 

Skuli ya Sekondari ya Donge inakusudia kuchukuwa wanafunzi 800 wakati ile ya msingi iliyopo jirani ina wanafunzi wasiopungua 1,000.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news