Man United vs Newcastle United bao 3-1 EPL, Inter Milan VS AC Milan 3-0 SERIE A

Marcus Rashford ameibuka kuwa mchezaji muhimu kwenye ushindi wa Manchester United dhidi ya Newcastle United katika mtanange wa Ligi Kuu nchini England uliopigwa Februari 21, 2021 huku United wakishinda 3-1, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa England aliitanguliza United ambao walikuwa wenyeji wa mchezo kwa shuti kali kunako dakika ya 30 ya mchezo kabla ya Allan Saint-Maximin kusawazisha baada ya makosa ya Harry Maguire.

Newcastle walianza kupoteza mechi baada ya Daniel James kufunga goli la uongozi kwa Manchester United akimalizia pasi ya kiungo mshambuliaji wa Ureno Bruno Fernandes kabla ya yeye mwenyewe (Bruno) kufunga goli kwa njia ya penati kufuatia Marcus Rashford kuangushwa eneo la hatari.

Kipigo hicho kwa kocha Steve Bruce kinaifanya timu hiyo kushika nafasi ya 17 alama tatu zaidi ya timu nafasi ya chini yake kuelekea kushuka daraja.

Unakuwa ni ushindi wa pili kwa kocha Ole Gunnar Solskjaer ambaye awali alishindwa kupata matokeo chanya katika mechi sita.

SERIE A

Inter Milan imeibuka na ushindi wa goli 3-0 dhidi ya wapinzani wao wa karibu AC Milan katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Italia uliopigwa Februari 21, 2021 na kukwea mpaka nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Serie A.

Magoli mawili ya Lautaro Martinez yaliwapa auheni Inter mbele ya AC Milan ambao wameongoza msimamo wa Ligi kwa muda mrefu huku wakiwa kwenye kiwango bora.

Staa Zlatan Ibrahimovic alikuwa aipatie timu yake magoli mawili lakini haikutokea hivyo kabla ya Romelu Lukaku kufunga goli la tatu na kumaliza kabisa mchezo, goli la Lukaku linamfanya kuwa mshambuliaji wa kwanza kufunga goli katika mechi nne mfululizo za Dabi ya Milan tangia Benito Lorenzi alipofanya hivyo mwaka 1950.

Post a Comment

0 Comments