MOI kwa kushirikiana na KCMC zaanza kutoa huduma za kupasua ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu

Taasisi ya Mifupa MOI kwa kushirikiana na Hospitali ya rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) Februari 5, 2021 zimeanzisha ushirikiano wa kutoa huduma za kibingwa za upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu kwa wakazi wa Kanda ya Kaskazini ili kuwaondolea adha ya kusafiri umbali mrefu kuafuata huduma hizo Dar es Salaam au kwenda nje ya nchi, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Madaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu wa MOI wakishirikiana na madaktari bingwa wa KCMC kufanya upasuaji wa uti wa mgongo katika hospitali ya KCMC, huduma hiyo imaenza ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kusogeza huduma karibu kwa wananchi.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda KCMC, Dkt. Sarah Urasa amesema ushirikiano baina ya MOI na KCMC utaleta tija kubwa sio kwa wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro pekee bali kwa mikoa yote ya kanda ya kaskazini na nchi jirani ya Kenya ambao wamekuwa wakifika KCMC kupata huduma.

“Kwanza niwashukuru ndugu zetu kutoka MOI ambao wamefika hapa ili tushirikiane kuanzisha huduma hizi za kibingwa za upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, tumekuwa tukitoa huduma hizi na sio kwa kiwango kikubwa hivyo kwa kushirikiana na MOI tutakuwa tunatoa huduma hizi kwa kiwango kikubwa,"amesema Dkt.
Sarah

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Respicious Boniface amasema kuanzishwa kwa huduma za kibingwa za upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu katika hospitali ya KCMC ni azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kusogeza huduma za kibingwa kwa wananchi na kuwapunguzia adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma Dar es Salaam.

“Tumekuja hapa kwa ajili ya kuanzisha ushirikiano na wenzetu hawa wa KCMC katika eneo la upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu ili wagonjwa wenye magonjwa hayo wapate huduma hizo hapa pasipo ulazima kuja MOI, wataalamu wetu wamekuja kufanya tathmini ili tuwashauri namna bora ya kutoa huduma na pia kuwajengea uwezo wataalam wa hapa,"amesema Dkt. Boniface

Ushirikiano baina ya MOI na KCMC unatekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya awamu ya Tano ya kusokeza huduma za kibingwa kwa wananchi ili kuwapunguzia usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo Dar es Salaam au nje ya nchi.

Tangu uhusiano huu wa tiba kati ya KCMC na MOI uanze tayari wagon jwa watatu wamepata huduma hii ya upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu ambapo wangeenda nje ya nchi serikali ya Tanzania ingelipa jumla ya sh. milioni 135 wakati hapa KCMC matibabu yao yamegharimu jumla ya kiasi cha shilingi sh.milioni 13.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news