Makachero wamnasa Mwalimu Mkuu kwa udanganyifu wa mitihani, afikishwa mahakamani

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wamemfikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Kiteto, Mwalimu Oscar Waluye baada ya mamlaka yake ya nidhamu kumfukuza kazi, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Alli Sadiki Hajji amesema, Waluye alikuwa Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Olkitikiti iliyopo katika Kijiji cha Engong'ongare wilayani Kiteto.

Amesema, Mwalimu huyo ameshitakiwa kwa kufanya udanganyifu katika mitihani ya Darasa la Saba iliyofanyika Oktoba, 2020 kitendo ambacho ni kinyume cha Kifungu cha 23 na 24 (1) Sheria ya Baraza la Mitihani Tanzania (CAP.107 R:E 2019).

Kesi hiyo ya jinai namba CC.32/2021 imefikishwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi, Wilfred John na ipo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Joakimu Mwakyolo.

Mshitakiwa amekana makosa yake na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana hivyo kupelekwa rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Februaru 16,2021.

Uchunguzi wa TAKUKURU Wilaya ya Kiteto unaonyesha kwamba, Waluye aliwalazimisha wanafunzi wa darasa la sita wawili katika shule hiyo kufanya mitihani ya darasa la saba, badala ya watahiniwa ambao uwezo wao darasani unaelezwa kuwa ni kiwango cha chini.

Pia Waluye anadaiwa alimkaririsha mwanafunzi mmoja aliyehitimu shuleni hapo mwaka 2019.

Wanafunzi hao wawili wa darasa la sita na mwanafunzi aliyehitimu mwaka 2019 walikamatwa na makachero wa TAKUKURU tayari wakiwa wamefanya mitihani ya masomo ya Kiswahili na Hisabati kwa niaba ya wenzao hao wa darasa la saba wanaodaiwa kuwa na uwezo mdogo huku aliyekaririshwa akitumia jina la mwanafunzi mtoro.

Katika mahojiano na maafisa wa TAKUKURU Wilaya ya Kiteto, Waluye alikiri kutenda makosa hayo kwa maelezo kwamba alitaka shule yake ionekane inafaulisha vizuri.

Aidha, kwa mujibu wa TAKUKURU, kitendo hicho ni kinyume cha maadili kwa kuwa kinawajengea watoto ambao ni Taifa la kesho tabia za ukiukaji wa maadili na wakati wote kuwa tegemezi.

"Rai yetu kwa wazazi, walezi na walimu, tuwalee watoto katika njia iwapasayo nao hawataiacha hata watakapokuwa wazee (Biblia Mithali 22:6)," amefafanua Kaimu Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara.

Pia ametumia nafasi hiyo kuwaeleza watumishi wa umma mkoani Manyara kwamba, kuanzia sasa, "wale tunaojiridhisha kuwa wametenda makosa ya jinai na rushwa. tutakuwa tunawafikisha kwanza kwenye mamlaka zao za nidhamu na kuwashtaki kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi zinazotawala kada zao ili waondolewe kwenye utumishi wa umma na wasiendelee kupokea mishahara bila kuifanyia kazi.

"Baada ya kuondolewa kwenye utumishi, mashtaka ya jinai yatafuata kama ilivyofanyika kwa Mwalimu Oscar Waluye kwa kuwa jinai haina ukomo wa muda,"ameeleza Kaimu Mkuu huyo, Alli Sadiki Hajji.

No comments

Powered by Blogger.