NAIBU WAZIRI MABULA ATAKA NHC KUKAMILISHA HARAKA KITEGA UCHUMI MUTUKULA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kukamilisha haraka mradi wake wa jengo lake la Kitega uchumi lililopo Mutukula wilaya ya Misenyi mkoa wa Kagera,anaripoti Munir Shemweta (WANMM) Misenyi.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Jengo la Kitega uchumi cha Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) uliopo Mutukula wilaya ya Misenyi mkoa wa Kagera tarehe 17 Februari 2021. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Misenyi Kanali Denice Mwila na kushoto ni Meneja Uhusiano na Huduma za Jamii Bw. Muungano Saguya.

Akiwa katika ziara yake ya siku moja katika mkoa wa Kagera kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na miradi inayojengwa na NHC, Dkt Mabula alisema kukamilika mapema kwa jengo la kitega uchumi katika eneo la Mutukula siyo tu litaliwezesha shirika kupata fedha lakini litakuwa kichocheo cha wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda.

"Mradi huu uko kistrategic ukikamilika tutapata wawekezaji na kasi ya wafanyabiashara kukimbilia upande wa pili itapungua hivyo nataka jengo hili liishe kufikia machi mwaka huu,"amesema Dkt Mabula.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ujenzi wa mradi wa kitega uchumi cha Mutukula umechukua muda mrefu na kusisitiza kuwa, kutokana na maendeleo mazuri ya ujenzi ni matumaini yake ujenzi wa mradi huo sasa utakamilika kwa wakati .

Amesema, mradi huo wa kitega uchumi cha Mutukula ni kama njia ya Shirika la Nyumba la Taifa kujenga majengo maengine ya biashara katika maeneo mengine na kuongeza kuwa miradi kama hiyo italisaidia sana Shirika kimapato.

Sehemu ya jengo la Kitenga uchumi cha Shirika la Nyumba la Taifa lililopo Mutukula wilaya ya Misenyi mkoa wa Kagera.

Kwa upande wake Meneja Huduma kwa Jamii wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Muungano Saguya amesema, shirika lake lina mkakati wa kujenga majengo ya kibiashara katika maeneo ya mipakani ili kuimarisha biashara katika maeneo hayo.

Ameongeza kuwa, pamoja na NHC kuendelea na ujenzi wa mradi wake katika eneo la Mutukula Shirika hilo liko katika mkakati wa kujenga vitega uchumi vingime katika meneo yote ya mipaka ya Tanzania na nchi zingine na kipaumbele kikiwa ni mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Sirari na Tanzania na Zambia, Tunduma.
Sehemu ya jengo la Kitenga uchumi cha Shirika la Nyumba la Taifa lililopo Mutukula wilaya ya Misenyi mkoa wa Kagera.

Msimamizi wa mradi wa Kitega Uchumi cha Mutukula mkoani Kagera Mhandisi George Shanali alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa mradi wa jengo hilo unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika Machi 15, 2021.

Amesema, mradi huo unaogharimu takriban bilioni 2.9 utajumuisha huduma za kibenki na maduka 36 ya biashara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news