Simba SC yaisogelea Yanga SC katika msimamo wa Ligi Kuu, Azam yaichapa Mbeya City

Benard Morrison kwake dakika ya 22 imetosha kuipa Simba SC ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Biashara United katika dimba la Karume lililopo mjini Musoma, Mara, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Raia huyo wa Ghana amefunga bao hilo baada ya shambulizi kali kupitia kwa winga Mzimbabwe, Perfect Chikwende, aliyesaidiana na beki Mkenya, Joash Onyango na kiungo mzawa, Said Ndemla.

Aidha, kutokana na ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi 42 baada ya kucheza mechi 18, sasa wakizidiwa pointi nne na vinara, Yanga SC ambao hata hivyo wamecheza mechi mbili zaidi.
 Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo Februari 18, 2021, JKT Tanzania imelazimishwa sare ya 1-1 na Polisi Tanzania Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
 
JKT walitangulia kwa bao la Daniel Lyanga dakika ya 45, kabla ya Marcel Kaheza kuisawazishia Polisi dakika ya 69, mabao yote yakipatikana kwa mikwaju ya penalti.

Wakati huo huo, Azam FC imeibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Kiungo mzawa Iddi Suleiman (Nado) dakika ya tano ameiadhibu timu yake ya zamani na mshambuliaji Mzimbabwe, Prince Dube Mpumelelo dakika ya 30 amefanya jambo lake huku Mbeya City lilifungwa na beki mzawa, David Mwasa dakika ya 69.

Hata hivyo, kwa ushindi huo, Azam FC inayofundishwa na kocha Mzambia, George Lwandamina inafikisha alama 36 baada ya kucheza mechi 20, ingawa inabaki nafasi ya tatu ikizidiwa alama sita na mabingwa watetezi, Simba ambao wapo nafasi ya pili kwa alama 42.

No comments

Powered by Blogger.