Matukio ya mashambulizi kwa raia yazua maswali huko Ituri, Beni

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) imeeleza kusikitishwa na ongezeko kubwa la matukio ya mashambulizi ya raia kwenye maeneo ya Irumu na Mambasa jimboni Ituri.

Sambamba na eneo la Beni katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet amesema, mashambulizi hayo yanafanywa  na kikundi cha waasi cha Allied Democratic Forces (ADF) sambamba na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyotekelezwa na vikosi vya ulinzi na usalama vya DRC.

Kupitia msemaji wake Marta Hutardo, Kamishna huyo alimnukuu ripoti za Ofisi ya pamoja ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa na DRC, UNJHRO ikisema, “raia 849 waliuawa katika maeneo hayo kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na ADF.

"Kati yao hao, 381 walikuwa ni wanawake waliouawa kati ya Januari na Juni 2020, na wengine 468 waliuawa kati ya mwezi Julai na Desemba mwaka huo wa 2020. Katika nusu ya pili ya mwaka huo, raia 62 walijeruhiwa na wanawake wanne walibakwa na waasi wa ADF,”amesema.

Aidha, ukiukwaji wa haki za binadamu na sheria za kibinadamu za kimataifa ni vitendo pia vilivyotajwa kufanyika kwenye maeneo hayo na vikosi vya ulinzi na usalama wakati wa operesheni zao dhidi ya ADF.

Kwa mujibu wa ripoti kuanzia Januari hadi Juni 2020, raia 22 waliuawa, wanawake 9 na watoto 12 walibakwa wakati watu 81 walikamatwa kiholela na vikosi hivyo vya ulinzi na usalama vya DRC.
 
Nusu ya pili ya mwaka wa 2020, kwa mujibu wa ripoti hiyo, ilisheheni matukio ya mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka kwa ADF dhidi ya raia kwenye maeneo ambayo awali yalikuwa himaya ya waasi hao.

“Mashambulizi hayo yalisababisha raia wengi kukimbia makazi yao halikadhalika kukamatwa kwa raia wengi zaidi na kutumikishwa kwenye ajira. Katika kipindi hicho, raia 534 walitekwa nyara na hadi sasa 457 kati yao hawajulikani waliko,”amesema Hurtado alipozungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi wakati akiwasilisha ripoti hiyo kwa niaba ya Bachelet.

Ripoti hiyo inaonesha kuendelea kwa ghasia hata mwaka huu wa 2021 ambapo tarehe 13 mwezi uliopita wa Januari katika eneo la Walese Vonkutu huko Irumu jimboni Ituri, kundi la watu wasiojulikana walishambulia watu wa kabila la Watwa na kuua watu 14, wakiwemo wanawake wawili wajawazito.
 
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kiwango, mfumo na aina ya mashambulizi na yanayofanywa dhidi ya raia, vinaweza kuwa uhalifu dhidi ya binadamu.

Ghasia hizo zinafanyika huku watekelezaji wakiendelea kukwepa sheria na ni matukio machache sana yanachunguzwa au wahusika kufikishwa mbele ya sheria.

Oktoba, mwaka jana, waasi wa ADF walivamia gereza la Beni ambako wafungwa 1,300 walitoroka na hivyo kurejesha nyuma mpango wa serikali wa kuwajibisha wavunjifu wa sheria.

Ripoti ina mapendekezo kadhaa kwa serikali ya DRC ikiwemo kuhakikisha vikosi vya ulinzi na usalama vinazingatia maadili na viwango vya sheria za kimataifa za haki za binadamu na kibinadamu.

Pia inataka mamlaka za DRC kuimarisha mfumo wa ulinzi wa raia hususan wakati wa operesheni zake za kijeshi.

Pamoja na hiyo, ripoti inataka haki kwa manusura wa vitendo hivyo na msaada wa kibinadamu ikiwemo wale waliofurushwa kutokana na ghasia.

No comments

Powered by Blogger.