Bao moja lazibeba Yanga SC, Azam FC katika Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania

Wanajangwani, Yanga SC licha ya kumaliza dakika zote za mchezo wakiwa pungufu katika dimba la Uhuru lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya Ken Gold bado waliweza kulinda ushindi wao wa bao 1-0 walilolipata awali, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Fiston Abdulazack, ingizo jipya ndani ya Yanga ndiye alipachika bao la ushindi dakika ya 40 kwa mkwaju wa penalti uliomshinda kipa wa Ken Gold, Adam John.

Aidha, bao hilo lilidumu hadi kipindi cha pili licha ya nyota wa Ken Gold kupambana kuweza kuweka usawa kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa.

Hata hivyo, jitihada zao zilikwama kwenye mikono ya kipa Faroukh Shikalo ambaye alianza kikosi cha kwanza.

Dakika ya 80 kiungo Carlos Carlinhos, raia wa Angola alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumpiga ngumi mchezaji wa Ken Gold jambo lililopelekea mwamuzi kumuonyesha kadi hiyo.

Inakuwa ni kadi ya kwanza kwa nyota huyo wa Yanga SC mwenye mabao matatu ndani ya Ligi Kuu Bara na aliingia akitoka benchi kuchukua nafasi ya mshambuliaji, Ditram Nchimbi.

Ushindi huo unaifanya Yanga itinge hatua ya 16 bora huku ikisubiri mshindi wa mchezo wa kesho kati ya Sahare All Stars ama Polisi Tanzania kwenye hatua ya 16 bora na timu hizo.

Katika mtanange mwingine, bao pekee la mshambuliaji Mzimbabwe, Prince Dube Mpumelelo limeipa Azam FC ushindi wa 1-0 dhidi ya Mbuni FC katika mchezo wa Hatua ya 32 Bora Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC).

Ni kupitia mtanange uliochezwa katika dimba la Azam Complex lililopo Kata ya Chamanzi Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam. 

Kwa matokeo hayo, wanalambalamba hao sasa watamenyana na Polisi Tanzania iliyoitoa Kwamndolwa FC katika mchezo wa karibuni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news