Rais Dkt.Mwinyi: Endeleeni kuniombea na tufanye kazi kwa bidii kwa kudumisha umoja na mshikamano

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi wa Zanzibar kuimarisha amani na umoja walionao ili kuiletea nchi yao maendeleo.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj, Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiondoka katika viwanja vya Msikiti Mkuu wa Ijumaa Bweleo baada ya kumaliza Sala ya Ijumaa iliofanyika katika msikiti huo leo na baadaye kwenda nyumbani kwa Rais Mstaafu Dkt. Ali Mohammed Shein kumsalimia. (Picha na Ikulu/Diramakini).

Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo huko katika Msikiti wa Ijumaa Bweleo, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi wakati akitoa salamu kwa Waislamu mara baada ya kukamilisha sala ya Ijumaa.

Katika salamu zake hizo, Alhaj Dkt. Mwinyi amesema wananchi wote wa Zanzibar wana kila sababu kuungana pamoja katika kuendeleza amani na umoja uliopo kwani bila ya kuwepo mambo hayo ya msingi maendeleo hayawezi kupatikana.

Amesema kuwa, kukosekana kwa amani hupelekea kutokufanyika mambo muhimu katika maisha ya wananchi ikiwemo kushindwa kutekeleza ibada hivyo, Alhaj Dkt. Mwinyi ameeleza kwamba kila mmoja ana wajibu wa kuendeleza na kuimarisha amani iliyopo.

Ameeleza kuwa, wananchi wana matumaini makubwa ya kupiga hatua za uchumi hapa nchini sambamba na kubadilika kwa maisha yao kwa sababu ya kuwepo kwa amani, hivyo, ni jukumu la kila mtu kuidumisha na kuihubiri amani na umoja uliopo.

Alhaj Dkt. Mwinyi amesema kuwa, upo umuhimu mkubwa wa kuimarisha umoja, kwani ni muhimu katika kujiletea maendeleo kwani kuwepo kwa mifarakano hakuna tija na wala hakutaleta maendeleo.

Ameeleza jukumu la wananchi la kuidumisha na kuihubiri amani na kusisitiza kwamba umoja ni jambo la msingi na ndio maana kwa upande wao viongozi wa siasa wameweza kuhubiri amani na umoja kwa vitendo kwa kuungana na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kuweza kuwaunganisha watu.

Hivyo, amewataka wananchi kuweka tofauti zao za kisiasa na kiitikadi pembeni na badala yake wawe kitu kimoja katika kuendeleza amani, umoja na mshikamano.

Alhaj Dk. Mwinyi ameeleza kwamba kwa upande wake ana jukumu kubwa la kuwahudumia wananchi pamoja na kutekeleza ahadi alizoziahidi wakati wa kampeni sambamba na kuhakikisha kwamba nchi inapata maendeleo ya haraka na maisha ya wananchi yanaimarika.

Kwa kutekeleza hayo, Alhaj Dkt. Mwinyi amesema kwamba, kuna hitaji msaada wa wamawazo, dua sambamba na watu kuwajibika katika kufanya kazi.

Kutokana na hayo, Rais Dkt. Mwinyi amewataka waumini hao kumuombea dua ili atimize majukumu yake na atende haki kwa kila mmoja kutokana na dhima aliyonayo mbele ya MwenyeziMungu na wananchi ya kutenda haki.

“Ombi langu kwenu ni kuendelea kuniombea”,amesisitiza Alhaj Dkt. Mwinyi.

Alhaj Dkt. Mwinyi amesisitiza kwamba amegombea nafasi hiyo kwa nia moja ya kuwatumikia wananchi wa Zanzibar ambapo kitu kilicho mbele yake hivi sasa ni utekelezaji.

Ameeleza kwamba katika utekekezaji kuna mamabo yatawakusa watu ambapo pale atakaposema watu wawajibike na kwamba hawatowajibika basi watawajibishwa hivyo, na hatua zinazochukuliwa ni kujenga na wala sio visasi.

Ameongeza kwamba watu wote wakiwajibika hasa watumishi wa umma katika maeneo yao maendeleo ya haraka yatapatikana.

Sambamba na hayo, Alhaj Dkt. Mwinyi ameeleza kwamba kuna mapambano dhidi ya rushwa, ubadhirifu, wizi, uzembe ambapo hayo yakiwachwa kuendelea hakuna maendeleo yatakayopatikana kwani wapo ambao wanabomoa wakati serikali inajenga.

Hivyo, amesisitiza kwamba kuna haja ya kupigwa vita vitendo hivyo kwa nguvu zote hasa kwa kutambua kwamba kupambana na vitendo hivyo kutagusa watu ambao ndani yake wamo jamaa, ndugu lakini lengo ni kutafuta maendeleo ya haraka na wala si kumkomoa mtu.

Mapema akisoma hotuba ya sala ya Ijumaa, Khatibu wa msikiti huo Sheikh Mussa Ali Kirobo ameeleza haja kwa waumini kushikamana na maamrisho ya Allah na wala wasifarakiane na kuwataka kuwa kitu kimoja.

Ameongeza kwamba, katika dini ya Kiislamu watu wote ni sawa na hakuna aliyebora hata mmoja na badala yake mbora ni yule anayemcha MwenyeziMungu zaidi.

Nae Katibu wa Mufti Sheikh Khalid Ali Mfaume amesisitiza haja kwa wananchi kumuombea dua Alhaj Dk. Mwinyi kutokana na mambo makubwa anayoyafanya na kuwataka wananchi kuithamini neema hiyo ya kupata kiongozi huyo bora.

Wakati huo huo, mara baada ya kumaliza Sala hiyo ya Ijumaa huko Bweleo Alhaj Dkt. Mwinyi alikwenda kumtembelea Rais Mstaafu wa Awamu ya Saba Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein huko nyumbani kwake Kibele, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi akimsalimia Rais Mstaafu wa Zanzibar Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, alipowasili nyumbani kwa Dk. Shein Kibele Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja kwa ajili ya kumsalimia.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Rais Mstaafu wa Zanzibar Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, alipowasili nyumbani kwa Dk. Shein Kibele Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja kwa ajili ya kumsalimia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news