KMC FC KUONDOKA KESHO NA WACHEZAJI 20 IKIWAFUATA TANZANIA PRISONS

Timu ya Manispaa ya Kinondoni, KMC FC kesho alfajiri itaondoka jijini Dar es Salaam kuelekea Mkoani Rukwa kwa ajili ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa siku ya Ijumaa saa 14.00 mchana katika uwanja wa Nelson Mandela.
Kikosi hicho cha wana Kino Boys kitaondoka kikiwa na wachezaji 20, viongozi watano pamoja na benchi la ufundi na kwamba katika mchezo huo KMC FC itakuwa ni wageni dhidi ya Tanzania Prisons.

Timu ya KMC FC ikiwa ni mara yake ya kwanza kucheza mchezo wa ligi kuu katika uwanja wa Nelson Mandela inakwenda ikiwa imejipanga vizuri ili kuhakikisha kwamba inashinda mchezo huo na hivyo kuondoka na alama tatu muhimu ikiwa ugenini.

Hata hivyo katika kikosi hicho hadi sasa hakuna majeruhi na kwamba kama timu imejiandaa vizuri katika michezo yote ya kipindi hiki cha duru ya lalasalama ikiwa ni pamoja na kufanya vizuri kwa kila mchezo husika.

Itakumbukwa kuwa KMC katika duru ya kwaza ilikutana na Timu ya Tanzania Prisons ikiwa nyumbani katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam na hivyo kuibuka na ushindi wa magoli mawili kwa moja.

Hata hivyo KMC inakwenda Mkoani Rukwa ikiwa imetoka kucheza mechi yake ya kiporo dhidi ya Namungo na hivyo kuweza kuibuka na ushindi wa magoli matatu kwa sifuri na kuiwezesha kufikisha alama 25 huku ikiwa kwenye nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara ikiwa imeshacheza michezo 18 hadi sasa.

Imetolewa na Christina Mwagala

Afisa Habari na Mawasiliano wa Timu ya KMC FC

Post a Comment

0 Comments