HATUA KWA HATUA MAZIKO YA MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KISIWANI PEMBA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi alitangaza siku saba za maombolezo ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kilichotokea Februari 17, 2021 majira ya saa 5:26 asubuhi, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Akitangaza kutokea kwa msiba huo, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amefariki dunia wakati akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa tokea Februari 9, 2021.
Mwili wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ukishushwa katika Helikopta ya Jesh la Wananchi Tanzania (JWTZ) baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar ukitokea jijini Dar es Salaam.
Rais wa Zanzibar a na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhajj Dkt. Hussein Ali Mwinyi na kushoto ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Hemed Suleimn Andulla na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mhe.Idrisa Kitwana Mustafa na viongozi wengi wa Serikali na chama wakiupokea mwili wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, ulipowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amari Karume Jijini Zanzibar, kwa ajili ya kuangwa na Wananchi wa Zanzibar katika viwanja vya Mnazi mmoja na kusafirika kwenda Pemba kwa maziko leo jioni. (Picha na Ikulu).
Wananchi wa Zanzibar wakiwa katika viwanja vya Mnazi mmoja wakisubiri kusalia mwili wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad,katika viwanja hivyo kabla ya kusafirishwa kwenda Pemba kwa maziko.(Picha na Ikulu).

RAIS WA ZANZIBAR ALHAJJ DK HUSSEIN ALI MWINYI AJUMUIKA NA WANANCHI KATIKA SALA YA KUUSALIA MWILI WA MAREHEMU SEIF SHARIF HAMAD VIWANJA VYA MNAZI MMOJA JIJINI ZANZIBAR
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi na Viongozi wengi wakijumuika na Wananchi wa Zanzibar katika Sala ya kuusalia mwili wa marehemu aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, ilioongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi, iliofanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Zanzibar leo 18-2-2021.(Picha na Ikulu).
Makanali na Mameja wa JWTZ wakiwa wamebeka jeneza la Mwili wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad uliopowasiliu Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar, kwa ajili ya kuagwa na Wananchi wa Zanzibar katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi na Viongozi wa Dini na Serikali wakiitikia dua ikisomwa na Katibu wa Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Abdalla Talib, baada ya kumalizika kwa Sala ya kuusalia mwili wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, iliofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).
Makanali na Mameja wa JWTZ wakiwa wamebeka jeneza la Mwili wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad uliopowasiliu Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar, kwa ajili ya kuagwa na Wananchi wa Zanzibar katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).
RAIS WA ZANZIBAR ALHAJ DKT. HUSSEIN ALI MWINYI AJUMUIKA NA WANANCHI KATIKA MAZIKO YA ALIYEKUWA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS MAALIM SEIF, NYALI MTAMBWE PEMBA LEO FEBRUARI 18, 2021

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo amewaongoza wananchi katika maziko ya Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad yaliyofanyika huko kijijini kwao Mtambwe, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kusini Pemba.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ikisomwa na Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh.Khalid Ali Mfaume.(hayupo pichani) baada ya kumalizika kwa maziko ya aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad na (kushoto kwa Rais) Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi, Rais Mstaaf wa Zanzibar Awamu ya Saba Alhajj Dk. Ali Mohamed Shein na Mlezi wa Chama cha ACT-Wazalendo Mhe. Zitto Kabwe na ( kulia kwa Rais) Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, wakiitikia dua.(Picha na Ikulu).
Viongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo wakiongozwa na Mlezi wa Chama hicho Mhe. Zitto Kabwe wakiweka udongo katika kaburi la aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, wakati wa maziko yake yaliofanyika Kijijini kwao Nyali Mtambwe Wiliya ya Wete Pemba.(Picha na Ikulu).
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiweka udongo katika kaburi la aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika maziko yaliofanyika Kijijini kwao Nyali Mtambwe Wilaya ya Wete Pemba.(Picha na Ikulu).
Rais Mstaafu wa Zanzibar Awamu ya Saba Alhajj Dkt. Ali Mohamed Shein akiweka udongo katika kaburi la aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika maziko yaliofanyika Kijijini kwao Nyali Mtambwe Wilaya ya Wete Pemba.(Picha na Ikulu)

Mapema Alhaj Dkt. Mwinyi aliungana na viongozi pamoja na wanafamilia na wananchi kadhaa katika kuupokea mwili wa Marehemu huko katika uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume, Jijini Zanzibar.

Baada ya hapo, Alhaj Dk. Mwinyi aliungana nao katika sala ya kumuombea Marehemu iliyosaliwa huko katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Jijini Zanzibar.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi, aliwaongoza viongozi, wanafamilia na wananchi kutoka maeneo mbali mbali ya Zanzibar na nje ya Zanzibar katika mazishi hayo yaliyofanyika huko kijijini kwao Nyali Mtambwe, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Pamoja na Rais Dk. Mwinyi viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali walihudhuria wakiwemo Viongozi wastaafu akiwemo Rais Mstaafu wa Zanzibar Awamu ya Saba Dk. Ali Mohamed Shein, Rais Mstaafu wa Zanzibar Awamu ya Sita Dk. Amani Abeid Karume.

Wengine ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Zitto Zubeir Kabwe Mlezi wa Chama cha ACT Wazalendo na viongozi wengineo pamoja na wananchi.

Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad baada ya mwili wake kuwasili kijijini kwao Mtambwe Nyali wananchi walipata fursa ya kipekee kwa kuuwaga mwili wa mpendwa wao kwa kumsalia na baadae kuzikwa katika eneo la makabuni yao ya familia.

Akitoa salamu za Serikali Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla aliwashukuru wananchi wote kwa ushirikiano wao waliouonesha katika kumsitiri makamo wa kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad.
Alisema kuwa Marehemu Maalim Seif, alianza kupata matatizo ya kiafya tarehe 29/1/2021 ambapo alipelekwa na kulazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya matibabu na baada ya hali kutotengamaa alisafirishwa kwenda Hospitali ya Muhimbili katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa matibabu zaidi mnamo tarehe 9 Februari, 2021.

“Tunatoa shukurani kwa madaktari wetu wote wa Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar na Muhimbili Dar es Salaam kwa jitihada kubwa walizochukua katika kutoa matibabu ili kuokoa maisha ya kiongozi wetu huyu,”alisema Makamu wa Pili wa Rais.

Alifahamisha kuwa katika uhai wake Maalim Seif alitowa mchango mkubwa kwa Zanzibar katika maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kwani mbali na kuwa mwanasiasa bali alikuwa mwalimu wa Skuli mbali mbali ambae aliwapatia watu wengi Elimu ambao wametumikia Taifa hili.



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar , Hemed Suleiman Abdalla, alisema Serikali itaendelea kumkumbuka kwani alishiriki katika michakato yote ya maridhiano baina ya vyama vikuu vya siasa ili kuweka mustakbali mwema wa uendeshaji wanachi kwa kuzingatia amani, umoja na mshikamano.

“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa dhati kabisa inapenda kutoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana nasi katika kushughulikia matibabu ya Kiongozi wetu huyu wakati akiwa katika Hospitali ya Muhimbili na baada ya kufariki kuhifadhiwa katika Hospitali ya JWTZ Lugalo Dares Salaam,”amesema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Aidha, alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar , inatowa pole kwa familia ya Marehemu, ndugu, jamaa na marafiki, viongozi, wapenzi na wanachama wa Chama cha ACT Wazalendo, viongozi na wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla kwa kuondokewa na Kiongozi huyo.
Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais,Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Dkt.Khalid Salum Mohammed akisoma wasifu wa Marehemu aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, wakati wa hafla ya maziko yake yaliofanyika Kijijini kwao Nyali Mtambwe Wilaya ya Wete Pemba.(Picha na Ikulu).

Akisoma wasifu wa marehemu maalim Seif Sharif Hamad , Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Sera na Uratibu na Shughuli za Baraza la Wawakilishi Zanzibar Dk. Khalid Salum Mohamed , alisema kuwa Marehemu Maalim Seif alizaliwa tarehe 22 Octoba mwaka 1943 , Mtambwe Nyali na alipata elimu ya Msingi katika Skuli ya Uondwe na Skuli ya Wete Boy’s huko Pemba kati ya mwaka 1950 – 1957.

Alieleza kuwa Maalim Seif alisoma Elimu yake ya Sekondari kuanzia mwaka 1958 hadi 1961 katika Skuli ya King Geoge VI Memorial mjini Zanzibar ambayo kwa sasa ni Skuli ya Sekondari ya Lumumba na aliendelea na masomo ya cheti cha cha sekondari katika skuli hiyo.

Mwaka 1972 -1975 , alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar-es –Salaam kwa masomo ya Shahada ya Kwanza katika fani ya Sayansi ya Siasa, Utawala wa Umma na Ushirikiano wa Kimataifa na kutumikia Digrii ya Heshima (BA honours)mwaka 1975.

Marehemu Maalim Seif Sharif alikuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri wa Elimu kuanzia mwaka 1977 hadi 1980 na kubahatika kuwa mmoja wa Wajumbe waanzilishi wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar mwaka 1980 na kuendelea hadi mwaka 1989 na mwezi Februari, 1984-1988 alikuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar.

Waziri Khalid alimuelezea Marehemu Maalim Seif jinsi alivyoanzisha chama cha CUF na baadae kujiunga na ACT Wazalendo mnamo Machi 2019 sambamba na kuteuliwa kuwa Makamo wa Kwnaza wa Rais aliyoishikilia kaunzia Novemba 9,2010 hadi Machi 2016.

Pia, Marehemu aliteuliwa tena kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais kufuatia kumalizika kwa uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020, na kuteuliwa kushika nafasi hiyo tarehe 7 Disemba nafasi ambayo aliishikilia hadi alipofikwa na mauti jana (tarehe 17 Februari,2021). Marehemu ameacha kizuka na watoto wane(4).

Mlezi wa Chama cha ACT Wazalendo , Zitto Zubeir Kabwe, akitowa salamu za Chama chake alitoa shukurani kwa Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi kwa mashirikiano aliyoyaonesha kwa kiongozi huyo katika kushughulikia afya yake.

Kiongozi mkuu huyo wa ACT Wazalendo, alimuelezea Maalim Seif katika uhai wake alikuwa ni baba wa Demokrasia na mpambanaji wa haki za watu wote ambapo Chama hicho kimepoteza mtu muhimu na mpatanishi ndani ya Chama chao.

Alisema katika hilo alikuwa na kifua kipana cha kuhimili suala la maridhiano wakati wote wa maisha yake na ndio mpaka anafikwa na umati alikuwa ni muumini wa suala la maridhiano ya kisiasa ndani ya nchi yake.

MABALOZI WAMLILIA MAALIM SEIF SHARIF HAMAD

Mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao hapa nchini wamemlilia Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad na kumuelezea kwa mema aliyoyafanya enzi za uhai wake hapa duniani.

Mabalozi hao wamewasili katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti kwa ajili ya kusaini kitabu cha maombolezo ambapo mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo baadhi yao wakaelezea walivyoguswa na msiba wa Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad.

Balozi wa Ufaransa chini Tanzania, Mhe. Frederic Clavier amesema kuwa ni pengo kubwa kwa Zanziba na kwa Tanzania pia kwani Mhe. Maalim Seif alikuwa kiongozi mahiri kwa taifa na aliyekuwa na uhamasisho kwa bara la Afrika.

“Alikuwa mtetezi wa masuala mbalimbali ikiwemo demokrasia na haki, pia katika enzi za uhai wake alikubali kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais kwa Serikali ya Zanzibar ni jambo la kuigwa kwa taifa la Zanzibar na Taifa la Tanzania kwa Ujumla,” Amesema Mhe. Clavier

Mhe. Clavier ameongeza kuwa “Maalimu Seif alikuwa kiongozi aliyependa amani, na aliyekuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya nchi yake……lakini pia alikuwa mpenda amani na alikuwa mwanasiasa makini ……..kwa kweli tutamkumbuka daimia, tunamuombea kwa Mungu apumzike kwa amani,”.

Kwa upande wake Balozi wa Finland hapa nchini Mhe. Riitta Swan amesema kuwa Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa kiongozi makini aliyependa amani na mshikamano wakati wa uhai wake.

“Kwa muda mfupi niliomfahamu kwa kweli alikuwa kiongozi mahiri aliyependa amani na umoja hakika pengo lake halitazibika kwa urahisi, Mungu ampumzishe kwa amani,” Amesema Mhe. Swan

Nae Balozi wa Zimbabwe hapa nchini, Mhe. Luteni Jenerali Mstaafu, Anselem Sanyatwe amesema kuwa Mhe. Maalim Seif alikuwa ni kiongozi mchapakazi na mzalendo kwa taifa la Zanzibar na Tanzania. “Kwa kweli Jamhuri ya MUungano imepoteza kiongozi mzalendo, kwa niaba ya Jamhuri ya Zimbabwe natoa pole kwa Tanzania kwa kuondokewa na Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar…..poleni sana watanzania kwa msiba huu mzito,” Amesema Mhe.

Kwa upande wake Balozi wa Kuwait nchini, Mhe. Balozi Mubarak Mohammed Alsehaijan amesema kuwa Mhe. Maalim Sief kiongozi mpenda amani na atakumbukwa daima kwa mema aliyoyafanya kwa Wazanzibari na watanzania kwa ujumla.

Baadhi ya mabalozi waliofika na kusaini kitabu cha maombolezo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Jijini Dar es Salaam ni pamoja na Balozi wa Zambia nchini mhe. Benson Keith Chali, Balozi wa Finland chini Tanzania, Mhe. Riitta Swan na Balozi wa Kuwait nchini, Mhe. Balozi Mubarak Mohammed Alsehaijan.

Wengine ni Balozi wa Pakistani hapa nchini, Mhe. Mohammad Saleem, Balozi wa Ufaransa hapa chini, Mhe. Frederic Clavier, Balozi wa Zimbabwe hapa nchini, Mhe. Luteni Jenerali Mstaafu, Anselem Sanyatwe pamoja na Mwakilishi wa Balozi wa Irani hapa nchini. Bwn. Mohammad Rezaee.

Balozi wa Ufaransa chini Tanzania, Mhe. Frederic Clavier akisaini kitabu cha maombolezo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad jijini Dar es Salaam.

Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Riitta Swan akisaini kitabu cha maombolezo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad jijini Dar es Salaam

Balozi wa Kuwait hapa nchini, Mhe. Balozi Mubarak Mohammed Alsehaijan akisaini kitabu cha maombolezo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad jijini Dar es Salaam.

Balozi wa Zimbabwe hapa nchini, Mhe. Luteni Jenerali Mstaafu, Anselem Sanyatwe akisaini kitabu cha maombolezo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad jijini Dar es Salaam.

Balozi wa Pakistani hapa nchini, Mhe. Mohammad Saleem akisaini kitabu cha maombolezo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad jijini Dar es Salaam.

Mwakilishi wa Balozi wa Irani hapa nchini. Bwn. Mohammad Rezaee kitabu cha maombolezo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad jijini Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

Previous Post Next Post

International news