Majaliwa asema Serikali itakamilisha utekelezaji vipaumbele vyote 2022/21

Serikali imejipanga vizuri katika kuhakikisha inakamilisha utekelezaji wa vipaumbele vyote ambavyo havikukamilika katika kipindi kilichopita sambamba na kusimamia ipasavyo maeneo mapya yaliyoibuliwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameyasema hayo leo Februari 2, 2021 bungeni jijini Dodoma alipowasilisha hoja kwa ajili ya wabunge kuanza kujadili hotuba ya Rais Dkt.John Magufuli aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa Bunge la 12 tarehe 13 Novemba 2020.

Waziri Mkuu amesema, Serikali itaendelea kutekeleza na kusimamia masuala muhimu yaliyoelezwa kwenye hotuba ya Rais Dkt. Magufuli ya kuzindua bunge la 11 tarehe 20 Novemba 2015 na amewasisitiza wabunge kutumia vema fursa hiyo adhimu.

“Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, sambamba na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020–2025, Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa ahadi na maelekezo ya Mheshimiwa Rais wetu mpendwa aliyoyatoa wakati akizindua Bunge la 12 sambamba na Bunge la 11,”amesema.

Amesema, Rais Dkt.Magufuli wakati akieleza vipaumbele mbalimbali vinavyotarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo aliweka bayana kuwa mambo yote muhimu yatakayotekelezwa yamebebwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 - 2025.

“Baada ya hotuba ya Mheshimiwa Rais kutolewa utekelezaji wa maelekezo yake ulianza mara moja kwenye maeneo mbalimbali. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wizara na taasisi zote za Serikali ziliainisha maeneo ya utekelezaji sambamba na kuja na mipango ya utekelezaji wa muda mfupi, muda wakati na muda mrefu,”amesema.

“Mheshimiwa Spika, ni ndoto ya Mheshimiwa Rais wetu mpendwa kuona Tanzania inajenga uchumi imara, shindani sambamba na kutengeneza ajira za kutosha kwa Watanzania. Hivyo basi, nitoe rai kwa waheshimiwa wabunge wenzangu kutumia vema fursa hii adhimu,”amesema.

Amesema licha ya kuanza kwa utekelezaji wa masuala mbalimbali yaliyomo kwenye hotuba hiyo, bado michango ya wabunge ni muhimu katika kuisaidia Serikali kutekeleza kikamilifu vipaumbele vilivyoainishwa pamoja na kushughulikia kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news