Maelfu ya waumini kwa Nabii Joshua waanza maombi ya kuliombea Taifa

Maelfu ya waumini wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania wameanza maombi mfululizo ya kuliombea Taifa ili Mungu aliepushe na nia mbaya za shetani ikiwemo magonjwa mbalimbali yanayoenda sambamba na hofu miongoni mwa jamii.
Aidha, maombi hayo yanaendelea usiku na mchana ambapo Machi 6 na 7, mwaka huu wa 2021 yatafanyika maombi ya Kitaifa kwa ajili ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli katika makao makuu ya huduma hiyo yaliyopo Yespa, Kihonda mjini Morogoro.

Kwa nyakati tofauti waumini hao kutoka mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Morogoro, Songwe, Mbeya, Manyara, Kilimanjaro, Arusha, Iringa, Jiji la Zanzibar na nje ya nchi wameeleza kuwa, wameamua kufanya hivyo ikiwa ni kuitikia wito wa Roho Mtakatifu wa kuliombea Taifa la Tanzania bila kuchoka kwa kuwa, rehema na neema za Mungu zinakwenda kuonekana.

Awali Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Joshua Aram Mwantyala alitangaza siku mbili maalum za maombi kwa ajili ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli ili Mungu amuwezeshe kukamilisha miradi mbalimbali ya kimkakati anayoianza na inayoendelea kutekelezwa kwa sasa.

Miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt.John Magufuli ni pamoja na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambapo kwa kipande cha kwanza kati ya Dar es Salaam hadi Morogoro kipo katika hatua za mwisho ili kukamilika.

Pia mradi mwingine ni ujenzi wa mradi wa bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere (JNHPP-MW2115) hii ikiwa ni kati ya miradi ya kihistoria ambayo kukamilika kwake kunatarajiwa kwenda kuifanya Tanzania kuwa na nishati ya kutosha kwa matumizi ya ndani na kuuza nje.
Nabii Joshua ameyasema hayo leo Februari 14, 2021 katika Huduma ya Sauti ya Uponyaji iliyopo Yespa, Kihonda mjini Morogoro wakati akizungumzia kuhusiana na maandalizi ya kongamano ambalo litaenda sambamba na maombi hayo.

Amesema,kongamano hilo litafanyika Machi 6 na 7, 2021 mjini Morogoro na linatarajiwa kuhudhuriwa na watu zaidi ya 5,000.

"Hili ni kongamano maalumu la ibada kumuomba Mungu amuwezeshe Rais Dkt.Magufuli aweze kutekeleza kikamilifu miradi aliyoianza ya kimkakati. Pia ni maombi yangu kwa Mungu, kama itampendeza amuongezee muda wa miaka saba ili kukamilisha miradi na kutengeneza Katiba mpya kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya kudhibiti wizi wa raslimali za nchi na mali za umma,"ameeleza.

Nabii Joshua amesema, Rais Dkt.Magufuli amekuwa mfano wa kuigwa katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa ikiwemo kukomesha vitendo vya ujangili ambavyo vilikuwa gumzo huko nyuma.

"Kutokana na hatua hizi, wale wote waliokuwa wanatenda hao matendo watakuwa wamejenga uadui mkubwa, hivyo ili Rais Dkt.Magufuli aweze kusonga mbele, yatupasa kumkabidhi mbele za Mungu, nasi tunakwenda kufanya hivyo na hakika Mungu wetu wa Mbinguni atakwenda kuachilia ulizi wa kipekee juu yake,"alisema Nabii Joshua.

Pia alisema mbali na hayo, Rais Magufuli ameendelea kuteleza miradi ya vituo vya kisasa vya mabasi kikiwemo cha Kimataifa kule Mbezi Luis, ununuzi wa ndege, viwanja vya kisasa vya ndege.

Mingine ni ujenzi wa barabara za kisasa mijini na vijijini, vituo vya afya, hospitali za kisasa, shule, miradi ya maji, elimu bure, ujenzi wa masoko ya madini, utoaji wa hati za kusafiria za kisasa, na vingine vingi.

Post a Comment

0 Comments