HOPE FOR GIRLS AND WOMEN TANZANIA WATOA MISAADA YA VYEREHANI KWA WASICHANA WALIOHITIMU MAFUNZO YA USHONAJI NA UJASIRIAMALI MKOANI MARA

Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania (HGWT) linalotoa hifadhi kwa wasichana wanaokimbia ukeketaji, ndoa za utotoni na kupigania haki za binadamu lililopo Mkoa wa Mara, limetoa msaada wa vyerehani tisa kwa wasichana tisa waliohitimu mafunzo ya miaka miwili ya ushonaji na ujasiriamali vyenye thamani ya Shilingi Milioni 2,205,000 baada ya kuhifadhiwa kituo cha Nyumba Salama kinachomilikiwa na shirika hilo kilichopo Kiabakari Wilaya ya Butiama, anaripoti Amos Lufungulo (Diramakini) Mara.
Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Butiama, Neema Joseph akiwa sambamba na Mkurugenzi wa Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwelly wakikabidhi cherehani kwa mmoja wa wasichana wa Nyumba Salama Kiabakari Wilaya ya Butiama baada ya kuhitimu mafunzo ya ushonaji ya miaka miwili waliyoyapata kituoni hapo. Walikimbia ukeketaji mwaka 2017 na kupewa hifadhi. (Picha na Amos Lufungilo/ Diramakini).

Wasichana hao waliendelezwa katika fani ya ushonaji na kufundishwa ujasiriamali na shirika hilo bure baada kupokelewa mwaka 2017 Kituo Cha Nyumba Salama wakikimbia ukeketaji na ndoa za utotoni kutoka katika familia zao.

Ambapo vitendea kazi hivyo, vitawasaidia kujiajiri wanapoondoka kituoni hapo kwenda kujitegemea kimaisha, waweze Kufanya kazi na kujipatia kipato katika kujikwamua kiuchumi na kuondokana na changamoto ya utegemezi, sambamba na kuendana na kauli mbiu ya Rais wa Tanzania,Dkt.John Pombe Magufuli ya 'hapa kazi tu'.

Hafla hiyo imefanyika leo Februari 5, mwaka huu katika Kituo cha Nyumba Salama kilichopo Kiabakari Wilaya ya Butiama ikienda sambamba na maadhimisho ya kupinga Ukeketaji duniani ambayo hufanyika kila mwaka Desemba 6 huku wasichana hao wakitakiwa kuwa mabalozi wa kwenda kutoa elimu juu ya madhara ya ukeketaji katika jamii yao ikiwemo kutokwa damu nyingi wakati wa kukeketwa, hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza, kukatisha masomo yao na kuozeshwa sambamba na kuathirika kisaikolojia.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Wilaya ya Butiama ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika hafla hiyo ya mahafali ya kuwaaga wasichana hao,Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Butiama, Neema Joseph ameiomba jamii kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na ukeketaji, ndoa za utotoni, mila kandamizi na aina zote za ukatili ambazo ni kikwazo kwa ustawi wao na maendeleo ya nchi, huku akipongeza shirika hilo kwa mchango wake katika kutokomeza vitendo hivyo.

"Wilaya ya Butiama inatambua mchango wako Rhobi Samwelly katika kutokomeza ukatili wa kijinsia, tutaendelea kufanya kazi bega kwa bega.Niwaombe pia wasichana mliopata elimu ya ushonaji na ujasiriamali na kupokea vyerehani mlivyopewa bure, kavitumieni kwa manufaa yenu kujikwamua kimaisha na pia kaelimisheni jamii iachane na ukatili ninyi ni mabalozi," amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania (HGWT), Rhobi Samwelly amesema kuwa wasichana hao walipokelewa Kituo cha Nyumba Salama Kiabakari mwaka 2017 wakati kituo hicho kikianza.

Amesema, walijenga mahusiano na wazazi wao wawapokee lakini walikaa na ndipo Shirika hilo likachukua jukumu la kuwaendeleza katika fani za ujasiriamali na ushonaji akawahimiza pia kutumia ujuzi walioupata kufanya kazi kwa uaminifu, ubunifu, na kusimama kidete kupinga ukatili kwa kuelimisha jamii yao.

"Wasichana tunaowapokea tunawapa hifadhi na kuishi nao kwa mujibu wa sheria za nchi. Wasichana hawa ambao wanaondoka wazazi wao tumejenga nao mahusiano na wasichana 7 wanaenda kwao wamekubali kuwapokea na 2 watabaki katika kituo wazazi wao hawapo tayari kuwapokea. 

"Na vitu wanavyovitengeneza shirika litakuwa likivinunua, sisi kama shirika tunatoa cherehani kwa kila binti na tutaendelea kuwafuatilia mara kwa mara kuona maendeleo yao tukishirikiana na Serikali ikiwemo Dawati la Jinsia, na Ustawi wa Jamii," amesema Rhobi.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Kukirango,  Martine Ndunguru amesema, jamii inawajibu wa kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa shirika hilo katika kuunga mkono mapambano dhidi ya ukatili wa jinsia ikiwemo kuwafichua wahusika wanaojihusisha na ukatili wa kijinsia na kuwaripoti katika vyombo vya sheria bila kuwaonea aibu.

Akisoma risala ya wahitimu hao kwa Mgeni rasmi Perepetua Simeon amesema, wasichana hao (9) walikimbia ukeketaji na mmoja (1) ndoa za utotoni walikuwa wenye umri Kati ya Miaka 15 na 17 mwaka 2017 wakiwa hawana Matumaini na maisha yao. 

Ambapo walipewa faraja kupitia Neno la Mungu,kujengwa kisaikolojia, na kupewa malezi na nasaha njema zitakazowasaidia maishani mwao pamoja na elimu ya ushonaji na ujasiriamali.

Selina Yohana ambaye ni miongoni mwa Wahitimu hao pia amesema analishukuru shirika hilo kupitia Mkurugenzi wake, Rhobi Samwelly kwa kuwapokea mwaka 2017 na kuwaendeleza katika fani ya ushonaji na ujasiriamali amesema kwa sasa anauwezo wa kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo batiki, kushona nguo na hivyo ataweza kujisimamia katika maisha yake na kuwaelimisha Wananchi madhara ya Ukatili wa jinsia na namna ya kuepukana na mila zote kandamizi.

Bernadetha Paulo amesema wakati anafika katika Kituo hicho hakujua kusoma na kuandika, lakini Shirika hilo limemuendeleza na kuwa na ujuzi wa kusoma na kuandika pamoja na ufundi hivyo kwa sasa ataweza kusimama kujipambania katika kuhakikisha anakuwa na uwezo wa kujipatia mahitaji yake kupitia ujuzi alioupata. 

Ameomba Serikali na wadau wote kupambana kutoa elimu ya ukatili hasa vijijini ambako vitendo hivyo huwanyima haki wasichana kupata elimu.

Kwa Mujibu wa Rhobi ambaye amewahi kutunukiwa tuzo ya Malkia wa Nguvu kutokana na juhudi zake za kutetea haki za binadamu na kupinga vitendo vya kikatili ikiwemo ndoa za utotoni, ukeketaji, tangu Shirika la Hope lilipoanza mwaka 2017 Mkoa wa Mara ameweza kuokoa wasichana zaidi ya 1,600 waliokuwa katika hatari ya kukeketwa, na kwa msimu wa ukeketaji ulioanza Novemba hadi Desemba 2020 wasichana 290 waliokolewa na kupewa hifadhi Nyumba Salama Mugumu na Serengeti na baada ya msimu kuisha walirejeshwa nyumbani.

No comments

Powered by Blogger.