Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester chataja changamoto uhaba wa wataalam

Mratibu na Mkurugenzi wa Operesheni, Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester, Tina Towo Sokoine amesema kuwa lengo la kiwanda hicho ni kutumia Wataalamu wa ndani lakini uhaba wa Wataalam wa masuala ya sayansi wenye ujuzi hasa wa vitendo unaelekea kukwamisha dhamira yao hiyo,anaripoti Mbaraka Kambona (Pwani).

Towo ameyasema hayo alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa kiwanda hicho kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel alipotembelea kiwanda hicho kilichopo wilayani Kibaha mkoani Pwani Februari 13, 2021.
Mkuu wa Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester, Dkt. Umapati Dasgupta (kulia) akimueleza jambo Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) alipotembelea kukagua kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani Februari 13, 2021.
Mtaalam wa Kuendesha Mitambo katika Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester, Geofrey Mahende (kulia) akitoa maelezo ya namna anavyofanyakazi yake kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) alipotembelea kukagua kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani Februari 13, 2021.

Amesema kuwa, kwa sasa wana wataalamu watatu tu kutoka nje nchi ambao wamewaajiri katika Kiwanda hicho lakini kwa hali ilivyo wanaona watashindwa na labda wanaweza kuomba vibali vingine vya kuajiri wataalamu kutoka nje.

“Nia yetu ni kufanyakazi na Watanzania tu lakini bado vijana wengi tunaowafanyia usahili wanakosa ujuzi hasa wa vitendo, tunaiomba Serikali na Vyuo vinavyoandaa hawa Wataalam kuhakikisha wanajikita katika elimu ya vitendo na sio nadharia peke yake ili kukidhi mahitaji ya sasa na kulinda ajira za Watanzania,”amesema Towo.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wataalam wa Kitanzania wanaofanyakazi katika Kiwanda cha kutengeneza Chanjo cha Hester alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Mkoani Pwani Februari 13, 2021. Wa kwanza kushoto ni Mratibu na Mkurugenzi wa Operesheni, Tina Towo Sokoine.

Kuhusu uzalishaji, Towo amesema kuwa wanatarajia kuzalisha chanjo ya kwanza mwezi wa nne mwaka huu, huku akiiomba Serikali kuona uwezekano wa taasisi zinazohusika na kusimamia uwekezaji kuunganishwa ziwe na lugha ya pamoja ili kumfanya muwekezaji aweze kupata huduma zote sehemu moja bila kuhangaika kama ilivyosasa.

Naye Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel aliutaka Uongozi wa Kiwanda hicho kuhakikisha wanazalisha chanjo zenye ubora ili nchi iweze kuondokana na utegemezi wa chanjo na bidhaa nyingine za mifugo kutoka nchi za nje.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akibadilishana mawazo na Mkuu wa Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester, Dkt. Umapati Dasgupta (kushoto) muda mfupi baada ya kumaliza kutembelea kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani Februari 13, 2021.

“Lengo la Wizara ni kuhakikisha kuwa nchi inaondokana na uagizaji wa chanjo kutoka nje, tunatamani kuwa na chanjo tunazoweza kudhibiti ubora wake na tuwe na uhakika nayo, hivyo uwepo wa kiwanda hiki kutatusaidia kuzalisha chanjo hapa hapa nchini ili kukidhi mahitaji ya Wafugaji wetu na Watanzania kwa ujumla,”amesema Prof. Ole Gabriel

Ameongeza kwa kusema kuwa Serikali inaweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili mahitaji ya wafugaji na wananchi yawe yanashughulikiwa ndani ya nchi.

Aidha, Prof. Ole Gabriel amewaomba wafugaji na Watanzania kuanza kujenga utamaduni wa kuthamini bidhaa za ndani na waondokane na ile dhana ya kwamba bidhaa bora ni ile inayotoka nje, wakithamini vya ndani wataongeza pato la Taifa na kukuza uchumi wa nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news