Al Ahly washusha kikosi cha mashambulizi dhidi ya Simba SC

Ujumbe wa klabu ya Al Ahly umewasili katika Jiji la Biashara la Dar es Salaam, Tanzania baada ya kukaa angani kwa saa tano na nusu kupitia ndege binafsi, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Kikosi hicho na ujumbe wake unaongozwa na Mjumbe wa Bodi ya klabu hiyo, Mohamed El Damaty ambao uliondoka jijini Cairo Ijumaa saa 5:30jioni (majira ya Cairo) umewasini nchini.  Wamekuja ili kusaka alama tatu muhimu katika mtanange wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ingawa Simba SC nao wameandaa mbinu mpya za kuwazima.
Awali Afisa Habari wa Klabu ya Simba, Haji Manara amesema, wameiandalia Al Ahly zawadi nono ambayo itatolewa kama dozi siku hiyo.

Amesema, dozi hiyo inakwenda kunogeshwa na kauli mbiu ya Total War ambayo ni mahususi kwa ajili ya kujikuasnyia alama tatu Februari 23, 2021.

“Mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati yetu Simba na Al Ahly kutoka nchini Misri itapigwa saa 10:00 jioni siku ya Jumanne Februari 23, 2021. Ni mechi kubwa sana kwa Simba, Tanzania na Afrika Mashariki,"amesema Manara.

Manara ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Februari 19, 2021 jijini Dar es Salaam huku akisisitiza kuwa, kauli mbiu hiyo itumike ili kuwapa nguvu Wanasimba wote kuelekea mchezo huo ili kuchukua alama zao tatu.
Afisa Habari huyo amesema, ili kuipa nguvu zaidi kauli mbiu hiyo wameiongezea maneo ya kutorudi nyuma (point of no return) hivyo watasindikizwa na TOTAL WAR, POINT OF NO RETURN.

“Ndugu zangu, hii ni sawa na mtu kuwa porini halafu akutane na chui, lazima apambane bila kukata tamaa vinginevyo atauliwa, hiyo ndio maana halisi ya kauli mbiu yetu hiyo ambayo itawafanya wachezaji waingie uwanjani wakiamini kuwa hakuna nafasi nyingine zaidi ya kushinda,”amesema.

“Mabingwa wa Afrika ambao wametoka kushiriki ubingwa wa dunia wamefanikiwa kushika nafasi ya tatu watakuwa nchini kuwakabili mabingwa mara nyingi zaidi wa Afrika Mashariki. Rekodi hizo zitaufanya mchezo kuwa wa kipekee.Mara ya mwisho tulikutana hapa Dar tukawafunga goli 1-0 kwenye mechi tuliyosema YES WE CAN na tukaweza. Al Ahly mara zote tukicheza Tanzania tunawafunga.
“Tunao uwezo wa kuwafunga tena, tunao uwezo wa kushinda mechi hiyo. Dhamira hiyo ipo kwa kila Mwanasimba kuanzia wachezaji, benchi la ufundi, viongozi, wanachama na mashabiki wote. Al Ahly sio timu nyepesi. Tunaposema tunaweza kuwafunga tunajua ukubwa wao, lakini Simba hupenda mechi kubwa kama hizi.Tumejiandaa kiakili na tunakwenda kwenye mchezo huu hakuna jambo lingine ila ushindi ili kukaribia lengo letu la nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

"Mechi ya mwisho tuliita WAR IN DAR, mechi ya jasho na damu ndani ya dakika 90 na sasa tunasema TOTAL WAR : POINT OF NO RETURN hii sasa ni vita kamili ya ndani ya uwanja.Malengo yetu ni makubwa, tunataka kuleta heshima kwa Afrika Mashariki. Tunawakilisha zaidi ya watu 150 milioni, wote hao wanategemea timu moja Simba SC. Tunaenda kutetea Simba, Tanzania na Afrika Mashariki yote,"amefafanua Manara.
Red Eagles wanatarajiwa kuchuana na Wekundu wa Msimbazi, Februari 23, mwaka huu katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam.

Miongoni mwa waliopo katika kikosi hicho ni Mohamed El Shennawi, Ali Lotfi, Mustafa Schubert, Hamza Alaa, Ahmed Ramadan Beckham, Yasser Ibrahim, Hamdi Fathi, Mohamed Sharif, Badr Banoun, Afsha, Akram Tawfiq, Junior Ajay na Mahmoud Waheed Rami Rabia, Mahmoud Kahraba, Marwan Mohsen, Ayman Ashraf, Ali na wengine.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news